Wizara ya Mambo ya Nje yaomba kutumia Sh1.71 trilioni 2024-25

May 16, 2024 4:47 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaongezeka kwa asilimia 32.5 kulinganisha na ile ya mwaka 2023/24.
  • Upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo si wa kuridhisha.
  • Kamati yasema ufinyu wa fedha za maendeleo utakwamisha miradi na huduma kwa wananchi.

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeliomba Bunge liidhinishe Sh1.71 trilioni kama mpango wa mapato na matumizi wa wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 wakiahidi kutekeleza vipaumbele sita ikiwemo kuboresha masuala ya haki jinai.

Hamad Masauni ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni leo Mei 15, 2024 amwaambia wabunge kuwa kati ya fedha inayoombwa Sh289.6 bilioni ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

“Kati ya fedha hizo, Sh551.5 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh 870.4 bilioni ni Mishahara, Sh 289.6 bilioni ni fedha za miradi ya maendeleo,” amesema Masauni jijini Dodoma.

Fedha za maendeleo zilizotengwa na wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 zimeongezeka kwa asilimia 175.8 kulinganisha na Sh105 bilioni zilizotengwa mwaka unaoishia mwezi Juni 2024.

Hata hivyo, mpaka Aprili 2024, wizara hiyo ilikuwa imepokea asilimia nne tu ya fedha za maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge.

Masauni amesema endapo fedha hizo zitaidhinishwa na Bunge wizara yake pamoja na taasisi zilizo chini yake zitatekeleza vipaumbele sita ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya tume ya haki jinai.

Itakumbukwa kuwa Julai, 2023 tume ya haki jinai chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mkuu Mstaafu Chande Othman iliwasilisha taarifa ya jinsi ya kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini.


Soma zaidi:Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi yapaa kwa zaidi ya asilimia 300


Vipaumbele vingine vitakavyotekelezwa na wizara hyo ni pamoja na kukamilisha, kuendeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari, kuongeza vitendea kazi vya kisasa katika kutoa huduma ikiwemo magari, pikipiki, boti na helkopta.

Masauni amesema watajikita pia katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa miji salama na mradi wa ukaguzi wa magari wa lazima, kuimarisha mifumo na matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma na kutumia nishati safi kwenye magereza na taasisi nyingine zilizopo chini ya wizara.

Ufinyu wa fedha za maendeleo waiibua kamati

Licha ya bajeti ya wizara kupaa kwa asilimia 32.5, Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeionya Serikali juu ya ufinyu wa fedha za maendeleo unaosababisha baadhi ya miradi kukwama hivyo kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Vita Kawawa, amesema hadi kufikia Aprili 2024 ni asilimia 4 ya Sh105 bilioni ya miradi ya maendeleo iliyotolewa kwa wizara kwa mwaka 2024/25 jambo lililofanya baadhi ya taasisi kukosa fedha kwa ajili ya miradi hiyo.

“Kamati ina maoni kuwa si jambo jema kwa miradi inayotekelezwa na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya wizara hii kutopewa fedha…upo umuhimu kwa Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengwa,” amesema Kawawa.

Miongoni mwa miradi iliyotakiwa kufanikishwa kwa mwaka 2023/2024 ni pamoja na ujenzi wa vituo vya polisi, ukarabati wa makazi ya Askari, vituo na ofisi. 

Kutofanikisha kwa miradi hiyo huenda kukawakosesha wananchi katika maeneo husika kupata huduma za Jeshi la Polisi kwa wakati na kuchochea uvunjifu wa amani au matendo ya kihalifu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW