Wananchi waomba meli ya mwendo kasi Ziwa Victoria

February 5, 2023 7:22 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataka meli hiyo ifanye kazi kati ya Mwanza na Kagera.
  • Wasema wanapoteza muda mwingi majini huku biashara zao zikiathirika.
  • Serikali yasema itajibu kilio chao.

Mwanza. Wakati uboreshaji wa huduma za usafiri ndani ya Ziwa Victoria ukiendelea, baadhi ya wakazi mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuboresha huduma kwa kuwajengea meli inayotumia saa chache ziwani.

Wakizungumza na Nukta habari baadhi ya wakazi jijini Mwanza wamesema Serikali inatakiwa kujenga meli inayotumia saa nne kwenda Bukoba mkoani Kagera na angalau iwe inasafiri mara mbili kwa siku.

Amina Oscar ni mkazi wa Igogo jijini Mwanza, amesema pamoja na juhudi za Serikali za kupunguza tatizo la usafiri ndani ya Ziwa Victoria lakini bado haijaleta meli inayoweza kusafiri kwa saa chache ziwani.

Ameiomba kufikiria wazo hilo ambalo si tu litapunguz adha ya usafiri bali pia litaongeza mapato.

“Zama za kusafiri usiku kucha ndani ya maji zimepitwa na wakati ni wakati wa mabadiliko mbona kuna mabasi yanaondoka Mwanza saa 5 asubuhi  kwenda Bukoba kwa nini isiwe kwenye safari wa meli?,” amehoji Amina.

Mkazi mwingine wa jijini hapa, Joshua Makaka amesema kwa sasa wanalazimika kusubiri usiku kusafiri kwenda Bukoba na kufika huko assubuhi wakati wangefikiria kujenga meli ya mwendo kasi ambapo mtu anasafiri asubuhi saa 5 anakuwa Bukoba na anafanya shughuli zake kisha kurudi Mwanza siku hiyo hiyo.

Akitolea mfano meli ya Mv Butiama na Claris Hapa Kazi Tu amesema zamani kabla ya meli hizo kuanza kazi, wakazi wa kisiwa cha Ukerewe walikuwa wanasafiri mara moja lakini kwa sasa wanaweza kusafiri asubuhi na kurudi jioni.

“Kwa maana hiyo kwa sasa mtu anaweza kwenda kununua samaki Ukerewe na akarudi nao jioni wakiwa fresh kabisa, hivyo hivyo kwa meli za Bukoba zinatakiwa zifanyiwe marekebisho,” amesema Makaka.

Meli ya Mv Victoria inayofanya kazi Ziwa Victoria. Picha |  Mariam John/Nukta.

Akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Edmund Lutta amesema Serikali imetenga Sh113 bilioni kwa ajili utekelezaji wa miradi 12.

Lutta amesema kati ya miradi hiyo minne ni mipya, mitano ni ya kufanyiwa ukarabati na mitatu inaendelea. 

Amesema kati ya miradi hiyo Sh53 bilioni zimetangwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba iliyoko katika ziwa Tanganyika na Sh57 bilioni ni kwa ajili ya utekelezaji miradi mitano iliyopo mkoani Mwanza na Sh2 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa meli ambazo MSCL imepewa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika ziwa Nyasa.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa ujenzi wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu ambao ulipokelewa kutoka kwenye Serikali ya awamu ya tano.

“Hadi sasa meli ya Mv Mwanza ipo kwenye hatua ya pili na kwamba mwanzoni mwa mwezi Februari itashushwa majini kwa ajili ya hatua ya ukamilishaji,” amesema Lutta

Miradi mingine ni ukarabati wa meli ya MV Ukerewe, Mv Liemba pamoja na ujenzi wa chelezo mpya Ziwa Tanganyika itakayokuwa na uwezo wa kubebea tani 4,500.

Lutta amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha usafiri wa majini kwa kujenga na kukarabati meli zilizokuwa hazifanyi kazi ili kuhakikisha usafiri wa majini unakuwepo wakati wote.

“Serikali imejidhatiti kuhakikisha inapunguza changamoto ya usafiri majini, tutaufanya usafiri huu uwepo masaa yote ili mtu aweze kusafiri muda na wakati anaotaka yeye,” amesema Lutta.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW