Tamu, chungu: Ujenzi wa madarasa kidato cha kwanza 2023
- Watoa ajira na kuwatua mzigo wa gharama za elimu wazazi mkoani Mwanza.
- Wananchi wataka Serikali itupie macho uhana wa walimu.
- Serikali yasema itafanyia kazi mapendekezo yote ya wananchi.
Mwanza. Ni zaidi ya wiki mbili, tangu muhula mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari uanze Tanzania. Wazazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza huenda Januari wanaimaliza kwa tabasamu.
Tabasamu hilo limekuja baada ya kupunguziwa gharama za kuwapeleka watoto wao katika shule za Serikali hasa wanaoanza kidato cha kwanza.
Miaka ya nyuma walilazimika kuchangia fedha kwa ajili ya kujenga madarasa na kununua vifaa vya kujifunzia ikiwemo madawati na meza ili kufanikisha elimu ya watoto wao.
Mwaka huu umekuwa tofauti kwao kwa sababu Serikali kwa kutumia kodi, fedha za tozo na Uviko-19 imefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kupata mazingira bora ya kusomea.
Wazazi katika manispaa hii iliyopo jijini Mwanza wanasema kazi kubwa imefanyika ingawa bado jitihada zinahitajika kuhakikisha wanaboresha zaidi mazingira ya kujifunzia hasa kwa wanafunzi wanaoishi mbali.
Kulwa Shitobelo ni mkazi wa Mtaa wa Nyamanoro Manispaa ya Ilemela anasema angalau sasa Serikali imewapunguzia wazazi michango iliyokuwa inawabana miaka ya nyuma.
“Wazazi wengi walishindwa kupeleka watoto shule, michango ilikuwa mingi lakini kwa sasa angalau,” anasema Shitobelo huku akisema walizimika kuchangia vifaa vya ujenzi wa madarasa ikiwemo saruji na mawe.
Mkazi mwingine wa Ilemela mwenye watoto katika Shule ya Sekondari Kilangi, Mtemi Majaliwa anasema ujenzi huo umepunguza gharama kubwa kwa kuwa hivi sasa wananunua sare za shule pekee na madaftari tofauti na miaka ya nyuma ambapo walilazimika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kupeleka vifaa vingine shuleni.
“Siku ya kwanza mtoto kuripoti shule alilazimika kwenda na dawati la kukalia pamoja na vifa vingine kama ndoo, jembe na fyekeo lakini sasa tumepunguziwa michango ambapo mzazi hatalazimika kununua dawati tena badala yake mtoto ataenda kuripoti shule akiwa na vifaa vingine tu,” anasema Majaliwa.
Mzazi mwingine Yohana Elias, mkazi wa Buswelu Mwanza anasema mzigo wa ada uliokuwepo awali haupo tena na fedha hizo wanazitumia kwa shughuli nyingine za maendeleo na kulea watoto wao ili wawe na afya njema kuwawezesha kufanya vizuri darasani.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza wakiwa darasani katika Shule ya Sekondari Bujingwa wakiwa darasani. Picha | Mariam John.
Serikali ilivyowatua mzigo wananchi
Wanafunzi 85,300 waliomaliza elimu ya msingi mwaka jana mkoani Mwanza wamechaguliwa kujiunga shule za sekondari. Kati yao, wanafunzi 12,548 ni kutoka Manispaa ya Ilemela.
Ili kuwezesha wanafunzi kusoma bila kikwazo, Serikali ilitoa Sh19.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 983 kwa Mkoa wa Mwanza.
Kati ya fedha, Sh2.2 bilioni zilipelekwa Ilemela na kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 katika shule 23 za sekondari pamoja na viti na meza 5,500 na ofisi tatu ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Aporinaly Modest anasema halmashauri hiyo ilikuwa na uhitaji wa vyumba vya madarasa 252 kwa ajili ya wanafunzi 12, 548. Kati ya vyumba hivyo, upungufu ulikuwa ni vyumba 110.
Ujenzi wa vyumba hivyo ulikuwa kwa ajili ya wanafunzi 12,500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari 32 za Serikali kati ya shule hizo 23 ndiyo zilikuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa. Hata hivyo, siyo wanafunzi wote wameripoti shuleni.
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaitaka Serikali kuhakikisha shule zinakuwa na miundombinu bora na ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote katika ngazi za elimu na mafunzo.
Pia kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia ujenzi wa madarasa.
Zinazohusiana:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
-
Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufaulu vizuri
Walimu na wanafunzi wazungumza
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bujingwa, Emmanuel Makaranga anasema kitendo cha Serikali kuwajengea vyumba vya madarasa kumesaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi.
Anasema kwa sasa ni kuweka juhudi zaidi kwenye masomo ili kuhakikisha wanakipata kile ambacho wamekifuata shule na kutimiza ndoto zao.
“Tunakaa kwa kupeana nafasi, mwalimu akifundisha tunamwelewa vizuri kuliko ilivyokuwa awali ambapo mrundikano ulisababisha makelele na kutoelewa ufundishwaji,” anasema Makaranga.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Bujingwa Juliana Aron anasema tangu amejiunga na shule hiyo Januari mwaka huu, mazingira ya kusomea ni ya kurishisha.
“Napenda kuishukuru Serikali na wadau wote walioweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu hii na tunaahidi kusoma kwa bidii kwani miundombinu rafiki itatusaidia kusoma vizuri,” anasema Juliana wakati akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bujingwa iliyopo Kata ya Buswelu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Magweiga Magabe, anasema Sh160 milioni zilipokelewa shuleni hapo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane pamoja na kununulia viti na meza 400.
“Uwiano huo utafanya kila darasa wanafunzi watakaa 50 hivyo kuondokana na uwiano wa zamani wa wanafunzi 70 hadi 75 kwa darasa moja,” anasema Magabe.
Kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali, darasa moja linatakiwa litumiwe na wanafunzi wasiozidi 45 ili kumuwezesha mwalimu kumfikia kila mwanafunzi na kutoa uhuru wa kusoma.
Ujenzi wa vyumba hivyo umesaidia pia wanafunzi kuripoti shule kwa wakati ambapo mzazi analazimika kununua mahitaji ya mtoto kwa wakati.
“Hii inaongeza hamasa kwa wanafunzi kujifunza na kuwa wasafi kwakuwa watakaa kwenye madawati na mazingira ya shule yatakuwa mazuri na walimu watafanya kazi kwa bidii kwa sababu miundombinu ipo vizuri,” anasema mkuu huyo wa shule.

Monekano wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa na fedha za zilizotolewa na Serikali kuu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Picha | Mariam John.
Kazi bado ipo
Licha ya juhudi hizo za kujenga madarasa, siyo wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wameripoti shuleni.
Hadi kufikia Januari 23 mwaka huu, asilimia 62 ya wanafunzi 85,300 walikuwa wameripoti kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza katika shule zote za sekondari za Mkoa wa Mwanza.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martine NKwabi amesema haya sio mahuhurio mazuri waliyokuwa wanayakusudia.
Nkwabi amesema hadi sasa wanashangaa kwanini wanafunzi wanasuasua kuripoti shule na kwamba wameagiza mamlaka zote za chini kuhakikisha wanawakamata wazazi wote ambao watoto wao wamefaulu na hawajaenda shule.
“Tumetoa maagizo kwa viongozi wa ngazi za chini wenyeviti wa mitaa na watendaji kuhakikisha wanawakamata wazazi wote wanaokwepa kuwapeleka watoto wao shule,” anasema Nkwabi.
Anasema ni lazima mtoto aandikishwe, awe mwenye ulemavu na asiye na ulemavu na kuwa wazazi wasiogope michango kwa kuwa mzazi hadaiwi mchango wowote.
Pia baadhi ya wananchi wanasema huenda kutokana ujenzi wa madarasa hayo kujengwa kwa muda mfupi, huenda yasidumu muda mrefu.
Mkazi wa Ilemela, Hassan Abel anasema anapongeza Serikali kwa jitihada za kuhakikisha wanapunguza changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati kwa shule za sekondari.
Anasema pamoja na mafanikio hayo lakini anafikiri vyumba hivyo havijengwi kwa utaratibu unaofaa.
“Kwanza wanatumia matofali mabichi na wakati mwingine mbao za kupaua ni mbichi haya ni madhara ambayo hayawezi kuonekana kwa sasa ila kwa baadaye tunaweza kushuhudia vyumba hivyo vikianza kupasuka na kusababisha nyufa,” anasema Abel.
Mkakati ni mzuri lakini anasema ufanyike kwa kufuata ubora wa ujenzi wa vyumba hivyo ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza hapo baadaye.
Pamoja na kutatua changamoto hiyo ya madarasa lakini wazazi wanaomba Serikali iongeze kuajiri walimu wa kutosha ili kusaidia katika suala la ufundishaji.
“Na si kuajiri tu pia waboreshe mazingira ya walimu kuishi iwapo mwalimu ataishi karibu nae neo lake la kazi ufundishaji utakuwa bora zaidi sio kama saivi ambapo walimu wanaishi mtaani na wanalazimika kutumia usafiri kwenda shuleni,” anasema Elizabeth Nkilijiwa mkazi wa Nyamadoke jijini hapa.

Baadhi ya wanafunzi wa shule moja ya sekondari katika Manispaa ya Ilemela. Picha | Mariam John.
Viongozi waingilia kati ujenzi
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Sylvester Mrimi anasema awali kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa uliokuwepo ililazimu wanafunzi kuchaguliwa kwa awamu mbili kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza.
“Huko nyuma kabla ya mwaka jana tulikuwa tunafanya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa awamu mbili kwa sababu tulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.
“Ukichagua awamu ya kwanza wale ambao wanakosa nafasi ilikuwa tunakimbizana kutafuta michango kwa wafadhili, wadau na wazazi ili tuanze kujenga tukishakamilisha ujenzi ndiyo tunachagua wengine kwa awamu ya pili,” anasema Mrimi.
Pia walimu walikuwa wanapata ugumu kufundisha kwa sababu awamu ya kwanza ya wanafunzi inakuwa imeishafika mbali kujifunza na awamu ya pili wanapokuja katikati ya muhula wanakuwa na ujifunzaji ambao siyo mzuri.
Mrimi anasema lakini mwaka huu wanafunzi wote wameandikishwa kwa wakati mmoja, hivyo wanaamini kuwa changamoto hizo hazitajitokeza badala yake itaongeza ufaulu.
Ujenzi wa madarasa ni ajira
Ujenzi wa madarasa 110 Ilemela pia ulitoa fursa kwa vijana na wanawake kujipatia kipato. Halmashauri hiyo ilitoa ajira 1,412 za muda mfupi, kuwezesha Serikali kupata kodi kutoka kwa mafundi na wazabuni waliouza vifaa vyao katika ujenzi huku jamii ikipata ujuzi wa namna bora ya kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Angellah Kairuki anasema Serikali itaendelea kuboresha elimu kwa kuhakikisha inaweza mazingira bora na rafiki ya kujifunzia.
Waziri Kairuki anasema mwaka 2022, zaidi ya Sh300 bilioni zilizotokana na mradi wa Uviko-19 zilisaidia kujenga vyumba vya madarasa 15,000 kati ya hivyo, 12,000 ni kwa shule za sekondari.
Mwaka huu 2023, Serikali pia imetoa zaidi ya Sh160 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 ya sekondari nchi nzima.
Kairuki anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira mazuri ya kujifunzia ili kuongeza ufaulu na kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani.
Anasema tayari Serikali ina mpango wa kuendelea kujenga shule kwa kila jimbo la uchaguzi ambapo kwa kuanzia zaidi ya Sh1.2 trioni zimetolewa kwa ujenzi wa shule hizo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Tangazo

Latest