Mafuta ya Sangara: Tegemeo la wengi kuinuka kiuchumi Kanda ya Ziwa
- Vijana na wanawake wayasaka ili kujiingizia kipato.
- Wanatumia njia za kienyeji kutengeneza mafuta ya samaki.
- Mafuta hayo hutumika kupikia na shughuli nyingine.
Mwanza. Huyu ndiye Sangara, samaki anayepatikana ndani ya Ziwa Victoria. Ni samaki wa aina yake..
Samaki huyu maarufu anayeutambulisha mkoa wa Mwanza, hutumiwa kwa matumizi tofauti. Wapo wanaomkaanga ili kuongeza ladha, wengine humpika kama supu lakini hubanikwa pia.
Mamia ya watu kutoka pande zote nchini, hupenda kuja Mwanza kwa ajili ya kula kitoweo hicho muhimu kwa afya ya binadamu kwa sababu ana kiasi kikubwa cha protini.
Samaki huyu kimaumbile anatajwa kuwa na uwezo wa kukua hadi kufikia urefu wa mita mbili na uzito wa kilo 200.
Licha ya kutumika kama kitoweo, samaki huyu ni chanzo muhimu cha mafuta ambayo hutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia.
Mafuta haya yanapatikanaje?
Jane Gerald (51), mkazi wa Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, alianza kazi ya utengenezaji wa mafuta ya samaki miaka 30 iliyopita.
Mama huyu mwenye watoto wanne anasema mafuta hayo hupatikana ndani ya samaki aina ya Sangara. Hutumiwa na wafanyabiashara wanaokaanga samaki kwa sababu ni salama ikilinganishwa na mafuta mengine.
“Ukimpasua Sangara, ndani utakuta kuna vitu vingi sana mfano utumbo, mabondo, koromeo na mayai, kwenye vitu hivyo ndipo yanapopatikana mafuta ya samaki,” anasema Jane.
Jane Gerald, mkazi wa Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ni miongoni mwa wanawake maarufu kwa utengenezaji na biashara ya mafuta ya Sangara. Picha | Mariam John.
Baada ya kutenganisha mafuta hayo na vitu hivyo kisha kuyawekea barafu ili kuondoa harufu (shombo), huwekwa kwenye sufuria na kupashwa kwenye moto.
“Mafuta yakianza kutoka unayachukua na kuyachunja kwenye chombo kingine na baada ya hapo utayaweka kwenye vifungashio ambavyo tayari umeshaviandaa,” anasema mama huyo.
Kwa mujibu wafanyabiashara wanaotengeneza mafuta hayo jijini hapa, ndoo moja ya lita 20 iliyochambuliwa hutoa mafuta kati ya lita 20 hadi 30.
Mafuta hayo ambayo yanakuwa yamechanganyika na vitu vingine ikiwemo utumbo huyanunua viwandani kwa bei ya Sh5,000.
“Tunachokifanya baada ya kununua utumbo huo ambao umechanganyikana na mafuta, tunaajiri watu ambao hutusaidia kuchambua ambao hulipwa kwa sh2,000 kwa ndoo moja,” anasema Jane.
Wanayoyatengeneza majumbani huyauza kwa Sh10,000 kwa dumu la lita 10.
Baada ya mafuta hayo kutengenezwa yanaweza kukaa kwa muda wa miezi mitatu hadi minne.
Ni sangara pekee anafaa kwa mafuta?
Samaki wengine wana uwezo wa kutengeneza mafuta na yakatumika kwa shughuli mbalimbali.
Hata hivyo, wavuvi na wafanyabiashara wa samaki akiwemo Marwa Chacha katika Ziwa Victoria wanasema Sangara ndiye hutoa mafuta ya uhakika ukilinganisha na mafuta mengine kutokana na sifa yake ya kukaa muda mrefu.
Zinazohusiana:
- Ripoti: Watanzania 9 kati ya 10 wanatumia miguu kama nyenzo ya usafiri
- Mfumuko wa bei za vyakula Tanzania watarajiwa kushuka Machi 2023
- Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD
Faida za mafuta ya Sangara
Mafuta ya samaki wakiwemo Sangara yana kiwango kikubwa cha Omega 3, kirutubishi ambacho huimarisha afya ya akili na ubongo hasa kwa watoto wadogo.
Matinde Wambura ni daktari wa watoto mkoani Mwanza anasema, mafuta hayo yakitumiwa vizuri yanaweza kusaidia katika ukuaji wa mtoto.
“Kwa sababu yana virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika kwenye mwili wa binadamu. Mathalan, protini A na B, kalisiamu na glucose hivyo mtoto mwenye tatizo la kutokula akitumia mafuta hayo yatamsaidia katika suala hilo na la ukuaji kwa ujumla,” anasema Dk Wambura.
Mafuta ya samaki huyo pia hutumika kukaangia samaki
Mmoja wa wachuuzi wa samaki, Salome Edward anasema toka aanze kukaanga samaki hutumia mafuta hayo kwa kuwa ni mabichi na hayajachakachukuliwa kiwandani.
Kwa mujibu wa Salome mafuta hayo huifanya samaki kuiva haraka lakini pia huwa na mwonekano mzuri kuliko yule aliyetumia mafuta ya kawaida.
Si mafuta tu, machicha yake ni kuni
Mabaki ya mafuta hayo kutoka kwa Sangara hujulikana kama ‘machicha’ hutumika kwa kazi mbalimbali kama kuchochea moto na chakula cha ndege maarufu ‘bwana afya’.
Mengine hutumika kwa ajili ya chakula cha wanyama kama nguruwe.
“Machicha haya hatuyatupi huwa tunayatumia kwa ajili ya kuchochelea moto, mengine huwa tunayauza kama chakula cha mifugo,” amesema Jane ambaye Sangara ndiye anamuweka mjini.
Mafuta ya Sangara yakichujwa baada ya kutengenezwa tayari kwa kuuzwa kwa wakaanga samaki. Picha | Mariam John.
Biashara ya mafuta inalipa
Kazi ya kutengeneza mafuta hayo hudharaulika na baadhi ya watu lakini kwa Jane na familia yake imekuwa na msaada mkubwa wa kusongesha maisha yao ikiwemo kusomesha watoto.
“Ni kazi ngumu kwa kuwa inakufanya unukie samaki muda wote, wanawake wengi hawaipendi kazi hii na hata pale wanapotukuta tunachambua huwa wanapita wameziba pua kutokana na harufu iliyopo,” anasema Jane.
Pamoja na ugumu huo, Jane anasema kwa siku huwa anatengeneza lita 20 hadi 400 na kwamba soko kuu la mafuta hayo ni nchi jirani ikiwemo Kenya na mikoa kadhaa ya Tanzania.
“Inategemeana na mzigo tunaopata kuna wakati samaki wanakuwa hawapatikani viwandani, kuna wakati wanapatikana kidogo tunatengeneza hata lita 20 tu za mafuta na kuna siku samaki ni wengi hivyo tunalazimika kutengeneza hadi lita 400,” anasema Jane.
Ana ndoto ya kuwa mfugaji wa samaki
Pamoja na kazi yake hiyo, ndoto ya Jane ni kuja kuwa mfugaji bora wa samaki. Yeye na wanakikundi wenzake sita wameomba mkopo kwa halmashauri wa asilimia 10 ili waongeze mtaji.
“Toka mwezi Novemba mwaka jana viongozi wetu walianza mchakato wa kuomba mkopo wa halmashauri wa asilimia 4 unaotolewa kwa wanawake wajasiriamali, bado hatujapokea majibu ingawa tunatamani tupate fedha kwanza tuboreshe mazingira ya kazi lakini pia tujenge bwawa kwa ajili ya kufuga samaki,” anasema.
Anasema ndoto yake ni kupunguza changamoto za upungufu wa samaki lakini pia kujiongezea kipato.
Kwa sasa wanategemea mikopo kwa watu na makumpuni binafsi ambayo huwa wanarejesha kwa riba kubwa.
Kila kazi ina changamoto
Richard Stephano ni miongoni mwa vijana wanaojishughulisha na kazi ya utengenezaji wa mafuta ya samaki anasema mazingira ya kufanyia kazi hiyo ni magumu kwa kuwa wanalazimika kutengenezea juani.
“Haya mafuta ni dawa yanasaidia watu wengi lakini pia mafuta haya hutumika kwa ajili ya kukaangia samaki lakini teknolojia zinazotumika katika kuyaandaa siyo rafiki,” anasema Stephano.
Anaiomba Serikali kuwatafutia eneo ambalo linafaa kwa ajili ya uandaaji wa mafuta hayo.
Licha ya mafuta ya Sangara kuboresha maisha ya watu Ziwa Victoria, teknolojia inayotumika kuyatengeneza ni duni jambo linalowafanya wasifaidike ipasavyo na bidhaa hiyo. Picha | Mariam John.
Viongozi waunga juhudi
Mwenyekiti wa soko la dagaa Mwaloni, Fikiri Magafu anasema mafuta hayo yanauzwa hadi nje ya nchi lakini mazingira yanayotengenezewa sio rafiki.
Magafu anasema kama viongozi wa soko wanashirikiana vyema kuhakikisha vikundi vya wajasirimali vinanufaika na kazi wanayoifanya ikiwa ni pamoja na kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazozalisha.
“Mafuta yanauzika sana nchini Kenya kwa sasa lakini tunaendelea kutafuta masoko nchi zingine ili yawe yanaenda,” amesema Magafu
Hata hivyo, mwenyekiti huyo anaiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wajasirimali hao ili waweze kupata eneo maalum ambalo litafaa kwa utengenezaji wa mafuta kuliko ilivyo sasa ambapo yanaandaliwa kwenye mazingira magumu.
Amesema eneo wanapotengeneza liko wazi, kipindi cha masika wanapata wakati mgumu na wa jua kali hivyo ni vyema likawepo eneo ambalo litafaa kwa ajili ya uandaaji wa mafuta hayo.
Tangazo
Latest



