Felister Kulwa: Mwanamke shupavu anayetaka kuwa mfugaji mkubwa Tanzania
- Ni miongoni mwa wanawake wanaoishi vijijini wanapambana kujikwamua na umaskini.
- Ana ng’ombe 10 anaowafuga kienyeji.
- Ndoto zake ni kufuga kisasa ili kufaidika na ufugaji.
Maswa, Simiyu. Katikati ya pori nene Felister Kulwa yupo na mtoto wa miaka 10 hivi akichunga ng’ombe katika eneo dogo la majani lililozungukwa upande mwingine na mashamba.
Ana zaidi ya Saa moja hapa tangu ameleta mifugo yake kwa ajili ya malisho baada ya kumaliza shughuli za shambani ambako amelima pamba, mahindi na alizeti.
Muda wote anazunguka huku na kule akiirudishe mifugo isile mazao yaliyopo mashamba ya jirani.
Haya yamekuwa maisha ya Felister mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa kwa takriban muongo mmoja sasa baada kumpoteza mmewe kipenzi.
“Nilianza kuchunga ng’ombe muda mrefu sana…nilianza na ng’ombe wawili lakini kwa sasa ninao zaidi ya 10, wanazidi kuongezeka kila siku,” anasema.
Felister ni miongoni mwa wanawake wanaoishi vijijini nchini Tanzania ambao wanapambana kujikwamua na umaskini.
Safari ya Felister katika ufugaji ilianza baada ya kufariki kwa mumewe huku akimuachia watoto tisa ambao kwa hali ya kiuchumi ya wakati huo ilikuwa ngumu kwa yeye kuwatunza bila shughuli imara ya kiuchumi.
Wakati huo, wanawe walikuwa wadogo wanaenda shule na hakuona sababu ya kuzuia wasiende kusoma ili kumsaidia kuchunga kama ambavyo imeripotiwa katika baadhi ya jamii za wafugaji nchini.
“Alipofariki mume wangu nilianza kuchunga, watoto walikuwa wanaenda shule nilibaki nyumbani pekee yangu, ilinilazimu nianze kuchunga mwenyewe,” anasema Felister.
Felister Kulwa akiwa porini na ng’ombe wake kuhakikisha wanapata chakula. Mama huyu amekuwa akitumia ufugaji kama nji ya kujiongezea kipato. Picha| Nuzulack Dausen.
Hadi sasa kupitia ufugaji, Felister amefanikiwa kuwapeleka watoto wake wote shule na wengine kuanza kujitegemea.
Kwa kipindi chote ambacho ameanza ufugaji, Felister ameona kuwa ufugaji wa kienyeji si rafiki na unazidi kumpatia changamoto kadri siku umri unavyoenda na ni ghali zaidi wakati ambao ukame unazidi kusambaa maeneo mengi Tanzania.
Mwishoni mwa mwaka 2021 ilimlazimu kuuza ng’ombe mmoja ili kupate fedha za kununua pumba ili kuwalisha ng’ombe wake ambao walikuwa wamekosa malisho kutokana na ukame.
Mama huyo anasema ukosefu wa miundombinu muhimu kama josho katika ufugaji vimefanya aongeze gharama za ufugaji.
Kukabiliana na changamoto hizo, amejiongeza na sasa hununua dawa katika maduka ya wanyama Maswa na kuja kuwapulizia ng’ombe ili waweze kuwa na afya bora.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
- Mikakati ya kuboresha upatikanaji wa maji Maswa
- Binti wa miaka 22 anayepambana kuung’oa umaskini Kanda ya Ziwa
Pamoja na kuwa hana elimu kubwa ya ufugaji anasema amechoka kufuga kienyeji na kwamba anataka kuwa mmoja ya wafugaji wakubwa wa kisasa kuongeza tija.
“Nataka nianze kufuga kisasa mimi ni mama mjane, nimeona hii kazi ya kuchunga ni ngumu nataka nibadilishe ili nisipate tabu ya kuja porini,” anasema Felister.
Felister anasema akikamua ng’ombe mmoja huwa anapata nusu lita ya maziwa ili hali wale ng’ombe wa kisasa hutoa hadi zaidi ya lita mbili za maziwa.
Mwamko wa Felister ni tofauti na wakazi wengi wa wilaya ya Maswa ambao bado wanafuga kienyeji na baadhi hawana mpango wa kujaribu kufuga kisasa.
Ufugaji duni ni moja ya matatizo yanayowakabili wakazi wa Maswa kiasi cha kuwafanya baadhi ya wadau wa maendeleo wakiwemo waraghbishi kulivalia njuga ili kuongeza tija kwenye shughuli hiyo muhimu ya uchumi nchini.
“Kufuga ng’ombe wa kisasa hawana gharama, ukiwapatia Majani na kuwatibu vizuri unapata maziwa mengi. Hawa wakienyeji maziwa hawana na kuwapatia chakula ni changamoto.
Kutimiza ndoto zake, amepanga kuuza baadhi ya ng’ombe zake ili anunue ng’ombe wa kisasa watatu kama kianzio.

Ukosefu wa mitaji ni moja ya changamoto kubwa inayowarudisha nyuma wanawake wanaojishuhulisha na kilimo na ufugaji.
Ripoti ya Sensa ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2019/20 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa wanakaya 294,618 walipata mikopo kutoka kwa vyanzo mbalimbali na ni 77,201 au robo tu (asilimia 26.2) walikuwa ni wanawake.
Hii ina maana kuwa wanaume waliopata mikopo kuendesha shughuli zao za kilimo na ufugaji walikuwa mara tatu ya wanawake.
“Serikali inapaswa kuja hapa watupatie elimu ya kufuga kisasa, sisi tuna ufugaji duni. Ni watu tuliotekelezwa. Kwa sababu ng’ombe wa kisasa tunaowana hata mjini, mtu anafuga wachache na kupata maziwa mengi,” anasema.
Kwake, anaamini ufugaji wa kisasa hauna gharama kubwa kama wa kienyeji ambao humpa shuruba ya kuzunguka porini kusaka malisho.