Corona: Sh90.2 bilioni za IMF zitakavyoinua utalii Tanzania

October 17, 2021 9:57 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kati ya Sh1.3 trilioni ilizopata Tanzania kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).
  • Fedha hizo zitatumika kutangaza utalii, kuimarisha miundombinu.
  • Pia zitanunua vifaa vya kujikinga na Uviko-19 na kusambaza chanjo.

Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itazitumia Sh90.2 bilioni za mgao wa mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) katika maeneo makuu matano ikiwemo kukarabati na kujenga miundombinu ya utalii ili kukabiliana athari za janga la Corona (Uviko-19) katika sekta hiyo na kuongeza watalii wanaotembelea Tanzania.

Tanzania ilipata mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka IMF ambao unatakiwa kutumika ndani ya miezi tisa ili kukabiliana na athari za Uviko-19 katika sekta mbalimbali na kuinua uchumi.

Katika mgao wa fedha hizo, Wizara ya Maliasili na Utalii imepata asilimia 6.9 ya fedha zote ambapo zimeelekezwa kutekeleza maeneo matano na miradi 23 ya kimkakati.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Damas Ndumbaro aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaaam leo Oktoba 17, 2021 amesema eneo la kwanza litakuwa kuimarisha utendaji wa taasisi tano za wizara hiyo kwa kuziwezesha kuboresha miundombinu na kununua vifaa mbalimbali.

Taasisi hizo ni Shirika la Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Sanaa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

“Ujenzi na ukarabati wa barabara takriban kilomita 4,881 ambazo zitaenda kutumia Sh23.4 bilioni. Barabara hizo ndiyo miundombinu pekee muhimu kuwawezesha watalii kuingia katika hifadhi zetu.

“Kipindi cha Uviko-19 kutokana na kupungua kwa watalii na mapato yatokanayo na utalii kiasi cha kufanya taasisi hizo kushindwa kujiendesha, miundombinu nayo imeharibika,” amesema Dk Ndumbaro. 

Amesema uboreshaji huo wa miundombinu utafanyika katika hifadhi za Taifa za Serengeti, Mkomazi, Tarangire, Nyerere, Kilimanjaro, Saadan, Gombe, Ngorongoro pamoja na na maeneo ya misitu 10.

Hifadhi za Tanzania zimesheheni vivutio mbalimbali vya utalii wakiwemo wanyama. Picha| Nukta.

Pia fedha hizo zitatumika katika ununuzi mifumo ya kielektroniki kufanya ufuatiliaji katika taasisi mbalimbali, mitambo ya ujenzi, kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nane ndani ya hifadhi ikiwemo Serengeti na kujenga mageti matano katika baadhi ya hifadhi.

Sambamba na hilo wizara hiyo inaenda kuboresha na kudhibiti ubora wa huduma za utalii ambazo zimeshuka sana wakati wa Uviko-19 ikiwemo hoteli, kutoa mafunzo na kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato katika vituo vya utalii.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya watalii imeongezeka mwaka huu na inaweza kuvuka matarajio ya awali yaliyowekwa. Kati ya Januari hadi Septemba 30 mwaka huu, Tanzania imepokea watalii wa kimataifa 623,800.

Idadi hiyo iko juu ikilinganishwa na watalii 620,000 walioingia Tanzania kati ya Januari na Desemba mwaka jana. 

Dk Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini amesema eneo namba mbili linahusu kuimarisha masoko na kutangaza utalii ambapo wizara itakarabati vituo saba vya urithi wa kiutamaduni na  kununua vifaa kwa ajili ya kutolea taarifa za utalii kwa njia ya kidijitali.

“Lakini pia tunafahamu “Royal Tour” alikwenda Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) akaifikisha, sisi hatutaki ipoe. Sisi tunakwenda kutanua wigo wa “Royal Tour” kutangaza zaidi vituo hivyo, Mheshimiwa Rais asingeweza kwenda kwenye kila kituo,” amesema Dk Ndumbaro.

Pia Wizara itashiriki na kuwezesha maonyesho makubwa mawili ya utalii ya kimataifa ili kutangaza zaidi vivutio vya utalii.

“Eneo tatu tunakwenda kuimarisha mazingira ya biashara ya utalii kwa kuhakikisha kwamba usalama na huduma za afya katika vituo vya utalii zinakuwa katika kiwango cha kimataifa,” amesema waziri huyo.

Amesema hakuna mtalii atakayekuja Tanzania kama usalama na huduma za afya zinalega lega.

“Kwenye hili tutashirikiana na wenzetu wa Tamisemi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya. Tutaendelea kusisitiza upatikanaji wa chanjo katika maeneo ya utalii,” amesema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa fedha hizo zitawezesha kuwepo kwa vifaa vya kupima Uviko-19 katika vituo vya utalii.

Katika eneo la nne, wizara hiyo ambayo inategemewa zaidi katika kukuza uchumi wa Taifa, fedha hizo zitatumika kushirikisha sekta binafsi kuwajengea uwezo kukabiliana na janga la Uviko-19.

Hiyo itahusisha kununua na kuvigawa vifaa vya kujikinga na Uviko-19 kwa sekta binafsi inayohusika na utalii na kutoa mafunzo ya jinsi ya kuvitumia. Mafunzo zaidi ya kujikinga na ugonjwa huo yatatolewa kwa wadau hasa katika mikoa ambayo yameathirika zaidi katika wa utalii.

Mikoa ambayo imeathirika zaidi na Uviko-19 katika sekta ya utalii ni Ruvuma, Mtwara, Lindi, Mbeya, Njombe, Mwanza na Mara ambayo mwaka jana haikupata kabisa watalii.

Fedha hizo za IMF pia zitatumika kuimarisha mifumo ya kidijitali ya takwimu za utalii ambazo zinahusisha idadi ya watalii wanaotembelea katika hifadhi, mapato yanayopatikana na muda wanaotumia kukaa katika maeneo hayo.

Huenda utekezaji wa maeneo hayo matano ya wizara hiyo yakasaidia sekta ya utalii kuimarika, jambo litakalosaidia kuimarisha uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV