Hesabu bado mfupa mgumu matokeo kidato cha nne Tanzania

January 24, 2025 4:31 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu waendelea kuwa chini ya wastani kwa muongo sasa.
  • Wadau wa elimu wapendekeza matumizi ya mbinu shirikishi kuongeza ufaulu.

Dar es Salaam. Ufaulu wa somo la hesabu kwa wahitimu wa  kidato cha nne umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi hao huku takwimu mpya zikionyesha kuwa asilimia 25.35 tu ya watahiniwa wamefaulu somo hilo, ikiwa chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 50.

Hii inamaanisha kuwa takriban wanafunzi 75 kati ya kila 100 wamepata daraja la F katika somo hilo, hali inayozua mjadala kuhusu hali ya ufundishaji, uelewa na umuhimu wa somo hili.

Hesabu ni somo muhimu kwa maisha ya kila siku, likikuza uwezo wa kutatua changamoto, kufikiria kwa mantiki, na kufanya maamuzi bora. 

Hesabu inatumika katika mipango ya kifedha, sayansi, teknolojia, na maendeleo ya kiuchumi. Pia, huchangia katika ajira, ubunifu, na maendeleo ya jamii kwa jumla. 

Uelewa wa hesabu huimarisha ujuzi wa kitaaluma na kuboresha maisha ya mtu binafsi na jamii.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed, matokeo ya hesabu yanaonyesha kushuka kwa ufaulu ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo asilimia 25.42 ya wanafunzi walifaulu.

 “Ufaulu wa masomo yote umeimarika, isipokuwa kwa somo la Basic Mathematics, ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa miaka mingi,” amesema Dk. Mohamed alipokuwa akiwasilisha matokeo ya kidato cha nne 2024 jana Januari 23, 2025.

Takwimu za miaka 10 zilizopita zinaonesha kuwa, licha ya maboresho madogo, ufaulu wa hesabu umekuwa ukibaki chini ya wastani. 

Mathalani, mwaka 2015 ufaulu ulikuwa asilimia 16.76, na miaka iliyofuata uliongezeka kwa taratibu hadi asilimia 25.42 mwaka 2023, kabla ya kushuka tena mwaka huu.

Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari katika matokeo ya miaka mitano iliyopita unaonesha ufaulu wa somo la Hesabu kuwa chini ya wastani mara mbili zaidi ya wastani uliowekwa kitaifa.

Mathalani, kwa mwaka 2019 ufaulu ulikuwa 20.03, ambao uliongezeka kiduchu mwaka uliofuata na kufikia asilimia 20.12.

Ufaulu ilishuka mwaka 2021 mpaka asilimia asilimia 19.6 na kupanda kidogo mwaka 2022 hadi asilimia 21.1.

Mwaka  2023, ulipanda kwa asilimia nne mpaka asilimia 25.42 ambapo umeshuka tena mwaka huu.

Wataalamu wa elimu wanaeleza kuwa miongoni mwa changamoto kubwa ni mtaala wa hesabu ambao una mada nyingi za kiufundi ambazo haziendani na uwezo wa wanafunzi. 

Mwalimu Veronica Sarungi kutoka Shule ya Sekondari Aga Khan Mzizima ameiambia Nukta Habari kuwa mtaala wa sasa umeelemewa na mada zisizo na ulazima, kama vile Vector, ambazo ni ngumu kwa wanafunzi wengi.

Sarungi pia ameongeza kuwa, licha ya Serikali kupunguza idadi ya mada kwa baadhi ya madarasa, bado kuna changamoto ya uhaba wa walimu, hali inayochangia wanafunzi kutopata uangalizi wa karibu wanaohitaji. 

“Hesabu ni somo linalohitaji mwalimu awe karibu sana na mwanafunzi, na ukosefu wa walimu unazidi kufanya somo hili kuwa gumu zaidi,” aliongeza Sarungi.

Hata hivyo, Sarungi ambaye amewahi kuwa mwanafunzi bora wa kidato cha nne mwaka 1989 ametoa wito kwa walimu kuongeza juhudi za kuondoa daraja la F kwa wanafunzi wote, badala ya kuwekeza juhudi kwa kundi dogo linaloweza kupata daraja A kwa ajili ya zawadi.

Amehimiza wazazi na jamii kwa ujumla kutowachukulia kawaida wanafunzi wanaofeli hesabu, badala yake wawasaidie kwa kuwapa msaada wa ziada hata kama hawajui somo hilo.

“Tunapaswa kutumia vipindi vya mtandaoni na mbinu za kisasa za kufundishia ili kuwafanya wanafunzi wapende hesabu. Pia, wazazi na walimu wanapaswa kushirikiana badala ya kurushiana lawama,” amesisitiza Sarungi.

Lishe ya binadamu yawatoa kimasomaso

Wakati Hesabu ikiendelea kuwatesa watahiniwa, somo la Chakula na Lishe ya Binadamu limeonesha mafanikio makubwa, likiwa na ufaulu wa asilimia 100.

Hii inaonyesha kuwa, kwa juhudi za pamoja na mabadiliko ya kimkakati, inawezekana kuboresha matokeo ya masomo mengine, ikiwemo hesabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks