Simulizi ya familia, nyumba zilizozingilwa na maji ya Ziwa Victoria

March 11, 2021 11:32 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mwonekano wa maji yalivyozingira nyumba katika mtaa wa Ziwa kufuatia mvua zilizonyesha mwaka mmoja uliopita na kusababisha kina cha ziwa victoria kuongezeka. Picha| Mariam John.


  • Ni nyumba tatu kati ya nyumba 43 zilizopo kando ya Ziwa Victoria katika mtaa wa Ziwa jijini Mwanza kuzingilwa na maji baada ya mvua kubwa mwaka 2020. 
  • Familia hizo zinapitia kipindi kigumu kutokana hatari ya magonjwa inayowakabili.
  • Wataalam wa afya washauri familia ziondoke eneo hilo. 

Mwanza. Ni takribani miezi 15 sasa toka nyumba 43 zilizopo kando ya Ziwa Victoria katika mtaa wa Ziwa jijini Mwanza kuzingilwa na maji kutokana na kina cha maji cha ziwa hilo kuongezeka.

Kuongezeka kina cha maji cha ziwa hilo maarufu Afrika hasa katika mtaa huo, kumetokana na mvua kubwa iliyonyesha ukanda wa Ziwa ambapo ilisababisha athari mbalimbali ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu zikiwemo nyumba. 

Wakati wakisubiri maji yapungue ili warudi katika makazi yao ya awali, ni familia za nyumba tatu kati ya 43 ndiyo zinaendelea kuishi katika eneo hilo, licha ya changamoto ya maji iliyopo.

Familia hizo zimeendelea kukaa katika hilo kutokana na kukosa maeneo mengine ya kuishi,  licha ya mamlaka kuwatahadharisha kuwa siyo sehemu salama ya kuishi kwa sasa. 

Clereonsia Marko ni mkazi wa mtaa wa Ziwa anasema hali ya kiuchumi imesababisha kuendelee kubaki hapo na hana jinsi zaidi ya kukabiliana na changamoto zinazomkabili. 

“Kipato ni kidogo hatuwezi kupanga chumba cha gharama, familia ni kubwa lakini  licha ya changamoto zote hizo  inatulazimu kuendelea kuishi hapa,”anasema Clereonsia

Vitanda wanavyolalia wamelazimika kuviweka juu ya matofali, huku wakitumia mbao zilizopangwa juu ya matofali ili kuwarahishia njia ya kuingia katika nyumba zao na kuepuka maji yaliyowazunguka.

Ukifika maeneo hayo, njia zote zimepangwa mifuko ya saruji iliyojazwa mchanga, matofali au mbao zinazowasaidia kufanya mihangaiko ya hapa na pale.

 Baadhi ya nyumba katika mtaa wa Ziwa zikiwa zimezungukwa na maji karibu na Ziwa Voctoria. Picha| Mariam John.

Wanyama kama nyoka, kenge na mamba imekuwa kawaida kupishana nao huku adha kubwa inayowatesa ndani ya mwaka mmoja huo ni ukosefu wa vyoo baada ya vilivyokuwepo kujaa maji.

“Ni kinyaa sana hususan nyakati za usiku wakati ukirudi kutoka matembezini unakuta maji  yanaingia ndani, uchafu wa kila aina huingia, hali inayosababisha kuhamisha vitu kutoa nje, hii ni kero kubwa sana,” anasema Severin John, mmoja wa watu wanaoishi katika nyumba hizo. 

Wanasema wanalazimika kwenda kwa majirani sehemu ya miinuko kujisaidia na wakati mwingine hasa nyakati za usiku hujisaidia ndani ya ziwa.

Kwa watoto, tatizo la mafua na shida ya upumuaji imekuwa ni kawaida kutokana na kupata hewa chafu inayosababishwa na mazingira yasiyoridhisha. 

Changamoto nyingine wakazi hao kusumbuliwa na fangasi miguuni kutokana na kukanyanga maji mara kwa mara huku mazingira wanayoishi yakiwa yamezungukwa na takataka za kila aina.

Kina cha maji kilivyoacha maumivu ya kiuchumi

Baadhi ya nyumba za eneo hilo zilikuwa ni sehemu ya wamiliki kujipatia kipato kutokana na makusanyo ya kodi kutoka kwa wapangaji waliopanga kwenye nyumba zao.

Suzan Butondo ni mmoja wa waathirika katika eneo hilo anasema kila baada ya miezi mitatu au sita alikuwa anapata fedha za kodi ya nyumba.

“Nimerudi nyuma kiuchumi, tegemeo langu ni kufanya vibiashara vidogo vidogo,  nguvu nilizowekeza hapa na fedha zote zimepotea na sasa kilichobaki ni kutafuta namna ya kubomoa kuchukua milango na madirisha,” anasema Suzan ambaye nyumba yake iko kwenye maji.


Soma zaidi: 


Ni nini kifanyike?

Hata hivyo, kuendelea kuishi kwa familia hizo katika eneo hilo kunawaweka katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya malaria, kichocho kuhara kwa sababu maji yametuhama na yanazalisha vijidudu vya magonjwa.

Dk Frank Minja kutoka Shree Hindu Mandal Hospital ya mkoani Dar es Salaam amesema maeneo hayo ni hatari kwa sababu ni chanzo kikubwa cha mazalia ya mbu na vimelea vingine vya magonjwa ambavyo vinaweza kuathiri za afya za watu.

“Njia rahisi ni kuondoka maeneo hayo au kutafuta ya kuyafanya maji yasituame na yaelekezwe kwenda maeneo mengine ya mabwawa au mifereji,” anasema Dk Minja. 

Wakizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz) kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi katika eneo hilo wanaiomba Serikali kuangalia eneo la kuwahamisha ili kuondokana na adha wanayoipata kwa sasa. 

Ili kuingia ndani, wakazi hao wanapita juu ya mbao na matofali ili kukwepa maji ambayo yamezingira nyumba za eneo hilo. Picha| Mariam John.

Mwenyekiti wa mtaa wa Ziwa, Abeid Mohamed anasema nyumba 43 zilizozingilwa na maji na kusababisha wakazi kuyakimbia maeneo yao kwenda kuhifadhiwa kwa ndugu jamaa na marafiki.

Mwenyekiti huyo anaiomba Serikali kuangalia namna ya kuwahamisha watu waliobaki kwenye nyumba hizo ambazo ni hatari lakini pia kufanya tathmini ili walipwe fidia.

“Hakuna vifo vilivyotokea isipokuwa watu wamepoteza vitu vingi vilivyoenda na maji, nyumba zao kuanguka huku baadhi zikiwa zimejaa maji,” anasema mohamed wakati akiongea na www.nukta.co.tz

Anasema wapo waliojaribu kurudi lakini wengine hawajafanikiwa  kabisa kuishi katika eneo hilo huku wakiwa na matumaini ipo siku moja watarejea. 

Huenda matumaini waliyonayo kurudi katika eneo hilo yasitimie kwa sababu wataalam wa masuala ya maji wanaeleza kuwa itachukua muda mrefu kwa kina cha maji katika ziwa hilo kupungua.

Huenda hali hii ikawa ya muda mrefu, kutokana na uchunguzi uliofanywa na Bonde la Ziwa Victoria limebaini kina hicho cha maji hakiwezi kupungua leo ama kesho.

Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Gerlad Itimbula anasema hakuna uwezekano wa kina hicho cha maji kupungua kwa haraka hivyo ni vyema wakazi wa maeneo hayo wakatafuta sehemu nyingine ya kuishi.

Enable Notifications OK No thanks