Simulizi ya vijana waliojiajiri katika biashara ya mabondo Ziwa Victoria
Wafanyabiashara katika soko kuu la Mwanza wakiendelea na shughuli kuwasafisha samaki na kutoa mabondo ambayo huuzwa kwa bei nzuriPicha na Mariam John.
- Watumia biashara hiyo kujikwamua kimaisha.
- Mabondo hayo hutumika katika shughuli za utabibu.
- Serikali yaombwa kuirasimisha biashara ya mabondo.
Mwanza. “Unaupiga mwingi’ ni msemo maarufu kwa sasa nchini Tanzania wenye tafsiri mbalimbali lakini maarufu ni ile ya mtu mchakarikaji na mwenye mafanikio kwenye jamii.
Basi, msemo huo unatimia kwa vijana walioamua kujikita katika biashara ya mabondo katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria likiwemo soko kuu la jijini Mwanza.
Mabondo ni sehemu ya kibofu cha samaki aina ya Sangara yanayomwezesha samaki kuelea akiwa kwenye maji.
Licha ya mabondo kuwa ni muhimu kwa uhai wa samaki lakini sasa ni kama lulu kwa wavuvi na wafanyabiashara kwa sababu ni dili la kuwaingizia kipato cha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Sehemu hiyo ya samaki inatajwa kutumika katika shughuli za utabibu hasa kutengenezea nyuzi kwa ajili ya upasuaji na bidhaa za plastiki.
Katika kipindi cha nyuma ilikuwa ni kawaida kwa mabondo kutupa baada ya kumsafisha samaki lakini uhitaji wa bidhaa hiyo hasa kutoka nje ya nchi ikiwemo China, imekuwa ni fursa muhimu kwa vijana kujipatia kipato.
Inakadiriwa kuwa mabondo yenye uzito wa kilogramu 1 huuzwa kwa Dola za Marekani 150 sawa na Sh350,000.
Kukua kwa biashara hiyo kumepunguza idadi ya vijana wasio na ajira ambao walikuwa wanashinda mitaani jijini hapa wakisubiri kuajiriwa.
Katika soko kuu la jijini Mwanza lililopo Mtaa wa Rufiji jijini hapa utakutana na ofisi karibu 10 zinazojihusisha na biashara ya mabondo. Pilika pilika za hapa na pale zikiwa zinaendelea.
Katika ofisi hizo utakutana na vijana wa kike na wa kiume huku macho yao wakiyaelekeza barabarani ambako kunauzwa samaki aina ya Sangara.
Mwandishi wa Nukta Habari (www.nukta.co.tz) alifanikiwa kuingia katika moja ya ofisi hizo na kukutana na kijana Isoki Joel (25) mkazi wa mtaa wa Kirumba Wilaya ya Ilemela. Yeye na wenzake wanaendesha maisha yao kwa biashara ya mabondo.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
Akiwa na miaka 14, tayari Joel alikuwa mtaani akiambatana na mama yake kupeleka samaki sokoni. Alivutiwa na biashara hiyo hali iliyomsababisha kukatisha masomo yake akiwa kidato cha pili na kugeukia shughuli ya kusaka mabondo kwa wavuvi.
“Nilikatisha masomo baada ya kumuona mama akipata fedha nyingi zaidi, nilikuwa mdogo lakini tayari nilikuwa nimeanza kuona mwanga wa maisha katika biashara,” anasema Joel.
Kabla ya kujiingiza katika biashara ya mabondo, Joel alikuwa anamsaidia mama yake kufuata samaki mwaloni na jioni kupeleka sokoni na kilichokuwa kinamsangaza alikuwa akimuona mama yake akitoa bondo kwenye Sangara pale tu mteja anapomnunua.
“Nilianza kuongeza uelewa na kuhoji kwanini samaki anapouzwa bondo linatolewa, katika udadisi nikabaini bondo lina bei kuliko samaki, mfanyabaishara yupo tayari kukupa samaki bure lakini bondo alitoe,” amesema Joel.
Joel anasema wakati huo hakukuwa na mizani ya kupimia kama ilivyo sasa bali walikuwa wanakadiria kwa kipimo cha mkono na ukubwa wa bondo.
“Mfano mfanyabiashara anakadiria hili bondo kubwa ni Sh50,000 au Sh70,000 na madogo yake Sh20,000 au 40,000,” anasema kijana huyo mrefu wa kimo, “ndivyo hali ilivyokuwa.”
Kukua kwa teknolojia kumesaidia wafanyabiashara wengi wa samaki kunufaika na biashara zao kwakuwa sasa mfanyabiashara hawezi kuuza bondo bila kulipima kwenye mizani.
Alianzaje biashara ya mabondo?
Joel alianza kwa kuingia mkataba na mmiliki wa kiwanda kinachonunua mabondo aliyempatia mtaji wa kuanzia biashara hiyo.
“Mtaji wa mabondo unahitaji fedha nyingi kwa chini kabisa ni Sh1 milioni au chini ya hapo, kwa kuwa bondo linapimwa kwa gramu na katika mzani tunapiga mahesabu kwa desimali yaani tunaandika 0.gram zilizopatikana tunapata kiasi cha hilo bondo,’ amesema Joel.
Kwa mujibu wa Joel, biashara hiyo inafanyika kwa makubaliano kati ya mnunuzi na mfanyabaishara wa samaki ambapo mfanyabiashara ananunua samaki kwa wavuvi na kuwatoa mabondo na kumpatia mnunuzi kwa kugawana kiasi cha pesa kinachopatikana baada ya mauzo ya bidhaa hiyo.
Anasema kwa sasa biashara hiyo imeshika kasi na imesaidia vijana wengi kupunguza makundi mitaani kwakuwa wanajipatia fedha ya kula na matumizi mengine.
Usikose sehemu ya pili ya makala haya ambayo itaangazia kwa kina namba biashara hiyo inavyohatarisha bei ya samaki na Serikali inavyosimamia ili iwe yenye manufaa.