Vyakula vya kuepuka msimu huu wa sikukuu

December 18, 2024 7:01 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na vyakula vya wanga, mafuta na sukari kwa wingi.
  • Wataalamu wa afya wanashauri kuepuka vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda .

Dar es Salaam. Chakula ni miongoni mwa mambo yanayokamilisha aina mbalimbali za sherehe au sikukuu ikiwemo za mwisho wa mwaka ambazo hukutanisha watu pamoja.

Wapo watakaoamua kuandaa vyakula vyao nyumbani huku wengine wakitembelea migahawa na hoteli ili kukamilisha siku hizo ambazo huacha kumbukumbu za kudumu katika maisha ya wengi.

Licha ya umuhimu wake, wataalamu wa afya wametoa tahadhari juu ya ulaji wa baadhi ya vyakula kwa wingi unaoweza kusababisha matatizo ya kiafya.

Malimi Kitunda, Afisa Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) amesema miongoni mwa vyakula vinavyotakiwa kutumiwa kwa uangalifu katika msimu huu wa sikukuu ni pamoja na wanga.

“Sana sana wanatakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wanga kwa wingi kwa wazee na vijana,’’ amesema Kitunda

Baadhi ya vyakula vyenye asili ya wanga ambavyo kwa mujibu wa wataalamu wa afya hupaswi kula kwa wingi. Picha/ Canva.

WHO inapendekeza ulaji wa wanga utokane zaidi na nafaka zisizokobolewa, mboga, matunda, na jamii ya kunde kwa watu wazima, gramu 400 kwa siku, watoto na vijana inapendekeza ulaji wa mboga na matunda kulingana na umri.

Miaka miwili hadi mitano angalau gramu 250 kwa siku, miaka sita hadi 9 angalau gramu 350 kwa siku na miaka 10 na zaidi angalau gramu 400 kwa siku.

Baadhi ya vyakula vyenye asili ya mafuta ambavyo hutumika katika milo ya kila siku. Picha/ Canva.

Mafuta

Msimu huu wa sikukuu ni kawaida kwa aina mbalimbali ya vitoweo kutliwa hususani kuku, nyama ambazo hukaangwa kwa kutumia mafuta mengi.

Mbali na vitoweo hivyo, mapishi kama biriani, pilau tambi nayo huliwa sana msimu huu jambo ambalo ni kinyume na ushauri wa wataalamu wa afya ambao wanafafanua kuwa matumizi ya mafuta mengi yanaweza kusababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Kwa mujibu wa chapisho la ulaji unaofaa la  TFNC, mafuta bora ni yale yanayotokana na mimea. Pia inashauriwa kutumia njia mbadala za kupika kama kuchemsha, kuchoma au kuoka badala ya kukaanga kwa mafuta mengi.

“Mafuta ya wanyama kama ngozi ya kuku yanapaswa kuondolewa kabla ya kupika, na inapendekezwa kutumia nyama au samaki wasio na mafuta mengi,” limesema chapisho hilo.

Sukari

Baadhi ya pipi zenye kiwango kikubwa cha sukari ambazo kwa mujibu wa wataalamu wa afya hazipaswi kutumika kupita kiasi. Picha/ Canva.

Sukari,  ambayo hupatikana katika juisi za viwandani pamoja na ulaji uliokikithiri wa matunda ni miongoni mwa masuala ya kuzingatia mzimu huu wa sikukuu.

Licha ya kuwa chanzo cha nishati, inaweza kusababisha kuongezeka kwa uzito na matatizo ya meno kama vile karisi.

Kitunda anashauri kuepuka vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda na badala yake kutumia vinywaji asilia kama juisi za kutengeneza.

“Juisi za kutengenezwa ndio zinapendekezwa haswa, ndio tunazoshauri watu watumie hizo lakini pia juisi za viwandani ambazo zina wingi wa sukari inabidi zipunguzwe,” amesema Kitunda.

Baada ya kuangazia vyakula hivyo na jinsi vinavyoweza kuhatarisha afya baada ya msimu huu kuisha wataalamu wa afya wanashauri matumizi ya mlo kamili wenye aina zote za chakula ikiwemo mboga mboga na matunda ili kuendelea kuimarisha afya.

Enable Notifications OK No thanks