Jinsi Tanzania itakavyoathirika na sitisho la misaada ya Marekani
- Ni pamoja na sekta za elimu, afya, uwezeshaji wa vijana, ukuaji wa uchumi, utawala bora, na usimamizi wa mazingira.
- Wadau wataka hatua za haraka zichukuliwe kuepusha athari kubwa zaidi hususan katika sekta ya afya.
Dar es Salaam. Taifa la Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), limesitisha utoaji wa misaada kwa kipindi cha siku 90 ili kupisha uhakiki wa programu za misaada hiyo kwa mataifa ya kigeni.
Baada ya kuapishwa kwa muhula wake wa pili Januari 20, 2025, Rais Trump alitoa amri ya kusitisha misaada ya maendeleo ya kigeni kwa muda wa siku 90 ili kufanya tathmini ya ufanisi wa misaada hiyo na kuhakikisha inalingana na sera yake ya kigeni.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Donald Trump za kuweka mbele maslahi ya Marekani kupitia sera yake ya ‘Make America Great Again.
Kwa mujibu wa Muhtasari wa Mradi wa USAID Tanzania, ndani ya miongo miwili iliyopita, USAID imechangia Tanzania ufadhili wa zaidi ya dola bilioni 7.5 za Marekani, sawa na shilingi trilioni 19 za Tanzania.
Kusitishwa kwa misaada hiyo kunaweza kuathiri sekta muhimu zilizobainishwa katika Mkakati wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Nchi (CDCS) wa 2020-2025, zikiwemo elimu, afya, uwezeshaji wa vijana, ukuaji wa uchumi, utawala bora, na usimamizi wa mazingira.
Misaada kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Ukimwi (PEPFAR), ambao umechangia pakubwa kupambana na maambukizi ya HIV/AIDS, ni miongoni mwa programu zitakazoathirika.
Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia Lusungu Mubofu amesema kusitishwa kwa misaada hiyo kunaweza kuleta athari kubwa hasa kwa sekta za kijamii kama afya ikiwa hakutakuwa na njia mbadala ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma na bidhaa zilizoathirika na kusitishwa kwa misaada.
Hata hivyo, Mubofu ameongeza kuwa kusitishwa kwa misaada hakutamaliza kabisa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania.
“Uhusiano utaendelea kwa masuala ya msingi, lakini hatua hii italeta changamoto kubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” ameeleza Mubofu.
Kwa upande wake Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof Anna Tibaijuka, kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), ameonya kuwa kusitishwa kwa misaada ya mashirika ya kimataifa kama PEPFAR na Global Fund kutahatarisha upatikanaji wa dawa muhimu za ARVs kwa waathirika wa HIV/AIDS.
Prof Tibaijuka ameisihi Wizara ya Afya kueleza hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na changamoto hiyo na kutoa wito kwa Umoja wa Afrika kuandaa mkakati wa pamoja.
“Aidha, juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi ziwekewe nguvu mpya. Upatikanaji wa ARVs utakuwa mgumu, na kununua dawa hizo kibiashara kutahitaji bajeti kubwa ambayo hatuna kwa sasa,” ameandika Prof Tibaijuka.
Kwa upande mwingine, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza wasiwasi mkubwa kupitia Mkurugenzi wake Mkuu, Tedros Ghebreyesus, juu ya athari za kifedha zitakazotokana na uamuzi huu.
Latest



