Fahamu vituo 9 maarufu kwa utalii Afrika.
- Ni pamoja na lango la jehanamu, kreta ya ngorongoro pamoja na mlima Kilimanjaro.
- Vivutio hivi ni fursa kwa nchi za Afrika kujiingizia mapato yatokanayo na utalii.
Dar es Salaam. Afrika ni miongoni mwa mabara yaliyobarikiwa vivutio vya utalii lukuki vinavyopendezesha na kuongeza mvuto katika nchi vilivyopo.
Vivutio hivi hufanya mamilioni ya watalii kutoka pande zote za dunia kutembelea bara la Afrika kila mwaka hususani katika kipindi hiki ambacho hatari dhidi ya janga la Uviko 19 imepungua katika nchi nyingi duniani.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) linasema kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024 Afrika imeweza kurudisha asilimia tano ya watalii waliokuwepo mwaka 2019 kabla ya kuingia kwa ugonjwa wa Uviko 19.
Hali hiyo inatoa hamasa kwa mataifa mbalimbali kuendelea kuboresha miundombinu na mandhari ya maeneo ya utalii ili kuweza kuvutia wageni wengi zaidi na hatimaye kukuza mapato ya nchi zao.
Nukta Habari imefanya uchambuzi wa vivutio tisa vya utalii unavyoweza kutembelea barani Afrika kama vilivyoanishwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA).
9. Lango la ‘Jehanamu’ Kenya.
Hifadhi hii ya kitaifa ya Lango la Jehanamu, yenye ukubwa wa eneo la takribani kilomita za mraba 68 ipo kilomita 90 kutoka makao makuu ya nchi ya Kenya Nairobi.
Hifadhi hii huwavutia watu kwa kuwepo kwa miamba mirefu na ndani ya mipaka yake imezungukwa na robo ya mifereji iliyoitiwa na bonde la ufa.
Pia hifadhi hii ina mandhari ya kuvutia ikiwa ni pamoja na miamba na minara mirefu, maporomoko ya maji, volkano zilizofunikwa na vichaka na mabomba ya mvuke na uwepo wa jotoardhi huifanya kuwa mojawapo ya mbuga za kuvutia zaidi barani Afrika.
Ukiwa katika hifadhi hii utafurahia kuona zaidi ya aina 103 za ndege wakiwemo tai wa ‘Verreaux’, ndege aina ya ‘Augur Buzzard’ na ‘Swifts’.
Mifereji inayoonesha kupitiwa kwa bonde la ufa | picha na BBC News Swahili.
8. Kreta ya Ngorongoro
Kwa mujibu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kreta ya Ngorongoro ndio kreta kubwa zaidi duniani, ikiwa na kina cha mita 610 na sakafu yake ina ukubwa wa kilomita za mraba 260.
Kreta hii inapatikana mkoani Arusha wilaya ya Ngorongoro na watu hupenda kuliita bonde hilo bustani ya edeni, hii ni kutokana na utulivu na hali ya hewa nzuri inayovutia wageni na wanyama mbalimbali kama vile pundamilia, tembo na wengine wengi.
7. Kisiwa cha Robben Afrika Kusini
Kisiwa cha Robben kipo kilometa 12 kutoka mji wa Cape Town Afrika kusini.
Kisiwa hiki ni moja ya kisiwa cha kale sana na chenye kuvutia kutokana na mandhari yake
Ukifika kisiwahi hapo utakaribishwa na ndege wakuvutia ambao huonekana katika makundi maeneo ya kisiwa hicho, pia utapata kuona majengo ya kale yaliyosanifiwa na mkoloni kwa ubora yaliyotumika kama magereza na sehemu ya kuhifadhia watu wenye ugonjwa wa ukoma.
Mbali na mandhari ya kuvutia kisiwa hicho kimebeba historia kubwa ya nchi ya Afrika Kusini kutokana na kutumika kama gereza la wahalifu wakati wa mkoloni huku Rais wa kwanza wa nchi hiyo Nelson Mandela akiwa miongoni mwa wa wafungwa katika eneo hilo kwa miaka 27.
Majengo ya Makumbusho ya Gereza la Robben Islad Afrika ya Kusini. | Picha na Aspire Life style.
6. Mbuga ya wanyama ya Taifa ya Ruwenzori-Uganda
Hifadhi hii inayopatikana pembezoni mwa mlima Rwenzoni magharibi mwa nchi ya Uganda ina eneo la kilomita za mraba 100,000 ikizungukwa na vilele vya milima vyenye barafu pamoja na maporomoko ya maji na maziwa ya kuvutia.
Ukiwa katika hifadhi hiyo pia utajionea mamia ya viumbe hai kama swala, punda milia wakijongea kwa mwendo wa taratibu utakaovutia macho yako.
5. Mbuga ya wanyama Bwindi – Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mbuga hii inapatikana mpakani mwa nchi ya Uganda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikichukua ukubwa wa takriban hekta 32,092, na ni mojawapo ya maeneo makubwa zaidi katika Afrika Mashariki.
Pia hifadhi hii ni maarufu hasa kwa kuwa na idadi kubwa ya jamii za sokwe wa milimani (mountain gorillas) ambao ni miongoni mwa wanyama waliopo hatarini kutoweka.
4. Maporomoko ya maji ziwa Viktoria – Zambia na Zimbabwe
Haya ni miongoni mwa maporomoko ya maji yenye kuvutia zaidi ulimwenguni. Mto Zambezi, ambao una upana wa zaidi ya kilomita mbili huporomoka kwa sauti ya kuvutia chini ya safu ya miinuko ya basalt na kusababisha ukungu unaoonekana zaidi ya kilomita 20.
Maanguko haya ya maji yana mipaka inayoenea zaidi ya hekta 6,860 na inajumuisha hekta 3,779 za Mbuga ya Kitaifa ya Mosi-oa-Tunya (Zambia), hekta 2,340 za Hifadhi ya Kitaifa ya Victoria Falls (Zimbabwe), hekta 741 za ukanda wa mto wa Hifadhi ya Kitaifa ya Zambezi (Zimbabwe).
Ukanda wa mto wa Hifadhi ya Kitaifa ya Zambezi unaoenea kilomita tisa magharibi kando ya ukingo wa kulia wa Zambezi na visiwa katika mto vyote viko ndani ya hifadhi hadi visiwa vya Palm na Kandahar, na maporomoko ya Victoria kuwa moja ya vivutio kuu.
3.Chemchemi za majimoto za Olkaria – Kenya
Kivutio hiki kipo karibu na Ziwa Naivasha katika bonde kuu la ufa nchini Kenya ambalo ni maarufu kwa kuwa na chemchemi za maji moto, kutoka ardhini.
Pia kivutio hiki kinatumika kuzalisha umeme unaokaridiriwa kufikia Megawati 2,000 ambao unatumika maeneo mbali mbali nchini Kenya.
2. Mlima Kilimanjaro – Tanzania
Kivutio hiki kinapatikana nchini Tanzania na ndio mlima mrefu zaidi katika bara la Afrika wenye urefu wa futi 19,341.
Mlima huu unapatikana mkoani kilimanjaro nchini Tanzania huku sehemu ndogo ya mlima huu ikipatikana nchini Kenya.
Huu ni moja ya mlima maarufu sana na unapenda kutembelewa zaidi barani Afrika ukivutia mamia ya watalii kuupanda kila mwaka kujionea kilele cha theluji, wanyama na milima.ya kibo na mawenzi inayopakana na mlima Kilimanjaro.
1. Uhamaji wa wanyama kati ya Mbuga za Wanyama Serengeti – Tanzania na Masai Mara Kenya
Uhamaji huu unahusisha kundi kubwa la wanyama ambao huhama kutoka mbuga ya Serengeti- Tanzania kuelekea Masai Mara- Kenya ambapo husafiri umbali wa takribani maili 500 sawa na zaidi ya kilomita 800.
Uhamaji Mkuu wa Serengeti huanza rasmi mwanzoni mwa mvua za masika, takribani mwezi wa Aprili. Nyumbu takribani 1,500,000 na pundamilia zaidi ya 200,000 pamoja na baadhi ya wanyama wengine kama swala huanza kuondoka katika maeneo ya kusini mwa Serengeti kuelekea kaskazini, wakipita katika hifadhi ya Ngorongoro, hifadhi ya Serengeti, na hatimaye kuvuka mpaka na kuingia Hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya.
Na mara mvua zinapoanza za mwezi Oktoba na Novemba basi wanyama hawa huanza safari ya kurudi tena katika mbuga ya Serengeti na kurudia tena mzunguko huo kila mwaka.