Bajeti ya Wizara ya Afya yaongezeka kwa asilimia 6

May 13, 2024 2:05 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bajeti kwa mwaka 2024/25 yafikia Sh1.31 trilioni.
  • Fedha za miradi ya maendeleo zapungua kwa asilimia 72.
  • Kumarisha afya ya akili, magonjwa ya mlipuko ni miongoni mwa vipaumbele vya wizara. 

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imeliomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh1.31 trilioni  kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa imeongezeka kwa asilimia 6.1.

Bajeti hiyo ya mwaka ujao wa fedha imeongezeka kwa Sh76.5 ukilinganisha na Sh 1.23 trilioni zilizoidhinishwa mwaka 2023/24.

Waziri Ummy Mwalimu, aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni Dodoma leo (13, Mei 2024) amesema zaidi ya nusu ya Sh1.31 trilioni itakayoidhinishwa ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

“Wizara imepanga kutumia Sh 679 .5 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 52 ya bajeti tengwa. Kati ya hizo, fedha za ndani ni Sh416.2 bilioni na fedha za nje ni Sh 263.3 bilioni,” amesema Waziri Ummy.

Fedha hizo za miradi ya maendeleo zilizoombwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni pungufu kwa Sh52.79 bilioni sawa na asilimia 7.2 kulinganisha na zile zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2024.

Mwaka 2023/24 Wizara hiyo iliidhinishiwa Sh732.3 bilioni kwa ajili ya shughuli za miradi ya maendeleo.

Upungufu huo wa fedha za maendeleo unakuja wakati ambapo Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imebaini ufinyu na kutokuwasilishwa kwa wakati kwa fedha za miradi ya maendeleo kutoka serikalini jambo linalosabaisha baadhi ya miradi kukwama kwa muda mrefu.


Soma zaidi:Wabunge walia ufinyu wa bajeti Wizara ya Maji 2024-25


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stanslaus Nyongo amesema hadi kufikia Februari 2024, fedha za ndani za maendeleo zimetolewa kwa asilimia 35 na fedha za nje kwa asilimia 30 tu ikiwa imebaki miezi minne kabla ya mwaka wa fedha 2023/2024 kuisha.

“Hali hii itasababisha miradi kutokukamilika ndani ya muda uliopangwa na kutofikia matarajio ya wananchi ya kupata huduma bora zilizokusudiwa…ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa fedha zote zinazoidhinishwa kwa bunge zinatolewa kabla ya mwaka wa fedha kuisha,” amesema Nyongo.

Mbali na fedha za maendeleo, Wizara ya Afya pia inatarajia kutumia Sh632.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 48 na Sh147.3 bilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Vipaumbele kwa mwaka 2024/25

Waziri Ummy amewaambia wabunge kuwa katika mwaka 2024/25 wizara yake itatakeleza vipaumbele 10 kiwemo kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma za afya.

“…Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa, kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa, kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini na kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga,” amesema Waziri Ummy.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalamu katika sekta ya afya kwa fani za kati,ubingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa naubingwa bobezi nchini.

Pia Wizara ya Afya itaendeleza na kusimamia afua za tiba asili na tiba mbadala, kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko pamoja na  kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.

Enable Notifications OK No thanks