Fedha za IMF zilivyokamilisha madarasa 92 Mwanza
Mwonekano wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwenye shule 25 vya sekondari katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Vyumba hivyo vimejengwa kwa fedha za Uviko-19. Picha|Mariam John.
Ni Sh1.8 bilioni za IMF kukabiliana na Uviko-19.
- Zimesaidia kuondoa upungufu wa madarasa Manispaa ya Ilemela.
Mwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imekabidhi vyumba vya madarasa 92 kati ya 97 vilivyotokana na fedha mgao wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kukabiliana na athari za janga la Corona (Uviko-19).
Mwaka huu, Tanzania ilipokea Sh1.3 trilioni kutoka IMF kwa ajili ya kuboresha na kujenga miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo afya na elimu ili kupunguza makali ya Uviko-19.
Katika ujenzi huo, halmashauri hiyo imeongeza ujenzi wa ofisi ndogo za walimu 28 na kati ya ofisi hizo nne zina vyoo vya ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, Modest Apolinary akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vyumba hivyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Bujingwa Desemba 16, 2021, amesema halmashauri hiyo ilipokea Sh1.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 97.
“Hadi Desemba 15, 2021 jumla ya shule 25 tayari wamekamilisha ujenzi wa vyumba 92 vya madarasa vyenye madawati 4,850 na ofisi 28. Aidha shule moja iko kwenye hatua ukamilishaji wa vyumba vitano vya madarasa na itakabidhi Desemba 28, 2021,” amesema Apolinary
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, mahitaji kwa mwaka wa masomo 2022 ilikuwa ni vyumba vya madarasa 211 kwa ajili ya wanafunzi 10,662, vyumba viliyokuwepo ni 114 na upungufu ni madarasa 97.
“Hivyo kwa mradi huu vyumba 97 vimekamilika kukidhi mahitaji ya wanafunzi wote waliofaulu na watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2022,” amesema Apolinary.
Licha ya kufanikisha zoezi la ujenzi wa madarasa hayo, kupanda kwa vifaa vya ujenzi ilikuwa changamoto katika utekelezaji wa zoezi hilo huku halmashauri hiyo ikibakiza Sh24 milioni.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza halmashauri hiyo kwa kwenda na muda wa ujenzi wa vyumba hivyo na kuvikabidhi na kuagiza halmashauri zingine zijifunze wilayani humo.
Amesema majengo hayo yana ubora kwa kuwa yamejengwa kwa kufuata hesabu za ujenzi, wametumia mbao ngumu za mkongo na kwenye vyumba hivyo wameunganisha mfumo wa umeme.
“Kwa ubora huu wa vyumba hivi vya madarasa hakuna haja ya kwenda kukodi ukumbi kwa ajili ya kufanyia mikutano, kila kitu kinaweza kumalizikia huku huku,” amesema Mhandisi Gabriel.
Zinazohusiana:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
- Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba
- Hisabati, Kiingereza bado pasua kichwa mitihani darasa la Saba Tanzania
Kuhusu chenji iliyobaki ya Sh24 milioni kwenye ujenzi wa vyumba hivyo, Mhandisi Gabriel amesema wakati wanapiga mahesabu alijua chenji itabaki kati ya Sh3 bilioni kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza.
Amesema wilaya ya Ilemela imetoa tafsiri kwamba darasa moja linaweza kujengwa chini ya Sh20 milioni.
Amepongeza mafanikio hayo na kuitaka halmashauri kuyalinda na kuyadumisha ili kuendelea kufanya kazi zingine za maendeleo kwenye halmashauri hiyo.
Pia ameagiza kuhakikisha viongozi wanasimamia mipango yote ya maendeleo kwa kushirikiana na wataalam wa halmashauri hiyo na kuendeleza moyo wa kujitoa kwa viongozi na wananchi wote walioshiriki katika ujenzi miradi mingine.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lumala ya jijini hapa, Angel Mussa amesema zamani wakati wanaenda kuanza masomo ya kidato cha kwanza walipangiwa kwenda na vifaa vingi ikiwemo kiti na meza lakini kwa sasa Serikali imewarahisishia na kuwapunguzia michango ambayo wangetakiwa kwenda nayo wanapoenda kuripoti.
Latest
