Taa za umemejua zinavyochangia uvuvi haramu Ziwa Victoria

May 26, 2022 6:40 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wavuvi kutumia taa zenye mwanga mkali kuvuta samaki wachanga.
  • Matumizi ya nyavu zilizopigwa marufuku nayo yatajwa.
  • Serikali yasema itawashughulikia wanaokiuka matumizi ya taa hizo katika uvuvi.

Mwanza.  Hana tena sababu ya kuingia gharama kubwa za kununua mafuta ili mwanga wa kalabai iendelee kuwaka wakati akipambana usiku kucha kuvua samaki katika Ziwa Victoria.

Ujio wa umemejua umemsaidia mvuvi wa samaki na dagaa, Alex Elia wa mkoani Mwanza kupata mwanga wa uhakika akiwa ziwani kuvua samaki bila hofu ya kukosa nishati hiyo muhimu.

Hata hivyo, Elia anasema huenda uvuvi huo usiwe endelevu kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya taa hizo za umemejua ambazo huchangia katika uharibifu wa mazalia ya samaki. 

“Uvuvi haramu umekithiri na hii inachangiwa na mabadiliko ya taa za uvuvi wakati tunavua kwa kutumia kalabai mazalia ya samaki na dagaa wachanga yalikuwa madogo ukilinganisha na hali ilivyo kwa sasa ambapo samaki wachanga ni wengi,” anasema Elia.

Mvuvi huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka mitano, anasema baadhi ya wavuvi huingia ziwani na taa hizo na betri zake, jambo linalochangia kuzalisha mwanga mkali ambao huwavuta kwa wingi samaki wakubwa kwa wadogo katika mitego ya wavuvi. 

Katika makubaliano ya wavuvi katika mkoa kuhusu matumizi ya taa hizo rafiki kwa mazingira, yalikuwa kuchaji taa kisha kuingia nazo ziwani na si kama inavyofanyika hivi sasa kwa baadhi ya wavuvi kuingia na betri zake. 

Matumizi ya taa za umemejua katika shughuli za uvuvi yanasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuwaongezea ufanisi wavuvi wanapovua samaki. Hata hivyo, baadhi ya wavuvi wanazitumia isivyo halali kuvua samaki wasioruhusiwa kisheria. Picha| TAREA.

Mwanga mkali ni hatari kwa samaki

“Zamani toka tuanze uvuvi wa kalabai hayakuwepo madhara makubwa ya kuvua na samaki wadogo  ambao ni kinyume cha sheria, hali ni tofauti sasa kwenye matumizi ya taa za umeme jua hata wavuvi wadagaa wanakuja na samaki wachanga kitendo ambacho ni kinyume cha sheria,” anasema Medard Kaijage , Mwenyekiti wa  Chama cha Wavuvi  Mkoa wa Kagera. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 inakataza wavuvi kuvua samaki ambao hawajatimiza muda wa kuvunwa ili kuhakikisha uendelevu wa rasilimali hiyo. 

Taa za umemejua wavuvi wengi walianza kuzitumia zaidi miaka mitatu iliyopita baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya kalabai zinazotumia mafuta ya taa ambazo zilikuwa zinasababisha ajali ikiwemo milipuko na uchafuzi wa maji.

“Imebadilika kwa sababu imepunguza gharama za mafuta lakini imeondoa harufu ya mafuta ya petroli yanayoweza kumwagikia  kwenye  mtumbwi  hali ambayo ilikuwa inahitaji umakini kwa mvuvi, lakini pamoja na kuondoa changamoto hiyo hivi sasa matumizi ya sola (umemejua) yanachangia wavuvi kuvua samaki wachanga”, anasema Kaijage.

Baadhi ya wavuvi wanaotumia taa zenye mwanga mkali sana huvua kati ya tani 100 hadi 200 za samaki wachanga kisha wanazichambua na kuziuza kwa wajasiriamali wadogo ambao huwakaanga na kuwauza samaki hao kwa mafungu.

“Kama Serikali haitaliangalia suala hili kwa makini itakuja kushtukia ziwa limebaki tupu, nguvu kubwa ya uvuvi imeongezeka mtu mmoja anamiliki mitumbwi 100 yote inatumia sola na yote ikiingia ziwani asubuhi inarudi na dagaa na hao samaki wachanga,” anasema Kaijage.

Ujio wa taa za umemejua umehitimisha safari ya matimizi ya kalabai kwenye shughuli za uvuvi nchini. Taa zinazotumia mafuta ya taa zimekuwa zikitajwa kuchafua mazingira ya majini na kuchangia ajali kwa wavuvi. Picha| TAREA.

Mwanga wa taa unaokubalika

Utaratibu uliopo ni kuwa mtego mmoja wa samaki unatakiwa kuwa taa za umemejua zenye wati 5 na wati 9 na taa hizo hazitakiwi kuwa kwenye betri badala yake zinachajishwa kabla wavuvi hawajaingia ziwani.

Matumizi ya betri na taa kwa pamoja hayaruhusiwi ziwani  ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wavuvi wakiendelea na kazi zao.

“Kinachofanyika hivi sasa ni kinyume kabisa, wavuvi  wanaingia na taa zaidi ya 10 kwenye  mtumbwi mmoja, ” amesema mvuvi Emmanuel Zagamba na kubainisha kuwa mtego mmoja hautakiwi kuzidi taa za umemejua 10.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi Tanzania (Tafiri) Ismael Kimilei anasema iwapo mvuvi atatumia taa yenye wati 5 hadi wati 10 kwenye uvuvi wa dagaa, nyavu zake zitaweza kuvua asilimia 4 hadi 5 pekee ya samaki ya Sangara. 

Tofauti na ilivyo sasa ambapo matokeo imekuwa ni asilimia 25.6 hadi 27.5 ya Sangara wanaopatikana kwenye vyavu za dagaa.

Dk Kimilei anasema historia inaonyesha kuwa tangu mwaka 2005 hadi sasa kiwango cha uvuvi wa dagaa ambao huvuliwa na sangara yameongeka kutoka asilimia 1.9 na kufikia asilimia sita.

“Katika utafiti wetu tulishauri kuwa taa zinapowekwa ziwani zinawashwa kwa muda wa dakika tano kisha zinazimwa ili kuwapa mwanya dagaa kunaswa kwenye nyavu zao tofauti na ilivyo sasa ambapo taa hizo zinawashwa muda wote,” anasema Dk Kimilei.


Zinazohusiana:


Nyavu za sangara hazitakiwi kutembea mvuvi anapotega na anatakiwa kuzifunga kwenye boya lakini hivi sasa nyavu hizo zinaachwa zikizagaa ziwani hali inayosababisha kuvua samaki wote wakiwemo wachanga.

“Tafiti zilizofanywa mwaka 2020 zinabainisha kuwa tani za dagaa ndani ya Ziwa Victoria zimepungua kutoka tani 600,000 hadi kufikia tani 500,000 upungufu huo ni sawa na asilimia 45 hadi 50 ya dagaa wachanga,” anasisitiza Dk Kimilei.

Mtafiti huyo pia ameshauri kuendelea kuyaacha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mazalia ya samaki hadi muda uliotengwa na vizimba vya kufugia samaki viongezwe kwa kuwa yapo maeneo zaidi ya 30 ambayo yanafaa kwa ajili ya kufugia samaki katika ziwa hilo.

Pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya taa za umemejua, wavuvi wengine wanaunganisha nyavu hadi 12 kwenye mtego mmoja, jambo linalosababisha kuzama hadi ndani kabisa ya ziwa na kukokota samaki wengi hadi wale wachanga.

Uvuvi haramu ni zaidi ya taa za umemejua

“Mfano mtu mmoja anamiliki mitumbwi 100 ya uvuvi na kila siku mitumbwi hiyo inaingia ziwani, kitendo hicho husababisha uvuvi haramu kuwa endelevu kwa kuwa kila mmoja anahangaika kuhakikisha angalau anapata chochote kitakachosaidia kujikimu,” anasema Emmanuel Emmanuel, mdau wa uvuvi mkoani Mwanza.

Nguvu kubwa ya uvuvi inayotumika kuvua inachangia uvuvi haramu kuliko uwezo wa ziwa, anasema Zagamba kuwa hakuna mkakati wa pamoja uliowekwa kuhakikisha suala hili linadhibitiwa na kutaja changamoto kubwa ni kutodhibiti wafanyabaishara wakubwa wa zana za uvuvi ambao wanaingiza zana hizo kwenye mipaka bubu.

Mkakati wa serikali kukabiliana na uvuvi

Ili kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa hilo, Jefta Mchengerwa, Katibu wa Chama Cha Wavuvi Tanzania anapendekeza adhabu na faini kwa wavuvi haramu iongezwe ili kukomesha vitendo hivyo hasa vya kutumia taa za umemejua isivyo sahihi.

“Mvuvi unampiga faini ya Sh10 milioni kwa kukamatwa na masala ya samaki wachanga, mvuvi huyo analazimika kwenda kukopa kiasi hicho cha fedha ili kukomboa zana zake za uvuvi ikiwemo mitumbwi, anaporudi ziwani analazimika kufanya uharifu tena mwingine kama huo wa mwanzo,” anasema Mchengerwa.

Ameiomba Serikali kufanya msako mkali kwenye mialo kubaini taa zisizoruhusiwa na kuwachukulia hatua wavuvi wanaotumia taa hizo.

Serikali imesema itaanza kutumia nguvu ya dola katika kupambana na uvuvi haramu ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya taa za umemejua  zinazotumika kinyume na sheria.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki anasema mvuvi anatakiwa kuwa mtu wa kwanza katika kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya zana za uvuvi zinazochangia kwa namna moja ama nyingine uvuvi haramu.

“Kama Serikali tutahakikisha tunatumia mbinu nyingi ili kuhakikisha tunahibiti uvuvi haramu, hatutaruhusu watu wachache wenye tamaa na walafi kuharibu uvuvi,” anasema Ndaki huku akiwaonya wafanyabiashara wa zana za uvuvi ambao wanaingiza nchini zana zisizoruhusiwa kuwa watawakamata na kuteketeza viwanda na maghala yao.

Baada ya kufanikiwa kuzuia uvuvi haramu, Serikali itaanza kushughulikia masuala mengine kama kodi, tozo na matumizi ya taa za umemejua.

“Kwa sasa tunadhibiti kwanza hili suala kwa sababu tusipofanya hivi hili Ziwa tulilobarikiwa na mwenyezi Mungu litageuka na kuwa jangwa,” anasema Ndaki.


Tangazo:


Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV