Kitendawili: Mtaa unaomezwa na maji Ziwa Victoria
Mwonekano wa nyumba katika Mtaa wa Ziwa kufuatia mvua zilizonyesha mwaka 2020 uliopita na kusababisha kina cha Ziwa Victoria kuongezeka. Picha| Mariam John.
- Watu wazikimbia nyumba zao, zageuka makazi ya wanyama.
- Matumaini ya kupungua kwa kina cha maji yayeyuka.
- Wadau washauri kuzingatia sheria za mazingira kuepuka madhara.
Mwanza. Bado ana matumaini kuwa ipo siku hali itarejea kama ilivyokuwa awali. Awe na huru wa kutembea na kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi.
Huenda matumaini hayo yasitimie kama anavyotarajia kwa sababu hayako ndani ya uwezo wake.
Ni Everina Mussa, mkazi Mtaa wa Ziwa jijini Mwanza. Mtaa huo uliofurikwa na maji ya Ziwa Victoria baada ya kuongezeka kwa kina cha maji cha ziwa hilo yaliyoingia katika makazi ya watu.
Licha ya wenzake kuhama katika eneo hilo tangu mwaka 2020 baada ya kuzama kwa nyumba walizokuwa wanaishi wakazi wa mtaa huo, Everina na familia yake waliamua kubaki kupambana na hali zao.
“Hatuna fedha za kwenda kwenye nyumba za kupanga ni gharama, tumeamua kurejea hapa kukabiliana na maisha,” anasema Everina, mama wa watoto watatu.
“Kuna wakati upepo ukivuma unashtukia maji yanaingia ndani,” anasema mwanamke huyo kuwa yuko katika wakati mgumu kwa sababu kila mahali wamezingirwa na maji hivyo hutumia vifusi vya mchanga ili kuingia katika nyumba yake ambayo imeharibiwa vibaya.
Kuongezeka kina cha maji cha ziwa hilo maarufu Afrika hasa katika Mtaa wa Ziwa, kumetokana na mvua kubwa iliyonyesha mwaka juzi ambapo ilisababisha athari mbalimbali ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu zikiwemo nyumba.
Wakati wakisubiri maji yapungue ili warudi katika makazi yao ya awali, ni familia za nyumba mbili kati ya 43 ndiyo zinaendelea kuishi katika eneo hilo, licha ya changamoto ya maji iliyopo.
Familia hizo zimeendelea kukaa katika eneo hilo kutokana na kukosa maeneo mengine ya kuishi, licha ya mamlaka kuwatahadharisha kuwa siyo sehemu salama ya kuishi kwa sasa.
Nyumba zote kwa sasa zimebakia magofu na makazi ya wanyama wakali, jambo linalohatarisha maisha ya Everina na wenzake.
“Usiku ukiingia hofu inakuwa kubwa, tunaogopa kubakwa na kuporwa mali zetu lakini pia tunahofia kuvamiwa na wanyama wakali kama mamba na nyoka kifupi tunaishi kwenye mazingira magumu na tunaishi kwa neema ya mwenyezi Mungu,” anasema Everina.
Mama huyu anasema hana fedha za kwenda kuishi sehemu nyingine na kwamba amefanya hivyo ili kupunguza changamoto ya watoto wake kwenda shule.
Tatizo la homa za mara kwa mara, malaria na fangasi miguuni limekuwa jambo la kawaida na kwamba muda wote wanakaa na dawa za kutuliza maumivu.
“Kifupi tunaishi kama wakimbizi kwenye nchi yetu wenyewe lakini tunavumilia ili maisha yaende,” anasema Everina.
Huenda kina cha maji kikaongezeka zaidi mwaka huu na kufifisha matumaini ya Everina baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri ujio wa za kutosha za masika na hivyo kuleta athari mbalimbali katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwemo Mwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliyekuwa akitoa utabiri wa mwelekeo za mvua msimu wa masika za Machi hadi Mei 2022 jijini Dar es Salaam Februari 17, 2022 alisema mvua hizo za masika zinaweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha na milipuko ya magonjwa.
Soma zaidi:
Kwa mujibu wa Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria, mwaka ulioishia Mei 2020 wastani wa kina cha maji katika ziwa hilo kilikuwa mita 1134.27 lakini kwa mwaka ulioishia Mei 2021 kiwango kimeongezeka kwa 0.60 na kufikia mita 1134.87 ambazo hazijawahi kufikiwa katika kipindi chote cha nyuma.
Bodi hiyo inaeleza kuwa kina hicho kinaweza kuongezeka zaidi na kuathiri watu wanaoishi pembezoni mwa Ziwa hilo ambalo ni kitega uchumi kwa kaya nyingi za mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inakataza kujenga na kufanya shughuli zisizo rafiki wa mazingira katika maeneo ya mabondeni na kwenye kingo za mito na maziwa ndani ya mita 60 ili kuepuka uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mafuriko.
Maumivu hadi kwa wamiliki wa nyumba, wavuvi
Baadhi ya nyumba za Mtaa wa Ziwa zilizoharibiwa zilikuwa ni sehemu ya wamiliki wake kujipatia kipato kutokana na makusanyo ya kodi kutoka kwa wapangaji waliopanga kwenye nyumba zao.
Suzan Butondo ni mmoja wa waathirika katika eneo hilo anasema kila baada ya miezi mitatu au sita alikuwa anapata fedha za kodi ya nyumba.
“Nimerudi nyuma kiuchumi, tegemeo langu ni kufanya vibiashara vidogo vidogo, nguvu nilizowekeza hapa na fedha zote zimepotea…,” anasema Suzan ambaye nyumba yake imezama ndani ya maji.
Wakati wakazi wa Mtaa wa Ziwa wakilalamika nyumba zao kuharibiwa, wavuvi na wachuuzi wanasema kuongezeka kwa kina cha maji kumesababisha baadhi ya mitumbwi yao kujaa maji huku maeneo ya kuanikia dagaa na uduvi yakikosekana.
“Eneo hili tulilitumia kwa ajili ya kuanikia dagaa na uduvi ni miaka miwili sasa maji bado hayajasogea kwa kiwango hicho kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, tumelazimika kutafuta eneo lingine ili kuendelea na shughuli zetu,” anasema Bahanuzi Joseph, mchuuzi wa dagaa mwalo wa Muswahili jijini hapa.
Mwenyekiti wa kikudi cha kutunza mazingira mwalo wa Muswahili, Mwala Buhalwe anasema kabla ya mvua ya mwaka 2020, hali ya maji ilikuwa vizuri na maji yalikuwa katika kina cha kati na walipata wa urahisi mazao ya ziwani lakini sasa hali ni tofauti.

Serikali na uongozi wa mtaa
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ziwa, Abeid Mussa amesema wameandika barua kwenda ofisi ya Mazingira na bodi inayoshughulikia Ziwa Victoria waangalie namna ya kuwasaidia watu ambao nyumba zao ziliingiliwa na maji lakini pia kuweka vigingi vitakavyosaidia wananchi kutojenga kwenye maeneo hayo tena.
Afisa Misitu na Mratibu wa shughuli za Mazingira Mkoa wa Mwanza, Mangabe Mnilago anasema wakazi wa mtaa huo ambao nyumba zao zimeharibiwa na ongezeko la kina cha maji walikuwa wamejenga nyumba zao bila kufuata utaratibu wa mipango miji.
Anasema watu walikuwa wanauziwa maeneo bila kujua kama yapo ndani ya mita 60 na kwamba kama Serikali wameendelea kutoa elimu kwa watu hao kuyahama makazi yao kwa kuwa walikuwa wavamizi.
“Serikali pia tunaendelea kuwaelimisha wananchi kuzingatia sheria za mazingira ili kuhakikisha hawaingii hasara ya kuondolewa au kutozwa faini,” anasema Mnilango.
Nyumba ambayo wakazi wake wamehama baada ya kina cha maji kuongezeka Ziwa Victoria. Kwa sasa nyumba hizo ambazo ziko Mtaa wa Ziwa ni makazi ya wanyama wakali kama mamba na nyoka. Picha| Mariam John.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria, Gerald Itembu, kinachofanyika kwa sasa ni kufanya kipimo pale maji yalipofikia kutoka usawa wa ziwa ili kutoa tahadhari kwa wananchi ili kupunguza athari za kimazingira zinazoweza kutokea.
Mwaka 2019, Jukwaa la Uchumi Duniani lilitoa mapendekezo matatu ambayo yanaweza kusaidia kupunguza athari za kuongezeka kwa kina cha bahari na maziwa ikiwemo kuanzisha miradi ujenzi wa kuta za bahari, vizuizi vya mawimbi, pampu za maji na vyumba vya kuhifadhia maji ili yasitoke kwenye kingo.
Pia kutumia mbinu za kimazingira zinazohusisha ufufuaji wa ardhi na urejeshaji wa miti na ardhioevu ili kusaidia miji kukabiliana na mafuriko ya maji. Mkakati wa tatu ni kuzingatia mipango miji, kujenga nyumba zinazoendana na mabadiliko ya tabianchi na kuondoka katika maeneo yaliyofurikwa.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.
Latest
