Fedha za Uviko-19 zitakavyosaidia kupunguza msongamano wanafunzi madarasani

December 21, 2021 11:45 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Naibu Waziri Tamisemi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Dk Festo Dugange akikagua Ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Ilemela ambavyo vimejengwa kwa fedha za Uviko-9. Picha|Mariam John.


  • Ni zilizotolewa na IMF kukabiliana na athari za Uviko-19.
  • Zimejenga madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.
  • Wanafunzi watasoma katika madarasa ya kisasa.

Mwanza. Wakati baadhi ya halimashauri zikijikongoja kukamilisha ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2022, wanafunzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza hawana hofu ya kukosa madarasa mwakani.

Halmashauri hiyo imefanikiwa kujenga madarasa 97 katika shule za sekondari 26 kwa kutumia Sh1.8 bilioni ambazo ni sehemu ya msaada wa dharura wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) zilizotolewa kwa Tanzania kukabiliana na athari za Uviko-19.

Awali manispaa hiyo ilikuwa na uhitaji wa vyumba vya madarasa 211 kwa ajili ya wanafunzi 10,662 kwa mwaka  2022, vyumba viliyokuwepo ni 114 na upungufu  vilikuwa 97.

Pia kwa kutumia fedha hizo imejenga ofisi 28 za walimu na kutengeneza madawati 4,850.

Tofauti na miaka iliyopita mwaka huu wanafunzi wote10,662 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani watasoma kwenye vyumba vya madarasa na hawatachangia meza na kiti.

Nukta habari imezungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ibinza katika manispaa hii ambao wamesema wakati wanaenda kuanza masomo ya kidato cha kwanza shule haikuwa na vyumba vya kutosha na waliruhusiwa kwenda na viti vya plastiki kwa ajili ya kujifunzia.

“Tulisoma kwa msongamano, tulilazimika kuchangia chumba kimoja wanafunzi 90 na pia tulilazimika kuchangia meza moja wanafunzi wawili au watatu, hali haikuwa nzuri kwa kuwa tulisoma kwa kubanana,” amesema Renatus Paul, mwanafunzi kidato cha pili.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Neema Shinje amepongeza juhudi za Serikali kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo ambao utapunguza changamoto iliyokuwa inawakabili awali.

“Tulisoma kwa wasiwasi hasa ukizingatia mlipuko wa ugonjwa wa Uviko- 19, kutokana na msongamano uliokuwepo tulihofia kuambukizana,” amesema Neema.


Zinazohusiana: 


Suala hilo pia limewagusa wazazi wa wanafunzi wanaoenda kuanza masomo mwakani ambapo wamesema fedha za IMF zimewapunguzia mzigo wa gharama za kuwasomesha watoto wao ikiwemo michango ya kununua madawati.

Nukta habari imetembelea baadhi ya shule zilizojengewa madarasa hayo na kukuta madarasa yaliyokuwa yanajengwa kwa nguvu za wananchi hayajakamilika. 

“Ni jambo la kupongeza, kwa miaka mingi tumeishi kwa kuchangia fedha kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa, lakini kwa sasa tumepunguziwa mzigo,” amesema  mkazi wa Ilemela, David Okupasi.

Akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri za Ilemela na Nyamagana leo Desemba 21, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Dk Festo Dugange amepongeza ujenzi wa vyumba hivyo ambavyo vimejengwa kisasa na vimezingatia ubora  na thamani ya fedha.

Amesema amefurahishwa na namna halmashauri hizo zilivyomalizia vyumba hivyo ambavyo vitasaidia wanafunzi kusoma kwenye mazingira mazuri na walimu watafundisha kwenye mazingira mazuri.

Mwonekano wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwenye shule 25 vya sekondari katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Vyumba hivyo vimejengwa kwa fedha za Uviko-19. Picha|Mariam John.

Serikali yatoa maagizo mazito

Dk Dugange ametoa siku 10 kwa halmashauri zote nchini ziwe zimekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 vilivyobaki.

Vyumba vyote hivyo ni kwa shule za sekondari na za msingi shikizi.

“Bado tunasisitiza kwa halmashauri zote kuhakikisha zinakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ifikapo Desemba 30 mwaka huu ili wanafunzi wote waliochaguliwa waweze kujiunga na mwaka huu hatuna chaguo la kwanza na pili hivyo wanafunzi watatakiwa kujiunga wote kwa wakati mmoja,” amesema Dk Dugange

Dk Dugange amesema mkoa wa Mwanza ulipokea zaidi ya Sh20.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,017 na kwamba ujenzi kwenye vyumba hivyo umefikia asilimia 82.

Akifafanua amesema Sh1.9 bilioni  zilipelekwa katika Halmashauri ya jiji la Mwanza ambapo ujenzi katika vyumba hivyo umefikia asilimia 90 na Sh1.9 bilioni zilipelekwa katika Halmashauri ya Manispaa ya IIemela ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

“Nimefurahishwa na ujenzi unaoendelea na hii imedhihirisha thamani ya Sh20 milioni ambayo inatosheleza kujenga chumba kimoja cha darasa, viti na meza ziko vizuri kifupi thamani ya fedha imeonekana,” amesema Dk Dugange.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW