Ilemela kumaliza tatizo la madawati ifikapo Septemba
Mwonekano wa sehemu ya madawati 12, 000 yaliyotengenezwa kutokana na fedha za ndani ambapo yamegawiwa kwenye shule 24 zenye mahitaji makubwa. Picha |Mariam John.
- Ni madawati 7,158 yanayohitajika shule za msingi.
- Kila baada ya miezi miwili au mitatu kutengeneza madawati zaidi ya 1,000.
Mwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imesema itahakikisha inakamilisha upungufu wa madawati 7,158 yanayohitajika katika shule za msingi wilayani humo ifikapo Septemba mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema mkakati huo ni makubaliano yaliyofikiwa kwenye Baraza la Madiwani kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kutengeneza madawati hayo.
“Tumekusudia kumaliza upungufu huo wa madawati ili nguvu zielekezwe kwenye mambo mengine ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na vyoo kwa wanafunzi wa shule ya msingi ambapo hivi sasa upungufu ni mkubwa,” amesema Masala leo Machi 1, 2022.
Amesema katika zoezi hilo watahakikisha kila baada ya miezi miwili au mitatu watakuwa wanakabidhi madawati zaidi ya 1,000 ili kufikia lengo tarajiwa la kumaliza changamoto hiyo ndani ya mwaka huu.
Awali, Afisa Elimu Vifaa na Takwimu Idara ya Elimu Msingi, Hellen John amesema halmashauri hiyo inahitaji jumla ya madawati 27,153 yaliyopo ni 19,995.
Hiyo ni sawa na upungufu ni madawati 7,158.
Amesema kupitia mkakati wa kupunguza madawati, hivi sasa halmashauri imetengeneza madawati 1,245 yenye thamani ya Sh90 milioni, fedha zilizotokana na makusanyo ya ndani.
Mbali na madawati hayo, pia halmashauri imefanikiwa kujenga vyumba sita vya madarasa mapya, ukamilishaji wa vyumba 27 vya madarasa, matundu sita ya vyoo na nyumba moja vikiwa na jumla ya Sh327 milioni.
“Katika kipindi hiki cha kutekeleza mkakati wa kupunguza changamoto za miundombinu na madawati katika shule za msingi, halmashauri imetumia zaidi ya Sh400 milioni,” amesema Hellen.
Zinazohusiana:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
- Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba
- Hisabati, Kiingereza bado pasua kichwa mitihani darasa la Saba Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amepongeza jitihada zinazofanywa na halmashauri hiyo na kuagiza zingine ziige mfano huo ili kuondokana na changamoto hizo.
“Viongozi katika wilaya hii wamekubali kuleta maendeleo ya kimapinduzi hivyo ni vema waungwe mkono kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa sawa,” amesema Mhandisi Gabriel.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza injinia wa halmashauri ya Ilemela kufanya ufuatiliaji kwenye shule zote zenye changamoto ya eneo ili zianzishiwe majengo ya ghorofa.
Alitoa siku 14 kwa injinia huyo kupeleka andiko la mradi wa ujenzi wa ghorofa katika Shule ya Msingi Mwenge ili lianze kujengwa mara moja.
“Leteni mpango huo mara moja ili mimi niweze kutafuta fedha za kujenga ghorofa hilo, hii itasaidia kupunguza changamoto ya eneo lakini pia itaondoa mrundikano wa shule tatu ndani ya eneo moja,” amesema Gabriel.
Latest