Hasara tupu: Ukame ulivyowarudisha wafugaji kwenye umaskini Tanzania

June 7, 2022 5:40 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukame wa mwishoni mwa mwaka 2021 umeacha mamia ya wafugaji na maumivu.
  • Serikali yashauri wafugaji kuvuna sehemu ya mifugo na kuwekeza maeneo mengine.
  • Wataalamu wa mifugo washauri wafugaji kulima malisho kupunguza hasara.

Maswa, Simiyu. Mwaka 2021 unavyoanza alikuwa ana matumaini lukuki kuwa ng’ombe wake aliokuwa nao wangechangia kwa kiwango kikubwa kumuongezea kipato na kumtoa katika umaskini. 

Miezi 11 baadaye ndoto ya Ndirana Ndirana Jijungu, mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa mkoani Simiyu ilizimwa ghafla kwa kupoteza ng’ombe wanne kati ya sita baada ya kukosa malisho kutokana na ukame. 

“Maisha yangu yamerudi nyuma sana,” anasema Jijungu (43) huku akitikisa kichwa na kuonyesha ng’ombe wawili waliosailia wenye mbavu zinazoonekana sawia kutokana na kukonda.  

Ndirana, baba wa watoto wanane alitumia zaidi ya miaka mitano kujichangachanga kupata ng’ombe hao maksai. 

Kwa miaka yote hiyo aliweza kumudu kuwalisha ng’ombe wake licha ya baadhi ya miaka kuwa na ukame. 

Hata hivyo, ukame wa mwishoni wa mwaka 2021 umemfanya apoteze sehemu kubwa ya mali na kumrudisha kwenye umaskini. 

Tofauti na miaka mingine, mvua hizo zilichelewa kiasi cha kuathiri upatikanaji wa malisho na maji maeneo mengi wilayani Maswa. 

Sehemu kubwa ya wakazi wa vijiji 120 vya Maswa wanajishughulisha na kilimo na ufugaji kwa mujibu wa uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo. 

Arudi kwenye umaskini

“Hawa ng’ombe walikuwa wakilima ekari moja napata Sh30,000 na kuna msimu unalima hadi ekari 12 na kupata zaidi ya Sh350,000,” anasema Jijungu na kubainisha kuwa fedha hizo zilimsaidia sana katika kumudu gharama za maisha nyumbani. 

Kufa kwa ng’ombe hao kumemkwamisha kupalilia kisasa na sasa anaiangukia Serikali kuwapatia wafugaji mikopo ya matrekta ya mkono ili kuendeleza kilimo badala kutegemea wanyama wanaokufa kwa ukame. 

Jijungu ni sehemu ya maelfu ya wafugaji Tanzania waliopoteza mifugo yao Tanzania kutokana na ukame hasa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na kaskazini hususan mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. 

Wafugaji wakinywesha mifugo yao katika Mto Magogo katika Kijiji cha Gula, kusini mwa Wilaya ya Maswa. Wakati wa ukame walilazimika kuchimba mashimo na kuichotea mifugo yao maji ya kunywa. Picha| Nuzulack Dausen.

Ni janga la Taifa zima

Mkoani Kilimanjaro, hadi Januari 22 mwaka huu mifugo 1,257 zikiwemo ng’ombe 841 zilikuwa zimepoteza maisha. Huko wilayani Kiteto mkoani Arusha, ng’ombe zaidi ya 25,000 zimekufa kwa kukosa malisho na maji kwa mujibu wa uongozi wa halmashauri hiyo. 

 “Natoa pole kwa wote mliopitia kipindi kigumu kutokana upungufu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba, Novemba na Disemba 2021 kwa mikoa inayopata mvua vipindi viwili kutokana na uhaba wa malisho na maji,” Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dk Pindi Chana aliwaeleza wanahabari Februari 24, 2022. 

Hali ya ukame, Chana alisema imesababisha baadhi ya mifugo kudhoofika na kufa kutokana na njaa na magonjwa nyemelezi. 

Wengine wahaha kujiokoa

Baadhi wenye ujuzi na mifugo kidogo walitumia njia nyingine kujinusuru kama Felister Kulwa, Mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza aliyeamua kuuza ng’ombe wake mmoja kati ya 11 ili aweze kununua pumba ya kuwalisha wengine. 

Kiasi cha pesa alichokipata, anasema kilisaidia pia kununua dawa za kuua wadudu kuzuia magonjwa katika kipindi ambacho hata josho la jirani lilikuwa halifanyi kazi. 

Katika vijiji vilivyokuwa na uhaba mkubwa wa maji, wafugaji walilazimika kwenda maeneo ambayo mito imekauka na kuchimba mashimo marefu angalau wapate maji.

“Tulikuwa tukitoa maji kwenye mashimo hayo tunayaweka kwenye dishi ili ng’ombe waweze kunywa kwa sababu hawawezi kuingia kwenye shimo,” anasema Minza Joseph (52), mfugaji wa Kijiji cha Sulu, kusini mwa wilaya ya Maswa.


