Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD

December 29, 2022 5:56 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Hali ngumu mwaka huu imechangiwa na athari za kiuchumi zilizotokana na janga la Uviko-19.

Dar es Salaam. Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imesema mwaka 2022 umekuwa mgumu huku baadhi ya familia zimekuwa zikihaha kuweka mlo mezani na kujikimu hadi lakini kuna suluhu za kimkakati na kimataifa kushughulikia changamoto hizo. 

Katibu Mkuu wa UNCTAD, Rebeca Grynspan akihojiwa katika kipindi maalum cha UNCTAD Tradecast kuhusu kumalizika mwaka huu wa 2022 amesema hali ngumu mwaka huu imechangiwa na athari za kiuchumi zilizotokana na janga la Uviko-19 na kujikwamua kwa polepole kutoka kwenye janga hilo.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mafuriko, lakini pia vita ya Ukraine imesababisha gharama kubwa ya maisha kupanda kote duniani, kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kuendelea kupanda kwa kiwango cha riba na nchi nyingi zinazoendelea kukabiliwa na mzigo usiobebeka wa madeni,” amesema Grynspan.  

Ingawa nchi zilizoathirika zaidi ni zinazoendelea lakini nchi zilizoendelea pia zimepata changamoto hizo lakini amesema tofauti ni kuwa zina nyenzo za kukabiliana na changamoto hizo zaidi ya mataifa duni. 

“Kuanzia katika kiwango cha kitaifa kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa kisera, hatua za kulinda watu lakini mwisho wa siku suluhu zinategemea hatua zilizoratibiwa za jumuiya ya kimataifa  na ndicho tunachojaribu kukisukuma mbele,” amesema katibu mkuu huyo wa UNCTAD kuhusu suluhu ya hali ngumu ya kimaisha. 

Pamoja na hatua hizo amesema pengo la usawa linazidisha changamoto hivyo kuliziba kutaongeza mnepo kwa dunia kupambana na changamoto hizo. 

Kuhusu matarajio yake kwa mwaka ujao amesema “natumai kwa dunia kutambua wajibu tulionao sasa, tunahitaji uratibu, mshikamano, hatua za pamoja na dunia iliyoungana ambayo inahitaji ujarisi na uongozi imara, natumai kuliona hilo 2023.”

Enable Notifications OK No thanks