Njia za kumsaidia mtoto wako kupenda hisabati

May 6, 2025 4:42 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kumpongeza na kumnunulia vitabu na programu za kielimu.
  • Mueleze mtoto umuhimu wa hisabati katika maisha yake ya kila siku.

Dar es Salaam. Somo la hisabati limekuwa kama ugonjwa usio natiba kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali za elimu nchini Tanzania. 

Hili limekuwa likijidhirisha katika matokeo ya mitihani ya kitaifa. Ufaulu wa wanafunzi katika somo hili umekuwa wa chini zaidi kuliko masomo mengine. 

Mathalani, katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024 yaliyotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), ni asilimia 25.35 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa hisabati, ndio walifaulu kwa kupata daraja A hadi D. 

Hiyo ni sawa kusema karibu robo tatu (wanafunzi 7 kati ya 10) walifeli somo hilo. Pia umefaulu huo wa mwaka jana umeshuka kutoka asilimia 25.42 iliyorekodiwa mwaka 2023. 

Suala hili la kufanya vibaya kwa wanafunzi katika somo la hisabati, limekuwa likiibua maswali mengi yasiyo na majibu miongoni mwa wazazi, walimu na wadau wa elimu. Baadhi ya wadau wanapendekeza uitishwe mjadala wa kitaifa kutafuta suluhu ya kudumu kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika soko hili. 

Mchambuzi wa masuala ya elimu na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amewahi kuiambia Nukta Habari (nukta.co.tz) kuwa suluhu ya pamoja itakayohusisha makundi yote kwenye jamii, inaweza kutoa mwelekeo mpya wa hisabati na kuwafanya wanafunzi wengi walipende somo hilo. 

Wadau wengine wa elimu wanasema mbinu shirikishi za ufundishaji zinaweza kusaidia wanafunzi kupenda somo hilo. 

Picha hii imetengenezwa kwa Akili Unde ikiwa lengo ni kukuonyesha namna unavyoweza kushirikiana na mwanao kuhakikisha anaelewa soma la hesabu.

Mwalimu wa hisabati kutoka Shule ya Sekondari Aga Khan Mzizima jijini Dar es Salaam, Veronica Sarungi, anasisitiza kuwa inawezekana kumfanya mwanafunzi kupenda hisabati kwa kutumia mbinu sahihi ikiwemo kutokumkatisha tamaa mtoto pale anapokuwa amefanya vibaya katika somo hilo. 

Ni kawaida kwa wazazi, walimu na hata wanafunzi wenzao kuwatisha watoto kwa kauli kama “Hisabati ni ngumu” au “Wewe huwezi hesabu.” 

Mwalimu Veronica anasema kauli hizo zina athari mbaya kwa watoto, kwani huwafanya kujiwekea vikwazo vya kisaikolojia na kuamini kuwa hawana uwezo wa kufanikisha somo hili. 

Badala ya kuwatia hofu, ni muhimu kuwahamasisha watoto kwa kuwatia moyo hata wanapokosea.

“Kwa mfano, mzazi au mwalimu anaweza kumwambia mtoto kuwa makosa ni sehemu ya kujifunza na mafanikio yanapatikana kwa kufanya mazoezi. Hili litawapa wanafunzi ujasiri wa kukabiliana na changamoto za somo hili bila woga,” anasema Mwalimu Veronica. 

Pia wape watoto changamoto ndogo ndogo wanazoweza kuzitatua kwa urahisi. Hii itawasaidia kuona hisabati sio somo gumu kama wanavyodhani au kuaminishwa. 

Mtaalam huyo wa hesabu anawashauri walimu wanaofundisha somo hilo kutumia mbinu za kisaikolojia zinazosaidia kujenga ujasiri wa wanafunzi. 

Mbinu rahisi kama kuanzisha maswali ya msingi, kuelezea dhana kwa njia ya mfano, na kuwapongeza kwa juhudi zao zinaweza kubadilisha mtazamo wao kuhusu hisabati.

Tumia mfano wa maisha halisi

Hisabati ipo kila mahali katika maisha yetu ya kila siku, na njia moja ya kumfanya mtoto aipende ni kuhusianisha somo hili na mazingira yanayomzunguka. 

Kwa mfano, mzazi anaweza kumwonyesha mtoto jinsi ya kuhesabu fedha anaponunua vitu dukani, kupanga bajeti ya matumizi ya nyumbani, au hata kupima vitu kama urefu na uzito.

Mfano mwingine ni michezo rahisi ya namba. Watoto wengi hupenda kucheza, na kwa kutumia michezo inayojumuisha hesabu, unaweza kuwafanya wajifunze kwa furaha.

Watoto wengi hupenda kucheza na kwa kutumia michezo inayojumuisha hesabu husaidia kuwajengea kumbukumbu nzuri kichwani. Picha/ Akili unde.

Hii huwasaidia kuelewa kuwa hisabati si somo la darasani tu bali ni ujuzi wa maisha ambao kila mtu anahitaji.

Pia katika shughuli za kila siku, mzazi anaweza kumuuliza mtoto maswali rahisi ya kihisabati kama, “tuna vijiko 10, tukiondoa viwili, vitabaki vingapi?”. 

Kwa njia hii, mtoto anapata fursa ya kujifunza hisabati kwa vitendo, jambo linalowafanya kuona somo hili kuwa la kufurahisha na linalotumika kila siku.

Nunua vitabu na programu za hisabati

Vitabu vya mazoezi ya hisabati ni nyenzo muhimu ya kujifunza, hasa kwa watoto wanaopenda kujifunza wakiwa nyumbani. 

Vitabu hivi vina maswali ya ngazi mbalimbali, kuanzia maswali rahisi hadi magumu, ambayo yanaweza kumsaidia mtoto kukuza maarifa yake hatua kwa hatua. 

Kwa mfano, vitabu vya watoto wa shule za msingi vinaweza kuwa na michoro na mifano ya kuvutia inayorahisisha uelewa wa dhana za msingi.

Uwepo wa vitabu mbalimbali humsaidia mtoto kuwa na uwezo wa kufanya maswali mengi kutoka kwenye vitabu tofauti. Picha/ Canva.

Kwa upande wa teknolojia, mzazi anaweza kutumia simu janja au kompyuta kuhamasisha mtoto kujifunza kupitia programu za kielimu.

Kuna programu nyingi za bure zinazopatikana mtandaoni ambazo zina michezo na maswali yanayofundisha hisabati kwa njia za kuvutia. 

Michezo kama hii inachochea ubunifu na hamasa kwa watoto, kwani wanajifunza kwa kucheza badala ya kuhisi wanalazimishwa.

Mbali na teknolojia, wazazi wanaweza kutumia majukwaa kama YouTube ambapo walimu wa hisabati huchapisha video za elimu. 

Video hizi zinaweza kuwa msaada mkubwa kwa watoto wanaopenda kujifunza kwa njia ya kuona, na zinawapa nafasi ya kurudia masomo mara kadhaa hadi waelewe kikamilifu.

Toa zawadi kwa mtoto akifanya vizuri

Kwa mfano, mzazi anaweza kumwekea mtoto changamoto ndogo, kama kumaliza maswali 10 ya hisabati, na kumpa zawadi endapo atamaliza kwa usahihi. 

Kulinganana tovuti ya Mrs Mayers Leaning Lab, watoto wanahamasika zaidi wanapopewa zawadi au pongezi kwa juhudi zao. 

Zawadi hizi zinaweza kuwa za vifaa kama kalamu, daftari, au hata vitu vidogo wanavyopenda, au maneno ya kuwahamasisha kama “Umefanya vizuri sana leo.”

Hii huwafanya watoto kuona hisabati kama mchezo wa kufurahisha unaowapa zawadi badala ya mzigo wa kimasomo unaowakandamiza.

Zawadi ni kitu kinachopendwa na kila mtu hivyo kumpa mtoto zawadi baada ya kufanya vizuri itamfanya kuongeza jitihada zaidi. Picha/ Canva.

Zaidi ya hayo, zawadi hizi huchochea ushindani wa afya ya akili miongoni mwa wanafunzi wa darasa moja au familia moja. 

Watoto wanapojua kuwa juhudi zao zinathaminiwa, wanakuwa na hamu zaidi ya kujifunza na kushinda changamoto nyingine. Hii huwasaidia kujiamini zaidi na kuona hisabati kama somo linalowezekana.

Michezo ya hisabati

Michezo ya namba ni njia bora ya kuwafanya watoto kushiriki kikamilifu katika kujifunza hisabati. 

Kwa mfano, michezo kama sudoku, ‘bingo’ ya namba, au kutafuta mifumo ya namba husaidia watoto kuboresha uwezo wao wa kufikiri.

Wakati wa kucheza, mzazi au mwalimu anaweza kuelezea dhana za hisabati zinazojitokeza kwenye mchezo husika, kama vile kujumlisha, kutoa, kuzidisha, au kugawanya.

Kwa kutumia michezo mbalimbali kunaweza kumsaidia mtoto kuwa na kumbukumbu za muda mrefu. Picha/ Canva.

Hii huwafanya watoto kuelewa kuwa hisabati si tu namba za kubahatisha bali ni somo linalohitaji mbinu na mikakati.

Michezo inayohusisha mashindano huwafanya watoto kuwa na hamu zaidi ya kushiriki. Wanafurahia changamoto wanapojaribu kuwashinda wenzao, huku wakiwa wanajifunza hisabati kwa vitendo. Kwa njia hii, hisabati inakuwa somo la kufurahisha na linalochochea maarifa mapya.

Tumia vifaa vya kuonyesha na vitu halisi

Watoto huelewa vizuri zaidi wanapofundishwa kwa kuona vitu halisi. Kwa mfano, walimu na wazazi wanaweza kutumia maharage, sarafu, au vijiti vya plastiki kufundisha dhana kama kuhesabu, kujumlisha, au kugawanya.

Mbali na vitu vya asili, chati na michoro pia ni nyenzo bora za kufundishia. 

Hii huwafanya watoto kuelewa dhana ngumu kwa urahisi zaidi ukilinganisha na njia za kawaida. Picha/ Canva.

Chati zinaweza kusaidia kuelezea mifumo ya namba, kama vile jedwali la kuzidisha, huku michoro ikielezea dhana za kijiometri kama pembe, mistari, na maumbo. Hii huwafanya watoto kuelewa dhana ngumu kwa urahisi zaidi.

Hii itawasaidia watoto kufikiri kuwa hisabati ni somo la vitendo na siyo nadharia pekee.

Anzisha mashindano ya hisabati

Mashindano ya hisabati ni njia nzuri ya kuwafanya watoto kujifunza kwa njia ya ushindani. 

Mashindano haya huwapa watoto nafasi ya kuonyesha maarifa yao, kujifunza kutoka kwa wenzao, na kupata hamasa ya kushinda zawadi au kutambuliwa.

Kwa mfano, kuna mashindano ya hisabati yanayoandaliwa na shule, vyuo, au taasisi za elimu, ambapo wanafunzi hushindana kutatua maswali ya hesabu kwa muda mfupi. Watoto wanaposhiriki katika mashindano haya, wanajifunza kushughulikia changamoto kwa haraka na kwa usahihi.

Kwenye mashindano siku zote kila mtu huwa na shauku ya kushinda hivyo na kwa watoto ushindani huwapa hamu ya kuwa bora zaidi. Picha/ Canva.

Kupitia mashindano haya, watoto hupata uzoefu wa kushirikiana na wenzao, jambo linalowasaidia kuboresha ujuzi wa kijamii na kuimarisha hamasa yao ya kujifunza. 

Wazazi wanashauriwa kuwatafutia watoto wao mashindano yanayofaa kulingana na umri na uwezo wao.

Elezea umuhimu wa hisabati katika maisha

Watoto mara nyingi huona hisabati kama somo lisilo na faida ya moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku. 

Kwa kubadilisha mtazamo huu, mzazi au mwalimu anaweza kuwaonyesha umuhimu wa hisabati kwa kuelezea jinsi inavyotumika katika kazi mbalimbali kama biashara, uhandisi, sayansi, na hata burudani.

Kwa mfano, msanii wa muziki anahitaji hisabati ili kupanga bajeti ya muziki wake, huku mwanamichezo akitumia hisabati kupima muda na umbali wa mazoezi yake. 

Ni vyema kuwajengea uwezo wa kujitambua mapema watoto ili kadri wanavyokuwa wasione hesabu kama janga la Taifa. Picha/ Akili Unde.

Hii inawafanya watoto kuona hisabati kama nyenzo ya kufanikisha ndoto zao za maisha.

Kuelezea jinsi hisabati inavyotumika kusimamia fedha, kupanga ratiba, au hata kupima afya kunawapa watoto mtazamo wa kivitendo kuhusu somo hili. 

Matokeo yake ni kwamba wanajifunza kuipenda hisabati kwa sababu wanaona thamani yake katika maisha yao ya kila siku.

Kwa kutumia mbinu hizi, mzazi au mwalimu anaweza kubadilisha mtazamo wa mtoto kuhusu hisabati na kumfanya aipende na kuimudu kwa urahisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks