Mikopo ya halmashauri inavyoweza kupunguza umaskini, ukosefu wa ajira Tanzania
- Baadhi ya wakazi wa Maswa mjini wajenga kiwanda cha kwanza cha mikate kupitia mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri
- Wengine walia ukosefu wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Maswa, Simiyu. Pamoja na kujikita zaidi katika ufugaji, uuzaji nguo na kilimo Anitha Mazoya anaona hajafika kiwango alichokuwa anahitaji katika maendeleo.
Mama huyo, mkazi wa Maswa mjini mkoani Simiyu amekuwa akihaha kutafuta mtaji utakaomsaidia kukuza biashara zake na shughuli za kilimo kumwezesha kuwa mfanyabiashara mkubwa.
“Kama Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) atanisikia naomba atusaidie wanawake atupatie mitaji ili tuweze kuendeleza shughuli zetu za ujasiriamali,” anasema Anitha akibainisha kuwa “mambo ni magumu.”
Anitha ni miongoni mwa Watanzania wanaopambana kusaka mitaji kupitia mikopo ya masharti nafuu Tanzania lakini kutokana na changamoto za masharti magumu ya taasisi za kifedha wamejikuta wakikosa fedha hizo.
Ukosefu wa elimu, mitaji waumiza wengi
Utafiti shirikishi uliofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza kwa kushirikiana na Shirika la Kasodefo la Maswa, ukosefu wa mitaji kwa wanawake, vijana na makundi maalumu ni miongoni mwa changamoto zinazowarudisha nyuma kimaendeleo wakazi hao wa kanda ya ziwa.
Utafiti huo uliofanyika kati ya Machi na Aprili 2021 unabainisha kuwa wakazi wengi wa wilaya hiyo wanatafuta njia bora za kuboresha maisha yao ikiwemo mikopo kwa makundi maalum na mbinu bora za kilimo na elimu ya ujasiriamali.
Ukosefu wa mikopo na riba kubwa inawakumba wakazi wengi wa wilaya ya Maswa wakiwemo wanaoishi katika vijiji vya Bushitala, Budekwa, Jija, Ilula, Gula, Lalago na Mwamihanza ambapo Nukta Habari tulibahatika kutembelea.
“Mfano, katika kijiji cha Mwandete wakazi wa eneo wanahitaji mikopo kwa wanawake na vijana wakati wakazi wa Stendi Mpya wanahitaji mitaji na elimu ya ujasiriamali,” anasema Baruani Mshale, Mkurugenzi wa Utifiti na Kujifunza wa Twaweza.
Mkazi wa Kijiji Mwamihanza wilayani humo Ndirana Jijungu sasa anasaka mkopo anunue trekta la mikono maarufu kama ‘powertiller’ baada ya ng’ombe wake wanne kati ya sita kufa kutokana na ukame wa mwishoni mwa mwaka 2021.
Ng’ombe hao walikuwa wakimsaidia shughuli za kilimo na kumuingizia kipato kwa kuwalimia wengine kwa Sh30,000 kwa ekari moja.
Wakulima na wafugaji wadogo kama Ndirana Jijungu (pichani) wanahaha kupata mikopo yenye riba nafuu ili wanunue mashine za kisasa za kilimo kama trekta la mikono ili kuongeza tija. Picha|Nuzulack Dausen.
Asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kuwaokoa?
Wakati baadhi ya wakazi hao wakisaka mitaji, Serikali imeweka utaratibu kwa halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani kutoa mikopo yenye masharti rafiki kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu iwesaidie kukuza biashara zao.
Hata hivyo, si halmashauri zote zimetekeleza kikamilifu utaratibu huo ulioanzishwa kisheria.
Mamlaka zinasema changamoto kubwa iliyojitokeza ni kuwa baadhi ya watu wanaotakiwa kupata mikopo hiyo hawataki kuunda vikundi ili waweze kukopeshwa mitaji.
Hata baadhi wanaopewa mikopo wanashindwa kutekeleza wazo lao kikamilifu kutokana na kutokuwepo usimamizi madhubuti.
Baadhi waliopewa walitokomea na kushindwa kurejesha mikopo hiyo ili wengine waweze kukopeshwa kwa dhana kuwa fedha za Serikali hazipaswi kurudishwa kama zile za taasisi binafsi za kifedha.
Kukabiliana na hali hiyo, Halmashauri ya wilaya ya Maswa imeanza utaratibu wa kuwaweka kwenye vikundi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwapatia mkopo mkubwa utakaoweza kuendesha miradi mikubwa itakayoweza kuajiri wengi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Vivian Christian anasema katika eneo la mjini wamepanga eneo maalum kwa ajili ya biashara ambalo watu watapewa viwanja na hati zitakazowasaidia kukopa kwenye taasisi za kifedha ili wapate mitaji.
Soma zaidi:
- CAG: Wahitimu 600,000 wanaingia soko la ajira bila ujuzi Tanzania
- Sekta binafsi inavyoweza kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori Tanzania
Serikali yaongeza mikopo miradi mikubwa
“Kwetu tumeacha kuwapatia watu fedha za miradi midogo midogo ya Sh1 milioni au Sh2 milioni badala yake tulinunua eneo na kuwagawia, wapo wanaofyatua tofali na wengine wamejenga kiwanda cha mikate kinachofanya kazi vizuri,” anasema Christian.
Kiwanda cha mikate cha Maswa Nutritious Bakery ndiyo kiwanda cha kwanza cha mikate katika wilaya hiyo kinachokuwa kwa kasi kilichopo eneo la viwanda Maswa mjini.
Christian anasema iliilazimu Serikali kuwakopesha kikundi cha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu Sh125 milioni kujenga jengo la kiwanda na kununua mashine za kutengenezea mikate.
“Tuliwagawia makundi yote matatu, tuliwasimamia wakajenga jengo, wakanunua mashine za mikate na sasa wanafanya vizuri na hapa wilayani mikate yote, maandazi na skonsi vinatoka kwenye kiwanda hicho,” anasema Christian.
Kiwanda hicho kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha mikate 1,000 kwa siku na malengo yao ni kuongeza uzalishaji mara dufu siku zijazo kwa mujibu wa Kulwa Makona, Mhasibu wa kiwanda hicho cha mikate.

Kiwanda chaokoa vijana na ukata wa ajira
“Hadi sasa kiwanda kimeajiri watu tisa tulioanza na mradi. Watumishi wote hapa ni vijana na tuna mpango wa kuongeza wengine siku zijazo,” anasema Makona.
Agnes Charles (24) anayefanya kazi za usafi kiwandani hapo anasema kiwanda hicho kimemsaidia kupata fedha za kujikimu na maisha kwa kuwa anapata fedha za kumpeleka mtoto wake shule na kukuza biashara ndogondogo anazozifanya.
Pamoja na kuwa kiwanda kimeanza kukua, kukatikakatika kwa umeme kumefanya waingie hasara za mara kwa mara hasa pale mikate inapokuwa kwenye mashine kiasi cha kwamba umeme ukikatika mali yote inakuwa imeharibika.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha mikate cha Maswa Nutritious Bakery cha wilayani Maswa mkoani Simiyu. Kiwanda hiki kilianzishwa kwa mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri mwaka 2021. Picha|Clifford Sangai\Nukta TV.
Kukatika kwa umeme kwachochea hasara
Kuna wakati ukikatika, Makona anasema huwa wanalazimika kutupa mikate hadi 400 kwa siku jambo lilowafanya kutafuta fedha kununua jenereta la akiba kupunguza hasara japo ongezeko la bei ya mafuta na ngano kwa sasa huenda vikazidi kuwapa changamoto zaidi.
Ili kuwapunguzia maumivu ya kurejesha mikopo ndani ya muda baada ya mradi kuanza, uongozi wa halmashauri hiyo unasema umewapa kipindi cha miaka miwili hadi miwili na nusu kama ahueni na baada ya hapo wataanza kulipa deni.
“Wenye miradi ya kijiendeleza huwa ni tatizo baadhi wanagawana fedha halafu wanashindwa kurejesha,” anasema Christian.
“Kwa hiyo hawa wenye miradi mikubwa kama kiwanda cha mikate wakishindwa tutachukua kile kiwanda maana yake fedha zetu zipo salama,” anasema.
Vijijini, Christian anasema wametumia sehemu kubwa ya fedha bila kutaja kiasi katika kuwakopesha wakulima wa pamba, alizeti na mengineyo na anatarajia baada ya msimu wa mavuno watarejesha fedha hizo.
Latest