Sintofahamu mabadiliko bei ya samaki Ziwa Victoria

November 15, 2022 12:03 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya samaki viwandani yashuka, wanunuzi wakipungua. 
  • Wachuuzi wauza vipande vya samaki  ili kupata faida kutoka kwa walaji.
  • Serikali yaombwa kuingilia kati suala hilo. 

Mwanza. Alianza siku yake kwa matumaini makubwa baada ya kununua samaki kwa wavuvi awapeleke kiwandani ili ajipatie faida. 

Hata hivyo, siku hiyo haikuisha vizuri. Wanunuzi wake walimtajia bei ya chini kuliko aliyotumia kununulia. Aliishiwa nguvu kwa sababu kilichofuata ni hasara. 

Huyo ni mfanyabiashara wa samaki mkoani Mwanza, Charles Msakatonge. Yeye pamoja na wenzake wamekuwa wakinunua samaki kutoka kwa wavuvi wa Ziwa Victoria na kuwauza kwa wenye viwanda ambao huwachakata kabla ya kuwasafirisha nje ya nchi. 

Changamoto inayowapata kwa sasa ni mabadiliko ya bei ya kitoweo hicho. bei hupanda na kushuka, jambo linalowaweka katika wakati mgumu wa kufaidika na biashara hiyo. 

Samaki ambao wanapatikana kwa wingi katika Ziwa Victoria ni sangara, sato, nembe, ningu, gogo, kambale na kamongo.

Msakatonge anasema bei wanazouziwa na wavuvi kwenye mialo kwa kilo ni tofauti na bei wanayoikuta viwandani na sababu kubwa ni kutokana na kukosekana kwa bei elekezi kwenye soko la dunia.

“Unakuta sisi huku visiwani tunanunua samaki kwa kilo moja Sh6,050 tukiamini kiwandani tutaenda kumuuza kati ya Sh7,000 au 7,800 matokeo yake tunakuta bei zimeshuka zaidi na kufikia Sh6,000 kwa kilo au Sh6,050 ile ile ambayo tulinunua kwa mvuvi wakati huo zimetumika gharama nyingi zikiwemo za usafirishaji,” anasema Msakatonge. 

Kabla ya bei hiyo kushuka miezi mitano nyuma walikuwa wakiuza samaki kwa Sh11,000 kwa kilo moja, bei ambayo imeshuka na kufikia Sh7,000 na wakati mwingine chini ya hapo.

Mfanyabiashara huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka sita anasema kinachotokea katika kipindi hiki kinawavunja moyo, na wanatamani kugeukia biashara zingine au kuuza samaki kwa bei ya rejareja ambapo zinalipa zaidi.

“Na changamoto yetu huku visiwani wakati mwingine barafu za kugandishia samaki zinaisha na kusababisha samaki kuharibika hivyo tunalazimika kuwauza hivyo hivyo kuliko kuwaacha wakaharibika,” anasisitiza Msakatonge.

Wafanyakazi wa samaki katika kiwanda cha samaki cha TFP cha jijini Mwanza  wakichakata samaki kabla hawajasafirishwa nje ya nchi.vPicha | Mariam John.

Baada ya shirika la ndege la Ethiopia kuanza kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi wafanyabiashara waliamini bei ya samaki itaimarika lakini hakuna mabadiliko. 

Mfanyabiashara mwingine, Edwino, Oking’o anasema zamani walilazimika kusafirisha mizigo kwa kupitia Nairobi nchini Kenya lakini sasa samaki  wanasafirishwa moja kwa moja kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza. 

Maboresha ya usafirishaji huo yangeenda sambamba na upatikanaji wa bei ya samaki ya kila siku ambapo mfanyabiashara au mvuvi angekuwa anaona soko la samaki lilivyo kwa siku hiyo hivyo kuamua kuvua au kutoingia ziwani.

“Tatizo bei inakatisha tamaa, tunatamani angalau tungekuwa tunajua bei ya soko la samaki ya kila siku ili mfanyabiashara anaamua kununua mzigo au kutonunua kabsa lakini pia hiyo itawasaidia wavuvi kama siku hiyo waingie ziwani kuvua au wasubiri kuona bei ya soko kama inashawishi kuingia kwa siku hiyo,” anasema Oking’o.


Zinazohusiana:


Ni kilio tu

Wakati wafanyabaishara wa samaki viwandani wakiangua kilio, upande wa pili kwa wachuuzi wao wanalalamikia ugumu wa maisha unaochangia samaki kupanda bei na kusababisha walaji kushindwa kununua.

Sikitu Tezela ni mchuuzi wa samaki katika soko la Mwaloni jijini Mwanza anasema hivi sasa biashara ya samaki ni ngumu tofauti na zamani kwa kuwa anashindwa kumaliza mzigo wa samaki alionao.

“Hali ni ngumu, nikinunua mzigo wa samaki wa Sh200,000 nauza na wanabaki na kuwahifadhi kwenye friza tofauti na zamani ambapo mzigo wa kiasi hicho cha fedha uliuzika wote,” anasema Tezela.

Anasema biashara ya kuuza samaki ameifanya tangu mwaka 2019 lakini bado ni ngumu na kwamba anachokifanya hivi sasa ni kumgawa samaki huyo kwa vipande vipande na kuuza kwa bei ya chini tofauti na zamani ambapo waliuza mzima.

“Kutokana na ugumu wa maisha sasa tumebuni mbinu ili kumfikia kila mmoja kulingana na pesa aliyonayo, ambapo hivi sasa samaki tunamgawanya kwa vipande vitatu hadi vinne na kipande kimoja kinauzwa Sh 2,000, hivyo mtu yeyote mwenye uwezo na asiyenao anaweza kununua kuliko kununua kwa bei ya Sh8,000,” anasema Tezela.

Ahamad Nchora ni mfanyabaishara wa samaki katika soko kuu jijini Mwanza anasema bei ya samaki ipo juu, jambo linalowaumiza wafanyabiashara.

“Hivi sasa samaki anauzwa kuanzia Sh4,000 kupanda juu ambapo mkubwa kabisa anauzwa Sh12,000 hadi 20,000 inategemea na ukubwa wa samaki, changamoto iliyopo hawauziki kutokana na ugumu wa maisha,” anasema Nchora.

Mambo yalichangia mabadiliko ya bei

Mwenyekiti wa Chama Cha Wavuvi Tanzania, Bakari Kadabi anasema kuporomoka kwa bei ya samaki kutasababisha wafanyabiashara wengi kufirisika na kuchangia uvuvi haramu kwani itawalazimu wavuvi kuvua samaki walio chini ya viwango ili wapate kipato kikubwa.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa bei halisi inayouzwa katika soko la dunia tofauti na bidhaa nyingine kama madini ambayo wao yana bei elekezi ya soko ambayo humsaidia mtu kufanya maamuzi. 

Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali kuingilia kati mabadiliko ya bei hizo za uuzaji wa samaki pamoja na mazao yake ikiwemo mabondo yanayotokana na sangara kwa kuwa hakuna utaratibu maalum wa uuzaji hivi sasa.

Mmoja wa wafanyakazi katika kiwanda cha samaki jijini Mwanza, ambaye hakupenda jina lake litajwe ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa bei ya samaki imeshuka kutokana na soko la samaki nje kuporomoka na kujikuta wanapata hasara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW