Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba

Mwandishi Wetu 0518Hrs   Oktoba 15, 2019 Habari
  • Wamefutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanya udanganyifu.
  • Imesema tayari wameshazitaarifu mamlaka za ajira na sheria ili ziwachukulie hatua waliohusika na udanganyifu huo.
  • Asilimia 81.5 ya watahiniwa 933,369 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Dar es Salaam. Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) limesema watahiniwa 909 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 wamefutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanya udanganyifu. 

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde aliyekuwa akitangaza matokeo ya darasa la saba leo (Oktoba 15, 2019) amesema kuwa katika matokeo hayo asilimia 81.5 ya watahiniwa 933,369 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Ufaulu huo ni sawa na ongezeko la asilimia 3.78 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka jana, huku wanafunzi 909 wakifutiwa matokeo kwa kuhusika na udanganyifu. 

Dk Msonde amesema katika huo uliofanyika Septemba 11-12, 2019 wamebaini kuwa baadhi ya Walimu Wakuu, wasimamizi na walinzi walihusika kufanya udanganyifu. 

Amesema katika kikao kilichokaa leo tayari wameshazitaarifu mamlaka za ajira na sheria ili ziwachukulie hatua waliohusika na udanganyifu huo. 

Hata hivyo, udanganyifu kwa ujumla umepungua ambapo mwaka 2011 ulikuwa 9,736 na mwaka huu umefikia 909.


Zinazohusiana:


Pia amesema mwanafunzi aliyeongoza kitaifa ni Grace Manga kutoka Shule ya Msingi Graiyaki ya mkoani Mara, akifuatiwa na Francis Gwagi kutoka Shule ya Msingi Paradise ya Geita.

Aliyeshika nafasi ya tatu ni Loi Kitundu kutoka Shule ya Msingi Mbezi ya Dar es Salaam, na Victor Godfrey kutoka Graiyaki ameshika nafasi ya nne.

"Katika ufaulu wa masomo, somo la Kiswahili, Kiingereza na Sayansi katika mtihani huo ufaulu wake umepanda na somo la Hisabati umeshuka," amesema Dk Msonde. 

Ufaulu wa somo la hesabu umeshuka kwa asilimia 1.05 ukilinganishwa na mwaka uliopita wa 2018. 

Related Post