Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi

Mariam John 0053Hrs   Julai 17, 2020 Ripoti Maalum
  • Ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamagana jijini Mwanza ambaye bado hajaonekana darasani baada ya shule kufunguliwa.
  • Mwanafunzi mzee aliyeondoa aibu ya utu uzima na kuamua kujiunga na elimu ya msingi ili asome pamoja na watoto wadogo.
  • Atarudi shuleni na kuendelea na masomo yake?

Mwanza.  Ni wiki ya pili sasa tangu shule zilipofunguliwa baada ya likizo ya takriban miezi mitatu iliyosababishwa na janga la corona, lakini Abdallah Mabindo (53) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamagana bado hajaonekana darasani.

Mabindo, ambaye alizua minog’ong’ono na majadiliano kwa jamii inayomzunguka wakati anaanza darasa la kwanza mwaka 2016, alipaswa kuendelea na masomo safari hii akiwa darasa la tano.

Yu wapi Mabindo, mwanafunzi mzee aliyeondoa aibu ya utu uzima na kuamua kujiunga na elimu ya msingi ili asome pamoja na watoto wadogo wenye umri wa kiwango cha wajukuu wake?  Je, ameingia mitini na kuitelekeza shule? 

Wakati anajiunga katika shule hiyo iliyopo katika halmashauri ya Jiji la Mwanza mkoani Mwanza, hata walimu hawakuweza kumuunga mkono ukiachana na majirani na ndugu wa karibu waliokuwa wakimcheka.

Wapo waliodiriki kumhusisha na mpelelezi aliyetumwa kufuatilia nyendo za shule hiyo huku wengine wakimkebehi kuwa anapoteza muda kwa kuwa umri alio nao hatoweza kufika mbali.

Pamoja na mijadala yote hiyo, Mzee Mabindo aliziba masikio na kuwaaminisha Watanzania na jamii yote inayomzunguka kuwa alienda shuleni kwa nia ya kujifunza.

Abdallah Mabindo (53) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamagana  akiwa darasani lakini wiki mbili sasa tangu shule zifunguliwe hajaanza masomo. Picha|Mariam John.


Kwanini alirudi shule akiwa mzee?

Kila kukicha dunia inabadilika na mambo lukuki yamebadilisha mfumo wa maisha ya kawaida ya binadamu. Kwa sasa kila kitu kinahitaji elimu angalau ya kiwango cha elimu ya msingi ya kujua kusoma na kuandika.

“Kadri siku zilivyoenda nilitamani sana kujua kusoma kwa kuwa mambo mengi yanabadilika,”anasema Mabindo.

Zamani elimu haikupewa kipaumbele, anasema, huku akitolea mfano kuwa hakuwahi kujua kuimba wimbo wa Taifa na wala hakujua kama umeandikwa kwenye kitabu.

Changamoto ya kutojua kusoma na kuandika pia ni moja ya sababu iliyomfanya kurudi shule baada ya Rais John Magufuli kutangaza elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne wakati anaingia madarakani mwishoni mwishoni mwa mwaka 2015.

Mbali na jambo hilo, pia aliwahi kudhulumiwa haki yake na aliyekuwa mwajiri wake katika moja ya kiwanda kilichopo jijini Mwanza. 

Mzee huyo anasimulia kuwa aliandikiwa kulipwa fedha Sh3 milioni lakini aliyekuwa ofisa utumishi wa kiwanda hicho alichana karatasi zilizokuwa zimeidhinisha malipo hayo na kusababisha fedha kupotea.

Kutokana na changamoto hiyo mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 49 alilazimika kuingia darasani ili kukabiliana na changamoto hiyo huku akiwa na matumaini ya kufika mbali kielimu na kuisaidia jamii ya watu wanaokabiliwa na changamoto kama ya kwakwe.


Zinazohusiana:


Mabindo, baba wa mtoto mmoja, mkazi wa mtaa wa Igogo jijini Mwanza ameiambia Nukta kuwa alichelewa kupata elimu kutokana na wazazi wake kushindwa kumpeleka shule wakati huo mwanzoni mwa miaka ya 1970.

“Nilipokuwa mdogo sikuweza kupata elimu kutokana na mfumo uliokuwepo wa kuchunga ng’ombe na kilimo lakini pia hakukuwa na hamasa ya kwenda shule kama ilivyo sasa,” anasema huku akionekana kufadhaika kutokana na kilichotokea wakati huo. 

Mabindo, ambaye ni mtoto wa sita kati ya watoto tisa wa mzee Mabindo Vita, anasema yeye pamoja na mdogo wake mmoja hawakuweza kusoma na kwamba kati ya mwaka 1973 na 1974 alipelekwa shule na kaka yake na alienda siku moja na hakuweza kurudi tena.

Anasema wapo baadhi ya ndugu zake waliosoma hadi ngazi ya kidato cha nne na wengine darasa la saba.

Wakati anaingia shuleni hapo, Mabindo anasema alikuwa hajui kusoma wala kuandika.

Anasema jitihada na nia aliyokuwa nayo vimemsaidia kuondoa giza lililokuwa mbele yake.

“Nilipofika shule walimu na wanafunzi walikuwa wananiogopa, baadaye niliwafuata na kuwaeleza kuwa nia yangu ni kutaka kujua kusoma na kuandika,”anasema Mabindo.

Baraka Samson, mmoja wa wanafunzi anayesoma pamoja na Mabindo, anasema wakati anaingia darasan alidhani ni mwalimu anakuja kuwafundisha lakini haikuwa hivyo kama alivyodhania badala yake alimuona akikaa kwenye dawati na kusubiri ratiba ya masomo.

“Nilidhani kuwa ni mwalimu lakini haikuwa hivyo kama nilivyodhania badala yake nilimuona akishiriki masomo pamoja na sisi,”anasema Baraka.

Watoto wengine, kutokana na umri wa Mabindo, walidhani ni mzazi amekuja kufuatilia maendeleo ya mtoto wake. Jambo ambalo walikuwa hawafahamu ni kwamba alikuwa ni mmoja wao ambaye akicheza nao, kusoma nao na kujadiliana nao. 

“Mimi nilidhani kuwa ni mzazi amekuja kumuona mtoto wake baadaye nilishangaa kumuona akiingia darasani kwetu na hata mwalimu alipoingia nilishtuka kumuona anachukua kalamu ya risasi na daftari na kuanza kuandika,” anasema Elizabeth.

 “Sikutegemea kama mtu mzima kama huyo aingie darasani na kuanza kujifunza pamoja nasi,” anaongeza.

 Wanafunzi hao wanasema baadaye aliwaeleza nia yake na kumchukulia kama mwanafunzi mwenzao na hata aliposhindwa kuelewa alinyoosha mkono kumuuliza mwanafunzi.

Abdallah Mabindo akiwa na wanafunzi wenzake shuleni hapo. Mwanafunzi huyo mwenye miaka 53 aliamua kwenda shule ili kujifunza kusoma na kuandika na kuondoa ujinga. Picha| Mariam John. 

“Hata kujibu maswali alikuwa ananyoosha mkono na kujibu na anaposhindwa mwalimu alimuinua mwanafunzi mwingine kujibu swali hilo… aliposhindwa swali kwenye mtihani wa majaribio alikuwa anatuuliza,” anasema Samson Emmanuel.

Mwalimu wa darasa tano katika shule hiyo, Domitila Lupeleleja anasema ujio wa mwanafunzi huyo hawakuutegemea  kwa kuwa wakati wazazi wanaleta watoto wao kuwaandikisha kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza na yeye alikuwepo.

“Tulidhani kuwa amekuja kumwandikisha mtoto wake lakini baada ya kutueleza amekuja kujiunga na shule hii kuanza darasa la kwanza hatukuamini,”anasema Domitila

Kwa mujibu wa Domitila mwalimu aliyekuwa anaandikisha mwanafunzi huyo ambaye Nukta hakijaweza kumpata kuzungumza naye, anasema alipata wakati mgumu kumwandikisha na alienda kupata mwongozo kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule kama inawezekana.

“Halikuwa tegemeo la kila mwalimu hapa shuleni kwanza hawakuwa na imani naye hata mimi pia sikuweza kumwamini tulidhani huenda amekuja kutuchunguza,”anasema.  

Hata hivyo, baada ya kutuaminisha kuwa amekuja kujiandikisha kusoma pamoja na kumpima kwa mambo mengi tuliamini kuwa amekuja kwa nia ya kujfunza na si vinginevyo.

Nini mstakabali wa mwanafunzi huyo? Atarudi shule na kuendelea na masomo? Usikose sehemu ya pili ya makala haya yatakayokujia kesho Julai 18, 2020. 

Related Post