Soma zaidi:


Ukame uliotokea mwaka jana huenda ukaendelea kutokea siku zijazo kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto na kubadilisha vipindi na kiasi cha mvua zilizozoeleka kwa miaka mingi sasa.

Takwimu za hali ya mvua Tanzania zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kuwa baadhi ya vituo vya hali ya hewa Tanzania vilirekodi mwenendo wa mvua uliokuwa ukibadilika badilika kwa kasi katika kipindi cha Oktoba na Desemba 2020 ikiwemo mikoa ya Mara na Shinyanga inayopakana na Simiyu.

Mfano, kituo cha hali ya hewa cha Musoma kilirekodi mvua kiasi cha milimita 57.1 Oktoba na kupanda mara tatu Novemba kufikia milimita 162.4 kabla ya kuporomoka kwa kasi hadi milimita 47 Desemba 2020. 

Hali hiyo ni tofauti na kituo cha Zanzibar ambapo takwimu hizo zilizopo kwenye Ripoti ya Takwimu Muhimu Tanzania mwaka 2020 (Tanzania in Figures 2020) zinabainisha kuwa mvua ilikuwa kubwa kiwango cha milimita 130.2 Oktoba, milimita 271.5 (Novemba) kabla ya kushuka kidogo hadi milimita 181.7 Desemba mwaka huo.

 

Mzee Makaya Ganyata wa Kijiji cha Lalago wilayani Maswa akichota maji kati mashimo madogo katika Mto Magogo. Wakazi hawa hutaabika wakati wa kiangazi kupata maji wakieleza kuwa maji ya mradi yanayotoka bombani yana magadi. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta. 

Dawa ni kupunguza mifugo, kulima malisho

Wataalamu wa mifugo wanasema hasara ya kupoteza mifugo iliwakumba wafugaji katika maeneo mengi nchini na miongoni mwa njia za haraka za kuwaokoa na hasara hizo ni pamoja na kupunguza idadi ya mifugo na kulima malisho kwa ajili ya matumizi ya wakati wa kiangazi kikali. 

Mtaalamu wa mifugo kutoka kampuni ya Azolla Feeders jijini Dar es Salaam, Dk Mzee Torokoko anasema wafugaji wadogo wanaweza kulima aina ya malisho yanayozaliana kwa wingi maarufu kwa kimombo kama ‘hydroponic fodder’ (nyasi maalum) kisha kuyavuna na kuyahifadhi kwa ajili ya vipindi vya ukame.

Dk Torokoko anasema nyasi hizo zinaweza kulimwa kwenye angalau hata nusu ekari ama ekari moja na zaidi kutokana na uwingi wa mifugo na huchipua kwa haraka na kwa wingi kiasi cha kusaidia malisho kipindi ambacho hakina malisho kabisa. 

“Njia nyingine rahisi ni kuvuna mabua ya mahindi, kuyakatakata na kisha kuyahifadhi kwenye handaki kubwa na kuyafunika ili yasipate unyevunyevu. Kuna wafugaji wanatumia mbinu hii na wanapata chakula cha kulisha mifugo kwa hata mwaka mzima,” anasema Dk Torokoko. 

Baadhi ya mbinu kama hizi huenda zikawa mtihani kwa wafugaji wenye ng’ombe zaidi ya 1,000 ambao ukame mdogo unaweza kuangamiza mamia ya mifugo. 

Ujio wa mvua mwanzoni mwa mwaka huu angalau ulipunguza kiwango cha hasara kwa wafugaji wa Kijiji cha Mwamihanza kwa kuongeza malisho na upatikanaji wa maji. Picha| Nuzulack Dausen.

Serikali yaja na mbinu kuwanusuru wafugaji

Mamlaka nchini Tanzania zinaeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, maofisa wa Serikali katika maeneo ya wafugaji wanawaelekeza wafugaji wa kienyeji kupunguza idadi ya mifugo ili kupunguza hasara inapotokea ukame. 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Vivian Christian aliiambia Nukta Habari kuwa Serikali imekuwa ikiwasisitiza wafugaji kuwa kulima angalau ekari mbili za malisho yatakayotumika wakati wa kiangazi kwa kuwa eneo hilo hukumbwa na ukame mara kwa mara. 

 “Njia nyingine tunayowafundisha ni kwamba wasiwe na mifugo mingi wajaribu kuvuna mifugo na kuwekeza kwenye vituo ambavyo vitazalisha ikiwemo kufuga kisasa (zero grazing),” anasema Christian na kubainisha kuwa wilaya yake ina mifugo zaidi ya 400,000 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na uwiano wa watu waliopo. 

Kutokana na ukame wa mara kwa mara, Christian anasema baadhi ya wafugaji wenye mifugo mingi wamehama eneo hilo na kwenda maeneo yenye malisho mengi kama mikoa ya Rukwa na Morogoro. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV