Unavyoweza kuandaa mirathi mtandaoni kupitia akaunti ya kidijitali
- Ni kwa kutumia nyenzo maalum ya usimamiaji wa mirathi ya kimtandao.
- Hupunguza upotevu wa taarifa mtandaoni baada ya mtumiaji kufariki.
Dar es Salaam. Matumizi ya teknolojia na mtandao yamezidi kushika kasi siku za hivi karibuni yakiwawezesha watu kuwasiliana huku wengine wakiitumia kuhifadhi mambo muhimu ikiwemo nyaraka za kibenki, hati za nyumba na kumbukumbu za maisha yao.
Lakini umewahi kufikiria nini kitatokea kwa taarifa ulizohifadhi mtandaoni baada ya kifo chako?
Watu wengi wamekua wakiacha mirathi ya mali zinazohamishika na wanazomiliki kwa wanafamilia wao ili wafaidike lakini husahau kuacha urithi wa taarifa muhimu walizohifadhi mtandaoni kwenye mikono salama.
Leo tunaangazia umuhimu wa kuandaa mipango ya kuhifadhi taarifa zako za mtandaoni kwa watu unaowaamini kabla ya kufariki.
Jinsi ya kuandaa mirathi ya akaunti yako
Intaneti imeongeza wigo wa ufikiaji na matumizi ya huduma mbalimbali kidijitali kama miamala ya kifedha, hifadhi ya nyaraka muhimu, hati, picha na video ambazo zinaweza kuwa na faida kwa watu wa karibu utakaowaacha, Google inaweza kuwaruhusu kupata baadhi ya vitu hivyo endapo utaamua mapema.
Kupitia huduma ya akaunti ya google isiyotumika, unaweza kuamua kitakachotendeka mara tu akaunti yako inapoacha kutumika kwa muda uliouweka, kuliko kuzuia kabisa ikae kwenye seva bila kufikika na watu muhimu wanaosalia.
Kwanza andaa orodha ya akaunti zote unazomiliki zikiwa na majina na nywila zake, kisha chagua watu au mtu unayemwamini atakayekuwa na jukumu la kuzisimamia kisha ufuate vigezo vya sera ya urithi ya mtoa huduma.
Kabla akaunti yako kufungwa kwa kutotumika ni muhimu kuweka mpangilio (setting) ili kupata taarifa kupitia barua pepe na ujumbe mfupi wa simu.
Warithi wa taarifa zako ulizohifadhi mtandaoni lazima wathibitishe kupitia ujumbe mfupi (SMS) kabla hawajapewa ruhusa ya ufikiaji wa taarifa hizo, pia unaweza kuwatumia jumbe binafsi za alama za kidijitali za vidole vyako ili kurahisisha zoezi hilo.
Baada ya kuthibitisha mrithi atapata sms itakayomjulisha kupewa taarifa hizo na kiungo maalum (link) itakayomuwezesha kupakua taarifa zote ulizohifadhi.
Usipoacha urithi wa kidijitali, watu wako wa karibu watahitaji kuwasiliana na Google juu ya akaunti yako ili kuwafahamisha kuwa umefariki, sambamba na kuwapa uthibitisho wa kifo ili waruhusiwe kupata vitu maalumu utakavyokua umeruhusu wao kuvifikia kwa sababu hawataweza kufungua vitu vyote vya kwenye akaunti yako.
Faida za kuacha mrithi wa taarifa za mtandaoni
Kupanga urithi wa akaunti za kidijitali husaidia ulinzi wa taarifa kwa kuhakikisha kuwa picha au video za familia, mawasiliano muhimu na nyaraka za kifedha zinabaki salama za kuweza kupatikana kwa warithi wako.
Pia husaidia kuwapunguzia watu wako wa karibu mzigo wa kutafuta na kupata taarifa zako baada ya kifo chako sambamba na kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinatumika kulingana na matakwa yako.
Usikose sehemu ya pili ya makala hii ambapo tutaangazia jinsi unavyoweza kupata taarifa zilizohifadhiwa mtandaoni na ndugu, jamaa au rafiki aliyeaga dunia.