Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari

Daniel Samson 0419Hrs   Mei 04, 2018 Habari

   Wanafunzi wakisubiri kufanya mtihani wa kidato cha nne katika shule mojawapo hapa nchini. Picha na Mtandao.

  • Robo tatu au asilimia 76 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017 walipata daraja la IV na sifuri.
  • Wadau wasema uwekezaji katika miundombinu muhimu ya elimu na walimu vitaongeza uelewa kwa wanafunzi na kuinua ufaulu.
  • Serikali yaeleza mikakati inayofanywa kumaliza ufaulu duni katika Manispaa ya Temeke.

Dar es Salaam. Wilaya ya Temeke iliyopo mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka mitatu mfufulizo imendelea kufanya vibaya  katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, licha ya kuwepo kwa juhudi mbalimbali za  uboreshaji wa miundombinu  ya shule na madarasa.

Uchambuzi wa takwimu za matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania iliofanywa na Nukta umebaini kuwa  kati ya mwaka 2015 hadi 2017 ufaulu wa wanafunzi katika Wilaya ya Temeke umekuwa ukishuka kila mwaka ukilinganisha na wilaya zingine za Tanzania.

Hali hiyo inatokea wakati serikali inaendelea na kampeni ya kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, ambapo imeongeza idadi ya wanafunzi katika shule lakini ufaulu wa wanafunzi umekuwa sio wa kuridhisha.

Kwa mujibu wa takwimu za Mpangilio wa Halmashauri kwa ubora wa ufaulu katika kidato cha nne (CSEE) 2017 zilizotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) zinaonyesha kuwa wilaya ya Temeke ilikuwa na shule za sekondari 60 na ilishika nafasi ya 141 kati ya wilaya 195 zilizopo nchini ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo ilishika nafasi ya 137.

Kimsingi ilishuka kwa nafasi 4 toka juu ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2015 ambapo alishika nafasi ya 105 kabla ya kufanya vibaya  mwaka uliofuata wa 2016 ambapo ilishuka kwa nafasi  32.

Mwaka 2017 hali ilikuwa ya kuridhisha kidogo ukilinganisha na mwaka 2016 lakini bado wilaya hiyo haiko katika nafasi nzuri ya ufaulu katika mchuano wa kiwalaya nchini.

Mwaka 2017 wilaya hiyo iligawanywa na kuzaa wilaya nyingine ya Kigamboni ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu kwa wananchi. Lakini hata baada ya kugawanya wilaya zote mbili ziliendelea kufanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne.

Mathalani, katika matokeo ya mwaka 2017, miongoni mwa Wilaya tano za Dar es Salaam, Temeke ilishika nafasi ya nne juu ya Kigamboni ambayo kitaifa ilikuwa nafasi ya 166.

Kinondoni na Ubungo zilifanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza na pili katika mkoa wa Dar es Salaam, huku kitaifa zikiwa nafasi ya 37 na 66 ikifuatiwa na Ilala. Hata hivyo ufaulu wa jumla  wa Dar es Salaam hauridhishi ukilinganisha na mikoa mingine na kiasi kikubwa unasababishwa na Temeke ambayo kwa miaka mitatu haijaingia kwenye wilaya 100 zinazofanya vizuri.

Kushuka kwa ufaulu wa Temeke kunathibitishwa zaidi na mpangilio wa madaraja ya ufaulu wa matokeo ya  2017 ambapo wanafunzi 2,681 zaidi ya robo (asilimia 28) kati ya wanafunzi 9,474 waliofanya mtihani wa kidato cha nne walipata daraja sifuri. Hii ikiwa na maana kuwa takriban kila wanafunzi 10 waliofanya mtihani huo, watatu walipata sifuri.

Katika matokeo hayo, wahitimu waliopata daraja la IV walikuwa 4,563  ambapo ni mara mbili ya waliopata daraja la I hadi III. Hiyo ina maanisha kuwa wanafunzi waliopata daraja la IV na sifuri ni robo tatu au asilimia 76 ya wanafunzi wote. Ni wachache  katika kundi hilo la daraja IV hufanikiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano.


Fahamu: Usiumize kichwa kujua shule bora katika mkoa wako. Soma zaidi ndani ya Elimu Yangu kujua mengi zaidi


Kwa matokeo hayo, wadau wanaeleza kuwa Temeke bado ina kazi kubwa ya kufanya kuongeza ufaulu wa wanafunzi ikizngatiwa mazingira yake ni bora zaidi kuliko wilaya zilizo pembezoni mwa nchi kama Kibondo ambayo ilishika nafasi ya nane na Igunga iliyokuwa ya 10 kitaifa.


Kwanini ufaulu unashuka Temeke?

Kumekuwa na sababu mbalimbali zinazosababisha shule nyingi za Serikali kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne; mojawapo ikiwa ni ongezeko la wanafunzi lisiloendana na uboreshaji wa miundombinu na idadi ya walimu.

Sababu nyingine ni umbali wa zilizoko shule na makazi ya wanafunzi na walimu. Baadhi ya shule ziko nje ya mji na wanafunzi hutumia muda mwingi kwenye magari na hata wakifika shuleni wanakuwa wamechoka.

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu (DUCE)  ya Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Luka Mkonongwa ameiambia Nukta kuwa changamoto nyingine inayokwamisha ufaulu wa wanafunzi ni bajeti ndogo inayotengwa na Serikali kila mwaka ambapo hawafikii wanafunzi wote shuleni.

“Bajeti zinazopelekwa kwenye shule nadhani zinatolewa bila kuangalia aina ya shule na uhalisia wake. Shule zina hali tofauti na idadi tofauti ya wanafunzi lakini zinapewa kiasi sawa. Kwa hili hatujajipanga vizuri,” amebainisha Dk. Mkonongwa.


Muarobaini wa tatizo

Ili kukabiliana na hali hiyo ya kushuka kwa ufaulu katika shule za sekondari,  serikali imeshauriwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa sahihi ya kuwawezesha kujibu mitihani na kukabiliana na maisha.

Mtaalam wa Uchambuzi wa Sera na Tafiti kutoka Shirika la HakiElimu, Mwemezi Makumba amesema sekta ya elimu iangaliwe kwa jicho la kipekee na serikali ihakikishe inapanga bajeti inayoweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi na shule ili kuongeza ufaulu.

“Shughuli nyingi za maendeleo zinazohusisha mipango mfano ujenzi wa miundombinu mashuleni, uwekaji wa mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia. Unapomuweka mtoto shuleni ajifunze unazungumzia uwepo wa miundombinu, uwepo mazingira mazuri, vifaa na uwepo wa mabweni na hii ndio shughuli kubwa ya bajeti ya maendeleo ya elimu,” amesema Makumba.

Uwekezaji katika elimu ikiwemo mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ni hatua muhimu kuinua ufaulu. Picha na Mtandao

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa elimu wanaeleza kuwa juhudi za kuimarisha uelewa na ufaulu siyo za serikali na walimu pekee.

Naye Mhadhiri wa Chuo cha Ualimu cha Dar es Salaam(DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lulu Mhai amesema wazazi wanapaswa kushirikishwa kwenye masuala yote ya elimu ikiwemo kufahamu maendeleo ya watoto wao wawapo shuleni ili wafikie malengo ya ufaulu katika mitihani yao.

“Uelewa, elimu na ‘exposure’ (kujua jambo vyema) ya mzazi vina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya mwanafunzi kielimu,” amesema Dk Mhai.


Mkakati wa Serikali kukabiliana na ufaulu duni

Serikali inaeleza kuwa kwa sasa inawekeza katika miundombinu muhimu mashuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amesema wanaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya madarasa, shule na kujenga mabweni ili kuwasaidia wanafunzi kusoma karibu na shule ili kuongeza ufaulu wao.

“Tunaendelea kuboresha mazingira ya elimu ikiwemo maslahi ya walimu, watoto, kujenga madarasa na shule na kutoa hamasa kwa wazazi kuwapeleka watoto shule,” amesema DC Lyaniva.

Akisoma hutuba ya makaridio ya bajeti ya wizara ya elimu 2018/2019 mwanzoni mwa wiki bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Prof Joyce Ndalichako alisema kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R) kwa mwaka 2018/19 wametenga kiasi cha Sh140 bilioni kwa ajili ya kutoa motisha kwa shule za Msingi na Sekondari zilizofanya vizuri na zilizoongeza kiwango cha ufaulu katika Mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba na Kidato cha Nne mwaka 2018.


Related Post