Fursa zinazoweza kuwatoa kimaisha vijana Kanda ya Ziwa
- Ni pamoja kulitumia vizuri Ziwa Victoria.
- Kuwekeza kwenye kilimo na uuzaji wa bidhaa zinazopendwa na wakazi wa kanda hiyo.
- Baadhi yao walia ukosefu wa mitaji unawarudisha nyuma.
Mwanza. Wakati serikali mkoani Mwanza ikifungua tena dirisha la vijana na wanawake kuanza kuchukua mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, baadhi ya vijana mkoani humo wamesema zitawasaidia kufikia ndoto zao kutokana na mkoa huo kuwa na fursa nyingi za kiuchumi.
Dirisha la maombi ya mikopo katika mkoa huo lilifungwa kwa siku 30 ili kupisha uchunguzi kama taratibu za utoaji zinafuatwa.
Nukta habari (www.nukta.co.tz) imefanya mahojiano na vijana mkoani Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine wameeleza kuwepo kwa fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuwatoa kimaisha.
Hata hivyo, wanasema pamoja na kuwepo kwa fursa hizo changamoto inayowakabili ni kukosa mitaji wa kuendesha shughuli zao.
Amir Samir ni mjasiriamali anayejishughulisha na ushonaji wa viatu vya ngozi katika Manispaa ya Ilemela anasema fursa za biashara mkoani Mwanza zipo nyingi ikiwemo hiyo ya ushonaji wa viatu ambavyo vinapendwa na watu wengi.
“Mahitaji ya viatu vya ngozi nchini ni makubwa na hata bidhaa zingine zinazotokana na ngozi, changamoto iliyopo ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kununulia bidhaa hizo,” anasema Samir.
Uwepo wa Ziwa Victoria pia ni moja ya fursa ambazo vijana wanaweza kuzitumia kujiajiri . Waliogundua siri hutumia mitumbwi kwa ajili ya kuvua samaki, usindikaji na uuzaji wa dagaa pamoja na ufugaji wa samaki.
Chausiku Saidi yeye ni mjasirimali anayejishughulisha na ufugaji wa samaki, aizungumzia fursa hiyo amesema inalipa ingawa changamoto ni ukosefu wa chakula cha samaki nchini.
Matumizi ya taa za umemejua katika shughuli za uvuvi yanasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuwaongezea ufanisi wavuvi wanapovua samaki. Hata hivyo, baadhi ya wavuvi wanazitumia isivyo halali kuvua samaki wasioruhusiwa kisheria. Picha| TAREA.
Chausiku anashirikiana na wanakikundi wenzake saba ambao wameanza ufugaji wa samaki tangu mwaka 2017 na mpaka sasa wana mabwawa matano ya kufugia samaki aina ya sato.
Amesema matokeo ya ufugaji wa samaki ni mazuri kwa kuwa wanapata faida, ingawa kuna changamoto ya ukosefu wa chakula cha samaki ambacho hakitengenezwi nchini.
“Tunalazimika kuagiza chakula cha samaki nje ya nchi ambacho kwa sasa kimepanda bei, mitaji ni midogo hatuwezi kumudu,” anasema Chausiku.
Fursa zingine ni vijana kujihusisha na kilimo cha mazao na kuuza bidhaa za utalii.
Serikali, wadau wanavyowainua vijana
Afisa Habari na Mahusiano ya Umma kutoka Shirika la kutetea haki za vijana na watoto (MYCN), Paul Bahati anasema shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na Serikali ili kuwasaidia vijana waweze kukua kiuchumi.
Shirika hilo kupitia mradi wa vijana na mkwaja wamewasaidia vijana kuanzisha vikundi ambavyo kwa baadaye wanaanzisha biashara au mradi watakaousimamia.
“Kama shirika tunachokifanya ni kuvisaidia vikundi hivyo katika kuvipatia ujuzi lakini pia kuwakutanisha na Sido kwa ajili ya kupata maarifa zaidi ya kuendeleza mawazo yao,” anasema Bahati.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
Amesema kupitia mradi huo zaidi ya vijana 146 wanawafuatilia ambao wameanzisha vikundi na miradi mbalimbali ikiwemo kiwanda cha kufyatua tofali, kilimo, ufugaji wa kuku, kiwanda cha kusaga karanga, kushona viatu na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
“Tunafanya kazi karibu na maofisa maendeleo ya jamii katika kuwasaidia vijana hao lakini pia tunahakikisha miradi inayoanzishwa inasimama na kuwasaidia vijana hao,” anasema Bahati.
Pamoja na kuwasaidia kubuni biashara pia kama shirika wanawasaidia kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alitoa maagizo kwa Afisa Maendeleo Mkoa wa Mwanza kufanya kazi kwa karibu na vijana ili wapate mikopo kwa ajili ya kuendesha shughuli walizojiajiri.
“Mpaka muda huu fedha zote za marejesho na zilizokuwa zimetengwa kuna zaidi ya Sh2.372 bilioni ambazo zipo tayari kugawiwa kwa vikundi vyote vya vijana, wanawake na wenye ulemavu,” alisema Mhandisi Gabriel.
Hata, hivyo aliwataka watu wanaochukua mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili iwanufaishe vijana ambao hawana mitaji.