Mfugaji anayeongoza safari ya ufugaji wa kisasa Simiyu

April 9, 2022 8:15 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Alianza kwa kufuga mbuzi wa kisasa na sasa amekuwa mwalimu wa kijiji kufuga kisasa. Katika kijiji kizima ni yeye tu ana ng’ombe wa kisasa.
  • Anasema ufugaji wa kisasa utamfanya “auage umaskini”.
  • Serikali inasema itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya mifugo kuongeza tija katika uzalishaji.

Maswa, Simiyu. Baada ya kumaliza shughuli zake za kilimo, Shidile Nkonya anawapeleka ng’ombe wake kwenye eneo dogo la malisho lililopo pembezoni mwa barabara ya kwenda Bariadi mkoani Simiyu.  

Tofauti na wafugaji wenzie wa Kijiji cha Gula wilayani Maswa wenye idadi kubwa ya mifugo, Nkonya ana ng’ombe watatu tu wa kisasa na mbuzi mmoja.

Ni mmoja wa wafugaji wachache katika wilaya hii ya kanda ya ziwa waliojikita kufuga kisasa ili kuongeza tija.

Kilichomfanya afuge ng’ombe wa kisasa, anasema, ni kwa sasabu wana faida kubwa licha ya idadi yao kuwa ndogo.

“Namna ya uchungaji wa ng’ombe wa kisasa ni rahisi siyo kama wale wa kienyeji ambao ni wengi na unasumbuka kuwachunga kwenye maeneo makubwa ukizingatia siku hizi maeneo ya malisho ya yamekuwa madogo,” anasema Nkonya.

Sehemu kubwa ya wafugaji katika eneo hili kwa mujibu wa asasi ya kiraia ya Kasodefo wanafuga kienyeji jambo linalowapunguzia tija hasa kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na vipindi vya ukame katika maeneo mbalimbali.

Ufugaji usio na tija ni moja ya changamoto zinawazokabili wafugaji wa wilaya hii ya Maswa na sasa wadau wakiwemo waraghbishi, Serikali na asasi za kiraia wanapambana kusambaza maarifa kwa wakazi hawa.

Tayari kuna watu ambao wamekuwa mstari wa mbele kama Nkonya katika kuitikia wito wa kufuga kisasa na ameanza kuwa mmoja ya watu wa kutegemewa kusambaza maarifa katika kijiji chao kilichopo kusini mwa Maswa.

Ufugaji wa kisasa wamwongezea kipato

Anasema ng’ombe wa kienyeji mwenye afya nzuri anaweza kutoa maziwa kati ya lita moja hadi mbili kwa wakati yule wa kisasa kama wake aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa kati ya lita nane hadi 10 kwa siku.

Kipato kinachopatikana, Nkonya anayepata Sh10,000 kila siku kwa kuuza maziwa anasema kimemsaidia kumuondoa katika dhiki kwa kuwa kwa sasa anamudu gharama za maisha ikiwemo kuwapeleka watoto shule na hata kukidhi mahitaji makubwa ya kifedha.

“Bado sijauaga umaskini kwa sasa,” anasema kwa kucheka ila “kama Mungu akinijalia ninaweza kuuaga umaskini.”

Kwa mujibu wa Nkonya hutumia wastani wa Sh10,000 kwa mwezi kununua pumba na kiwango hicho huzidi kidogo pale anapokuwa anahitajika kuwapatia dawa.

Madaktari wa Serikali humpunguzia maumivu

“Madaktari wa mifugo wa Serikali huwa wanakuja bure kunipa ushauri wa namna bora ya kuwafuga ila kwenye masuala ya kuwachoma sindano sasa nimekuwa kama mtaalamu,” anaeleza huku akitabasamu.

Ufugaji wa kisasa unampunguzia maumivu ikilinganishwa na wenzie wa wanaofuga kienyeji kama Ndirana Jijungu mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa aliyepoteza ng’ombe wa kienyeji wanne kati ya sita mwishoni mwa mwaka 2021 kutokana na ukosefu wa malisho na maji.

Mfugaji wa kisasa Shidile Nkonya wa Kijiji cha Gula wilayani Maswa sasa amekuwa mwalimu wa wengine wa kuwafundisha namna bora ya kufuga. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta. 

Jijungu ni mmoja ya watu ambao wamerudi nyuma katika jitihada za kujikwamua na umaskini kwa kutokana na kutokuwa na maarifa stahiki ya kufuga kisasa na njia za kupunguza hasara kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hana maumivu kama wafugaji wa kienyeji

Kwa kuwa alikuwa anafuga kienyeji kwa ajili ya kulimia, Ndirana yeye anahisi suluhu ya matatizo yake ni kuanza kuwekeza kwenye matrekta ya mkono ya kulimia badala ya kutegemea ng’ombe ambao anasema “wanakufa kufa kila siku”.

Hii ni tofauti kwa mwezie Felista Kulwa wa kijiji hicho mwenye ng’ombe 10 ambaye kwa sasa ana haha kupata maarifa na mtaji ili angalau afikie kiwango alichofikia Nkonya cha kufuga kisasa.

Kwa sasa Felister anapata maziwa kidogo tu ikiwa ni robo tu ya yale anayopata mwenzie Nkonya mwenye ng’ombe watatu akiwemo ndama.

Ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa ng’ombe wa kienyeji hutoa wastani wa lita tatu za maziwa kwa siku ikiwa ni chini ya mara tatu ya maziwa anayozalisha ng’ombe wa kisasa. 

Kwa Tanzania Bara, ripoti hiyo inabainisha kuwa ng’ombe wa kisasa huzalisha lita tisa wakati wa masika na lita nane wakati wa kiangazi wakati visiwani Zanzibar ng’ombe wa kisasa huzalisha wastani wa lita 10 wakati wa masika na lita tisa wakati wa kiangazi. 

“Nitauza baadhi ya ng’ombe wangu ili ninunue wa kisasa wenye faida nyingi,” anasema Felister.

Changamoto kama zote

Pamoja na kuwa baadhi ya wafugaji hapa wanataka kuwekeza zaidi kufuga kisasa bado wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazorudisha jitihada zao ikiwemo ukosefu wa majosho ya kuogeshea mifugo, ukosefu wa mitaji na mabadiliko ya tabianchi yanayohatarisha upatikanaji wa malisho na maji.

“Kuwapata ng’ombe wa kisasa ni ngumu sana,” anasema Nkonya kwa sababu katika wilaya hiyo ni adimu sana.

“Mfano, kwa hapa kijijini ni mimi pekee yangu ndiyo nina ng’ombe wa kisasa,” anasema.

Nkonya anasema yeye alianza kwa kununua ndama jike mwenye miezi miwili kwa Sh500,000 kutoka kwa mmoja ya wafugaji wa kisasa mkoani Shinyanga anayeishi zaidi ya kilomita 100 kutoka kijijini kwao.


Soma zaidi: 


Safari ya Nkonya kabla ya kufuga ng’ombe wa kisasa anasema ilianza kwa kufuga mbuzi wa kisasa ambao aliwauza na kununua ndama huyo wa kisasa kama mtaji.

“Nina mpango wa kuongeza ng’ombe wengine zaidi lakini nimeona niwatunze hawa kwanza wazaliane ndiyo nifanye uamuzi wa kuwaongeza,” anasema mfugaji huyo.

Mwalimu wa kijiji ufugaji wa kisasa

Ili kusambaza elimu hii, Nkonya yeye amekuwa akifundisha wanakijiji wenzie namna ya kufuga kisasa na mbinu ambazo wanaweza kutumia kupata mitaji na kuiikinga mifugo yao na maradhi.

“Wapo wengi wananifuata wananiomba elimu na wanaomba niwauzie ng’ombe wa kisasa na tayari nimeshauza wawili,” anasema.

Kwa Felister mbali na kulia mtaji ili aanze kufuga kisasa, anasema Serikali inapaswa kuwapatia wafugaji elimu ya ufugaji wa kisasa na mikopo isiyo na masharti makali ili nao waweze kupata faida.

Mtaalamu wa mifugo kutoka Azolla Feeders Dk Mzee Torokoko anasema wafugaji wanatakiwa kuelimishwa namna bora za kufuga kisasa ikiwemo kuandaa maeneo maalumu ya kulima malisho ya mifugo.

Shidile Nkonya alisha mifugo yake katika shamba lake la malisho lilopo pembezoni mwa barabara ya kuelekea Bariadi mkoani Simiyu. Ufugaji wa kisasa umesaidia kumpunguzia makali ya maisha. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta. 

Uwekezaji wa elimu, mitaji suluhu ya vyote

Uwekezaji wa elimu na utoaji wa mikopo rafiki, anasema utawasaidia wafugaji wengi wa kienyeji kumudu gharama za ufugaji kisasa kama kununua mbegu bora na kuzalisha chakula cha mifugo kijulikanacho kama hydroponic chenye tija.

Dk Torokoko anasema nyasi hizo huzaliana kwa wingi na kutoa kiwango kikubwa cha malisho ambayo yanaweza kuifadhiwa hata kwenye handaki kavu na kutumika kipindi chenye ukame.

Kupitia maofisa mifugo, Serikali inasema inaendelea kuwekeza kuboresha sekta ya mifugo kwa kujenga au kukarabati majosho, kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kutoa elimu ili wafugaji wengi waachane na ufugaji wa kienyeji usiokuwa na tija kwa kupunguza idadi ya mifugo yao na kugeukia mbinu za kisasa za ufugaji.

“Tunawafundisha kwa sasa kuwa kila mfugaji awe na shamba la malisho angalau ekari mbili litakalowapa uhakika wa malisho na wafuge kisasa wanaita ‘zero grazing’,” anasema Vivian Christian, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa.


Tangazo:

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW