Hisabati, Kiingereza bado pasua kichwa mitihani darasa la Saba Tanzania

Nuzulack Dausen 0500Hrs   Oktoba 16, 2019 Habari
  • Ufaulu wa Hisabati washuka kidogo kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana.
  • Kiingereza ndiyo somo ambalo lina ufaulu mdogo zaidi huku wadau wakiomba juhudi zaidi kufanyika kuwaokoa watoto.

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PLSE) au maarufu kama darasa la Saba huku yakionesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa takriban asilimia 4 kutoka mwaka jana.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde aliwaambia wanahabari kuwa pamoja na matokeo hayo, ufaulu wa masomo ya Kiswahili, Maarifa ya Jamii, Kiingereza na Sayansi ulipanda kati ya asilimia 1.83 hadi asilimia 6.86.

Wakati ufaulu wa masomo hayo ukipanda, Kiingereza na Hisabati yameendelea kuwa pasua kichwa. Safari hii ufaulu wa Hisabati umeshuka kidogo kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka 2018.

Katika matokeo yaliyotangazwa jana (Oktoba 15, 2019) Hisabati ina wastani wa ufaulu wa takriban asilimia 65 ikilinganishwa na asilimia 66 iliyorekodiwa mwaka jana. Mwenendo wa ufaulu wa somo hilo umekuwa ni wa kupanda na kushuka na mwaka huu upo chini ya wastani wa jumla wa ufaulu kimasomo wa asilimia 73.

Somo la Kiingereza ama English Language kwa lugha ya kimombo, lenyewe licha ya ufaulu wake kupanda kidogo kwa takriban asilimia nne mwaka huu, bado ndiyo somo lenye ufaulu wa chini zaidi kwa mujibu wa Necta. 

Kiingereza lina ufaulu wa asilimia 53.2 ikiwa ni ahueni kidogo kutoka asilimia 49.6 iliyorekodiwa mwaka 2018.


Zinazohusiana: 


Hii ina maana kuwa kati ya wanafunzi 932,095 wenye matokeo, kwa mujibu wa Necta, wanafunzi 436,147 walifeli Kiingereza wakipata alama D na E. Kwa lugha nyingine takriban nusu (asilimia 47) ya wanafunzi walifeli, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na takriban mwanafunzi mmoja kati ya 10 katika somo la Kiswahili.

“Takwimu za matokeo zinaonesha kuwa ufaulu katika somo la Kiingereza bado uko chini ukilinganishwa na masomo mengine pamoja na kuwa unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka. Hivyo, juhudi za makusudi zinahitajika kuendelea kufanyika ili kuinua kiwango cha ufaulu wa somo hili,” Dk Msonde aliwaambia wanahabari.

Ifahamike kuwa somo lilofanya vizuri zaidi katika matokeo hayo ya mtihani wa darasa la Saba ni Kiswahili likifuatiwa na Sayansi na Maarifa ya Jamii. Wanafunzi wa darasa la saba huketi kufanya mitihani mitano.

Ufaulu usioridhisha wa masomo ya Kiingereza na Hisabati unaibua mjadala juu ya mustakabali wa Tanzania katika kuwaandaa vijana na fursa zilizopo ulimwenguni za kibiashara, sayansi na teknolojia ili kushindana na nguvukazi ya mataifa mengine yenye mfumo imara wa elimu.

Somo la Kiingereza ama English Language kwa lugha ya kimombo, lenyewe licha ya ufaulu wake kupanda kidogo kwa takriban asilimia nne mwaka huu, bado ndiyo somo lenye ufaulu wa chini zaidi kwa mujibu wa Necta. Picha|Mtandao.

Wadau wanaeleza msingi dhaifu wa wanafunzi katika uelewa katika elimu ya msingi unaathiri ufanisi katika kujifunza katika elimu ya juu na hata wanapoingia katika majukumu ya kazi au kufanya biashara siku zijazo.

“Ukiangalia insha za wanafunzi wa elimu ya juu zilizoandikwa kwa Kiingereza kuna wakati unastaajabu kabisa…hivi huyu ni mwanafunzi aliyefika hadi ‘form six’ (kidato cha sita)?...kutokana kutokuwa na viwango. Hata barua za kazi wanazoandika bado ni balaa…hii ni kwa sababu ya msingi mbovu katika elimu ya msingi,” amesema Jamal Maringo, Mratibu wa Matukio wa Chama cha Walimu wa Kiingereza Tanzania (TELTA).

Maringo anasema sababu kubwa ya wanafunzi kutofanya vizuri katika somo la Kiingereza ni walimu wengi hususan wa umma kutumia “mbinu za kizamani” kufundishia, jambo linalopunguza ufanisi wa wanafunzi kuelewa vizuri somo hilo ikilinganishwa na shule za binafsi.

“Ufundishaji wa kuhubiri kwenye darasa lenye wanafunzi wengi hauna afya na unapunguza ‘critical thinking’ (uwezo wa kufikiri kwa kina). Inatakiwa mwalimu ufundishe kwa vitendo,” amesema.

Maringo, ambaye ni mwalimu wa Kiingereza, amesema mbinu ya kutengeneza jumuiya za walimu kujifunza (Community of practice) katika kila kata itasaidia kuondoa changamoto ya maarifa na kuwasaidia walimu kujifunza mbinu mpya.

Related Post