Namna ya kuwaokoa wakulima na kilimo duni Tanzania
- Mashamba darasa yaweza kuwasaidia wengi kujifunza mbinu bora za kilimo.
- Wananchi wataka Serikali kusaidia kupunguza bei ya pembejeo.
Simiyu. Nje ya nyumba yake Agnes Mussa amezungukwa na mashamba aliyolima pamba, mahindi, mpunga na alizeti.
Katika moja ya mashamba yake, Agnes mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa, Simiyu amechanganya mazao zaidi ya mawili kwa kupanda pamba, mahindi na maharage.
Baadhi ya mazao katika mashamba haya ya Agnes ni dhaifu huku majani ya mahindi yakiwa yamechanwachanwa na wadudu.
Kutokana na kukua kwa haraka na kupandwa kwa mistari, mahindi yamefunika pamba na maharage yanayohangaika kutafuta mwanga.
“Ninalima kisasa na mazao yangu naweka na samadi,” anasema Agnes kwa Kisukuma huku akitabasamu.
Mama huyo ni miongoni mwa wakulima wengi Tanzania ambao hawalimi kwa kufuata mbinu bora za kilimo, jambo linalowapunguzia kiwango cha uzalishaji mazao na kurudisha nyuma jitihada zao za kujikwamua na umaskini kupitia kilimo.
Miongoni changamoto inayoikabili Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ni wakulima kufanya kilimo cha kienyeji bila kufuata miongozo ya kulima kisasa kama inavyoshauriwa na maofisa ugani.
Kilomita 50 kutoka katika eneo analoishi Agnes, baadhi ya wakulima wenzie wa Kijiji cha Gula wameanza kulima kisasa baada ya kufuata maelekezo ya wataalamu wa kisasa.
Upandaji mazao usiofuata ushauri wa kitalaamu ni moja ya vyanzo vinavyopunguza tija katika kilimo. Pichani ni moja ya mashamba ya alizeti katika Kijiji cha Lalago wilayani Maswa mkoani Simiyu. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Shamba la mfano laokoa wengi
Katika kijiji hiki cha cha Gula kuna shamba darasa, shukran kwa Serikali na waraghbishi ambao wanawahimiza wananchi kushiriki kujifunza kupitia mashamba hayo.
Mange Ngussa, mkazi wa Kijiji cha Gula aliyebahatika kupata mafunzo kupitia shamba darasa, anasema amelima pamba pekee yake bila kuchanganya na mazao mengine na amepanda kwa mstari akiacha nafasi kama walivyoelekezwa na mtaalamu wa kilimo wa Kata ya Lalago wilayani humo.
“Wakulima sasa wamebadilika wengi wanakatia (wanapunguza idadi ya miche ya pamba kwenye shimo moja)…kitongoji hiki kwa sehemu kubwa hawajapanda pamba kienyeji na wanapulizia dawa za wadudu kwa wakati,” anasema Ngussa.
Wakati tunatembelea shamba lake, pamba ilikuwa imeota vizuri ikiwa ina kiwango sawa na kile cha shamba darasa.
Shamba darasa la pamba lipo kilomita moja tu kutoka makao makuu ya kijiji chao.
Tofauti na mashamba ya jirani yaliyopanda pamba kienyeji na kuchanganya na mazao mengine, pamba iliyopo kwenye shamba darasa ina afya na imekua kwa haraka licha ya kupandwa miezi ya hivi karibuni kutokana na kuchelewa kwa mvua za vuli.
Soma zaidi:
- Gharama ya uhai: Ukosefu wa zanahati unavyohatarisha maisha Maswa
- Wakulima wa mahindi walivyovuna zaidi ya Sh10,000 kwa gunia Tanzania
- Kupanda bei za vyakula, CPB waja na suluhu
Shamba darasa limewasaidia wakulima wengi katika eneo hili kiasi cha kulima kwa kufuata kanuni za kisasa.
Grace Jiduma, Mraghbishi wa Kijiji cha Gula hutenga muda wake na wenzie 10 wa kamati ya maendeleo kuhamasisha wakulima kujitokeza kujifunza mbinu bora za kilimo ikiwemo namna ya kuchagua mbegu bora, upandaji kwa mistari, upaliliaji, upuliziaji viuawa wadudu, uvunaji na kutunza pamba iliyovunwa.
‘Wakulima hawataki kujifunza’
Hata hivyo, si watu wote wanafuata maelekezo ya kitaalamu na mahudhurio ya mashamba darasa katika baadhi ya vijiji Tanzania ni hafifu kama ilivyo Maswa.
Ofisa wa Kilimo wa Kata ya Lalago wilayani Maswa, Anthony Strathony anasema kuna mwitikio mdogo katika kushiriki mikutano ya kujifunza kilimo kwa sababu ya elimu duni jambo linalorudisha nyuma jitihada za kuongeza tija kwenye sekta hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi.
“Katika kitongoji chenye wakulima 200, ukiwaita washiriki madarasa ya kilimo wanakuja watu 10 tu…hii ni idadi ndogo sana ukilinganisha na idadi yao kwenye eneo husika,” anasema Strathony akibainisha hali hiyo hutokea licha ya kuwashirikisha viongozi wa vijiji na vitongoji.
Ili kuongeza tija katika kilimo, wakulima wanapaswa kutii ushauri wanaopewa na wataalamu ukiwemo wa kutumia mbegu bora, mbolea na kulima kwa wakati kwa kufuata vipimo vya kitaalamu.
Mange Ngussa mkazi wa Kijiji cha Gula wilayani Maswa akikagua pamba katika shamba lake. Ngussa ni moja ya wakulima waliolima kisasa baada ya kupata mafunzo ya shamba darasa. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Wakulima wawezeshaji waandaliwa
Katika njia ya kuwaongezea maarifa, Strathony anasema huwa wanawachukua wakulima wawili kila kijiji na kuwapatia elimu ya kilimo bora na wakulima hao ambao huitwa wakulima wawezeshaji.
“Kuna mabadiliko makubwa sana kwa miaka mitatu tangu nimefika, mfano, mwaka huu asilimia 60 ya wakulima wa kata hii wamefuata kanuni bora za kilimo hasa katika zao la pamba,” anasema.
Baadhi ya wakulima wa wilaya ya Maswa wameiambia Nukta Habari kuwa moja ya changamoto zinawakwamisha kulima kisasa ni ukosefu wa mbegu bora, kupanda kwa bei ya mbolea na kuchelewa kwa vifaa vingine vya ugani.
Neema Dengeli, mkulima wa Kijiji cha Mwamihanza anaiomba Serikali iwapunguzie bei ya pembejeo kwa sababu anadai ipo juu sana.
Wakulima walia na pembejeo
Mfano, anasema mfuko wa mbegu bora za mahindi unauzwa Sh12,000 dukani bei ambayo imedumu kwa miaka miwili sasa ila kwa wenye eneo kubwa bei hiyo ni ghali sana.
“Kuna watu hawajiwezi, hawawezi kupata hiyo fedha huwa wanalazimika watuombe wakulima wenzao mahindi yaliyotumika mwaka jana kama mbegu, unamsaidia anapanda,” anasema Dengeli.
Kilimo duni kinaathiri kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo na kunapunguza jitihada za kuwaokoa wakulima na umaskini.
Sekta ya kilimo inaajiri idadi kubwa ya Watanzania baada ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kubainisha kuwa kaya millioni 11.7 kati ya kaya milioni 12 zilizopo Tanzania zinafanya shughuli za kiuchumi.
Hii ina maana theluthi mbili au kaya mbili kati ya tatu Tanzania zinajishughulisha na kilimo.
Tangazo:
Serikali yachukua hatua kuongeza tija
Katika kukabiliana na kilimo kisichokuwa na tija kuna wakati halmashauri ya Maswa mkoani Simiyu ililazimika kuwakamata baadhi ya wakulima ambao walichanganya pamba na mazao mengine ili kuwafungulia mashtaka ila uongozi wa mkoa uliamuru waachiwe na waelimishwe zaidi.
“Tunaamini wakipata mazao mazuri baada ya kufuata mbinu bora za kilimo itawasaidia wale wanaochanganya mazao kuona mfumo huo hauleti tija
“Tunatarajia msimu ujao wa kilimo wakulima kupitia elimu tunayotoa watakuwa wameelimika na watafuata mbinu za kilimo bora,” anasema Vivian Christian, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa.
Wilaya hiyo ina lengo la kuzalisha tani milioni 1.3 za pamba kwa msimu wa kilimo wa 2021/22 na Christian anasema kwa mwenendo wa hali ya hewa wanaweza kutimiza lengo ama kufikia asilimia 85 walichopanga kuvuna.
Pamba na alizeti ni sehemu ya mazao makuu ya biashara ambayo yanachangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa wilaya hii iliyopo kanda ya ziwa.
Serikali ya Tanzania inalenga kilimo kikue kwa angalau asilimia 10 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 jambo ambalo linategemea zaidi matumizi ya mbinu bora za kilimo.
