Wananchi zaidi ya 450,000 kunufaika na mtambo mpya wa maji Mwanza
- Mtambo huo umegharimu zaidi ya Sh70 bilioni
- Serikali yasema utaratibu wa kuwasha mitamboni endelevu
Mwanza. Huenda wananchi zaidi ya 450,000 katika mitaa tisa mkoani Mwanza wakaondokana na uhaba wa maji mara baada ya Serikali kuanza majaribio katika mtambo mpya wa maji wa Butimba uliopo jijini humo.
Wananchi hao ni kutoka mitaa ya Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwanima, Fumagila, Sawa, Igoma, Kishiri na Nyamhongolo ambao wamekuwa na uhaba wa maji katika maeneo yao kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Neli Msuya, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (MWAUWASA) aliyekuwa akizungumza na wananchi Septemba 15, 2023, amesema mtambo huo utapunguza shida ya maji inayowakabili wakazi wa maeneo hayo.
“Mtambo huu uliowashwa leo una uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku ukijumlisha na lita milioni 90 zilizokuwepo awali utaona tutakuwa tumepunguza ingawa bado mahitaji ni makubwa hivyo tutaendeleaa kupunguza kidogo kidogo,” amesema Msuya.
Kabla ya chanzo hicho kufanya kazi wakazi hao walitegemea chanzo cha ‘Capri Point’ kilichozalisha lita za maji milioni 90 kwa siku ambazo hazikidhi mahitaji ya wakazi hao wanaotumia lita milioni 160 za maji.
Hata hivyo, kiongozi huyo amewatahadharisha wananchi kuchemsha maji hayo kabla ya kunywa ili kulinda afya zao.
“Niwakumbushe wananchi kuwa maji ambayo yamenza kutoka leo ni ya majaribio hivyo bado hayako salama hivyo niwakumbushe wakazi kwenye mitaa husika ambayo itafikiwa na huduma hiyo kuchemsha maji hayo kabla ya kutumia,” ameongeza Msuya.
Soma zaidi
-
Upungufu wa walimu shule za msingi unavyoathiri elimu Tanzania
-
Afrika inavyoweza kukabiliana na baa la njaa
Ni ahueni kwa wananchi
Baada ya mtambo huo kuwashwa baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wamesema watapata ahueni baada ya shida ya maji kuwatesa kwa zaidi ya mwaka mmoja licha ya mitaa yao kuwa karibu na ziwa Victoria.
“Tunaishi karibu na ziwa (Viktoria) lakini tunapata shida kupata huduma ya maji, maji yanatoka mara moja kwa wiki na wakati mwingine hayatoki kabisa, hata yakitoka ni usiku hivyo tunapata shida kuamka kwenda kukinga,” amesema Tumaini Shomari mkazi wa Buhongwa
Naye Jeska Samsoni, ameimbia Nukta Habari kuwa kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja walilazimika kutumia maji ya mabwawa, kukinga ya mvua na kununua maji ambapo ndoo moja ya lita 20 iliuzwa Sh5,000.
Hata Hivyo, wanachi hao wameiomba Serikali kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ujenzi wa mitambo mingine ili kumaliza kabisa changamoto hiyo ambayo inawatesa kwa muda mrefu.

Wanawake na watoto ndio wahanga wakubwa wa shida ya maji iliyowatesa wakazi wa mkoani Mwanza.Picha|Mariam John
Utaratibu wa kuwasha mitambo ni endelevu
Mtambo huo uliowashwa kwa mara ya kwanza umegharimu zaidi ya Sh70 bilioni huku matengenezo zaidi yakiendelea kwa awamu nne zilizobaki mpaka kukamilika.
Aidha, Kaimu Meneja Msuya aliwaambia wananchi kuwa utaratibu wa kuwasha mitambo mingine na kujenga mantaki ya maji bado unaendelea ili kufikia mitaa ya nyegezi, Luchelele, buhongwa, Buswelu na Butimba.
Katika mitaa ya Buswelu, Kahama, na Nyamadoke Sh4.3 bilioni inatarajiwa kutumika kuongeza mifumo ya usambazaji wa maji na kulaza mabomba huku wakitarajia kuongeza matenki ya maji katika mitaa mbalimbali ikiwemo Nyamazobe, Buhongwa Fumagila Bujora na usagara..
“Mpango huu wa utekelezaji unatarajiwa kuanza Disemba mwaka huu kwa fedha za ndani ambazo tayari zimetengwa na tunatarajia kutangaza zabuni kwa mkandarasi atakayeshinda ili anze kazi hiyo,” amesema Msuya
Pamoja na mpango huo, Mamlaka hiyo inakumbana na changamoto ya kutumia gharama kubwa kutumia jenereta kusukuma maji kutoka na umeme kukatika mara kwa mara.