Kwa nini wananchi hawa wanaoishi kando ya Ziwa Victoria wanakabiliwa na uhaba wa maji?
- Ni baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mwanza ambao hulazimika kutembea zaidi ya saa moja kutafuta maji.
- Wanapata maji kwa mgao baada ya mashine ya kusukumia maji kuharibika.
- Serikali yaingilia kati yataka wapatiwe maji ya uhakika kabla ya Desemba 2022.
Mwanza. Kila anapohitaji maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, Agnietha Marco (38) hulazimika kutenga zaidi ya saa moja kwenda kuteka maji kwenye kituo cha jirani licha kuwa anaishi kilomita chache tu kutoka Ziwa Victoria.
Mama huyo, mwenye watoto watatu, anayeishi mtaa wa Buhongwa Amani jijini Mwanza, anasema kitendo hicho cha kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kusaka maji kumemkwamisha kutekeleza majukumu yake ya ujasiriamali na yale ya familia kwa wakati.
Katika mtaa wao wa Buhongwa, Agnietha ambaye ameishi hapo kwa miaka mitano sasa anasema upatikanaji wa maji huwa mgumu hususan kipindi hiki cha kiangazi ambapo maji hutoka mara moja kwa wiki au baada ya wiki mbili.
“Pale maji yanapotoka hayakai (hayatoki) muda mrefu, yanaweza kukaa siku moja au mbili yanakatika, changamoto hii inasababisha hata wanafunzi washindwe kufua sare zao za shule kutokana na kukosa maji,” anasema Agnietha.
Pamoja na kutembea mwendo huo wa saa moja bado maji hayo huyanunua kati ya Sh100 au Sh200 kwa ndoo ya ujazo wa lita 20. Iwapo atahitaji maji hayo karibu na nyumbani, atahitaji kutumia wastani wa Sh500 hadi Sh600 kwa dumu la lita 20 kutoka kwa vijana wanaosambaza maji kwenye mikokoteni au bajaji.
Uhaba wa maji, hasara kubwa
Changamoto hiyo ya maji haijamwathiri Agnietha pekee katika masuala ya nyumbani bali hata wajasiriamali wengine wanaotumia zaidi maji katika kutengeneza bidhaa au kutoa huduma wakiwemo mama lishe.
Baadhi wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kwamba maji yakikosekana kwa muda mrefu biashara zao huyumba na kuhatarisha mwenendo wa kipato chao kinachotumika kuendesha familia zao.
Jackline Juma, Mama lishe mtaa wa Buhongwa Mashariki anasema ukosefu wa maji huchelewesha wateja wake kupata chai na chakula kwa wakati na huongeza gharama za kuandaa chakula kwa kuwa hununua maji kwa bei ya juu.
“Kwetu uhaba wa maji ni tatizo kubwa hivyo tunaiomba Serikali itusaidie kuleta maji kwenye maeneo yetu ya miinuko ili tupate ya uhakika kupunguza changamoto hizi,” anasema Jackline.
Maeneo mengi ya Mwanza iliyopo pembezoni mwa ziwa kubwa zaidi Afrika, Ziwa Victoria yapo kwenye miinuko au vilima na kufanya upatikanaji wa visima vya kawaida kuwa tatizo kubwa.
Kisima kilichopo Buhongwa mkoani Mwanza ambacho hakitoi maji. Katika eneo hilo watu hulazimika kutembea umbali wa saa maoja kuyasaka maji kwa shughuli za nyumbani. Picha | Mariam John.
Kwa nini uhaba wa maji kilomita 16 tu kutoka ziwani?
Licha ya Buhongwa wanapoishi Jackline na Agnietha ni kilomita 16 tu kutoka ziwani bado mtandao wa maji si wa uhakika kwa miaka yote ambayo wamekuwa wakiishi hapo.
Hivi sasa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maji Mkoa wa Mwanza unazalisha lita milioni 90 za maji ambazo zinasambazwa kwenye maeneo yote ya jiji la hilo.
Mahitaji ya maji kwa mkoa huo ni lita za maji milioni 160 hivyo kuwa na upungufu wa lita za maji milioni 70. Hii ina maana kuwa wakazi wa mkoa huo wa kanda ya ziwa wanapata zaidi ya nusu au takriban asilimia 56 ya mahitaji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Hamis Mijie anasema hali ya upatikanaji wa maji kwenye mtaa wake si ya kuridhisha kwa kuwa maji yanatoka mara moja kila baada ya wiki moja au mbili.
Anasema hivi sasa tatizo ni kubwa hasa baada ya mashine za kusukumia maji za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kuharibika ambapo maji yamekuwa ya mgao na yanachukua muda mrefu kutoka.
‘Wanaishi kwa kubangaiza’
“Kifupi wanaishi kwa kubagaiza si wale wanaofanya miradi ya ujenzi, mama lishe na hata watu wa kawaida ambapo wanalazimika kutafuta maji umbali mrefu au kununua kwa wanaouza ambao huyafuata sehemu nyingine,” anasema Mijie.
Wakazi hawa wameshuhudia miradi mikubwa ya maji ikitoa maji Ziwa Victoria na mingine inayojengwa katika maeneo yao ikichelewa kuwafikia.
Mijie anaiomba Serikali kuhakikisha miradi ya maji inayojengwa jijini Mwanza inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto iliyopo kwa wananchi.
Hadi sasa matumaini ya wakazi hawa yapo katika mradi mpya ujenzi wa chanzo kipya maji na tiba kinachojengwa Butimba jijini Mwanza ambacho kitasaidia kupeleka maji maeneo ya pembezoni mwa miji na yenye miinuko ikiwemo Buhongwa.
Soma zaidi:
- Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 1
- Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi
- Simulizi ya familia, nyumba zilizozingilwa na maji ya Ziwa Victoria
Nuru ya matumaini
Mradi huo unaojengwa na Serikali kwa kushirikiana na wabia kutoka Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (EIB) na Shirika la AFD, kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo, unatarajia kukamilika Februari mwaka 2023 na kunufaisha wakazi zaidi ya 450,000.
Miongoni mwa maeneo yatakayofikiwa na mradi huo ni pamoja Nyegezi, Buhongwa, Mkolani, Lwanima, Fumagila, Sawa, Igoma, Kishiri na Nyamhongolo, Usagara na Nyashishi wilayani Misungwi
Maeneo mengine ambayo mradi huo utayahudumia iwapo utakamilika kwa wakati na kutoa huduma kama ilivyopangwa ni Fela, Bujora na Isagijo wilayani Magu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Antony Sanga anasema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 95 kuweka zege na kilichobaki ni kazi ya kuweka umeme ili mradi uanze kufanya kazi.
Anasema mradi huo ni mahususi kwa ajili ya kupeleka maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji lakini pia maeneo ambayo hayafikiwi na maji kutokana na kuwa na miinuko.
“Mradi unatekelezwa kwa gharama za zaidi ya Sh69.3 bilioni na miongoni mwa miradi ya maji inayotekelezwa ndani ya Ziwa Victoria ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa maji kwenye maneo hayo,” anasema Sanga.
Tangazo:

Hapana, zege lisilale mwaka huu
Hata hivyo, kutokana na uhaba wa maji kukithiri katika eneo hilo, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango baada ya kuweka jiwe la Msingi kwenye chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba alitaka mradi ukamilike ifakapo Desemba 2022 na si Februari 2023 kupunguza maumivu zaidi kwa wakazi hao.
Katika hotuba hiyo, Dk Mpango alisema si jambo jema watu wanaokaa karibu na ziwa kubwa Afrika kukosa huduma ya uhakika wa maji.
Yale ambayo Nukta Habari ilibaini katika baadhi ya mitaa ya pembezoni mwa jiji la Mwanza kabla ya uzinduzi wa chanzo hicho cha maji ndiyo pia aliyofikishiwa kiongozi wa pili wa juu nchini.
“Nilipokuwa nazindua stendi ya mabasi Nyamhongolo jana nilipokea kero na kelele nyingi za uhaba wa maji hivyo naomba wananchi wapate zawadi ya Krismasi kwa kuwa na maji ya uhakika,” alisema Dk Mpango.
Baadhi ya wanawake wa Buhongwa mkoani Mwanza wakitembea kufuata maji umbali wa saa moja, licha ya kuishi karibu na Ziwa Victoria. Picha | Mariam John.
Kufa kufaana
Wakati Serikali ikiendelea kutatua tatizo la uhaba wa maji mkoani Mwanza kwenye maeneo yenye miinuko, baadhi ya vijana hapa wamegeuza shida hiyo kuwa fursa.
Michael Joshua, mkazi wa Mtaa wa Sawa jijini Mwanza anasema kwa siku anaingiza kati ya Sh10,000 hadi 20,000 kwa kusambaza maji kwa wakazi wa eneo hilo wanaohaha kupata huduma hiyo kwa wakati.
Kwa kutumia mkokoteni wake hupanga madumu saba hadi nane na kuwapelekea wateja wake wa nyumbani na hotelini.
Anasema dumu moja la lita 20 huuza kati ya Sh500 na wakati mwingine Sh600, na inategemea na upatikanaji wa maji kwa siku hiyo na kwamba yeye huuziwa Sh100 hadi 200 kwa dumu moja.
“Faida yangu ni kidogo sana ni Sh300 kwa dumu moja na inapotokea nimesambazia wateja watano hadi 10 kwa siku ndio napata angalau kifedha cha kutumia,” anasema Joshua.
“Wasiwasi wangu ni kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo wa maji nitakosa ajira ya kulisha familia yangu.”
Kutokana na tatizo la uhaba wa maji, baadhi ya vijana wanaitumia fursa hiyo kuyasaka maji na kuyauza mtaani. Picha | Mariam John.
Latest