Zaidi ya robo tatu bajeti Wizara Mambo ya Ndani ni matumizi ya kawaida
- Asilimia 85 ya bajeti kutumika kwa mishahara na matumizi mengineyo.
- Bajeti ya maendeleo yapungua, yatengewa asilimia nane ya bajeti nzima.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni ameomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh1.2 trilioni kwa ajili ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 huku zaidi ya robo tatu ya bajeti ya wizara hiyo ikielekezwa kwenye mishahara na matumizi mengineyo.
Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ni miongoni mwa wizara nyeti na muhimu ambayo inasimamia taasisi zinazohusika katika kuimarisha amani, utulivu, pamoja na utii wa sheria.
Miongoni mwa taasisi zinazosimamiwa na wizara hiyo ni pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Uhamiaji ambazo zina wajibu wa kulinda maisha na mali, kuwezesha na kuthibiti utokaji na uingiaji nchini kwa raia na wageni, kuwarekebisha wafungwa na kutoa huduma kwa wakimbizi waliopo nchini
Masauni aliyekuwa akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24 leo Mei 29, 2023 amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha hizo Sh 678.6 sawa na asilimia 52 ya bajeti ni kwa ajili ya mishahara.
“Sh510.1 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh105 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Masauni jijini Dodoma.
Bajeti ya matumizi ya kawaida ambayo inajumuisha mishahara na matumizi mengineyo ni Sh1.18 trilioni sawa na asilimia 85 ya bajeti yote ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2023/24.
Soma zaidi
-
Yafahamu matunda yanayoweza kutibu na kukupa kinga ya maradhi
-
Namna ya kuepuka kupokea barua pepe usizozihitaji
Pamoja na bajeti inayoombwa kuongezeka kwa Sh81 bilioni, fedha za miradi ya maendeleo ambazo ni asilimia 8 ya bajeti nzima zimepungua kutoka Sh140 bilioni mwaka uliopita hadi Sh105 bilioni.
Miongoni mwa miradi ambayo hutekelezwa chini ya wizara hii ni pamoja na ujenzi wa nyumba za makazi za watumishi wake, ujenzi wa ofisi za taasisi zilizo chini ya wizara kama vituo vya polisi, ofisi za uhamiaji na magereza pamoja na ujenzi na ukarabati wa vyuo vya mafunzo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Vita Kawawa, amebainisha kuwa kamati hiyo imebaini utoaji wa fedha za maendeleo ili kufanikisha utekelezaji wake kwa bajeti iliyopita hauridhishi kwa kuwa mafungu yote ya miradi ya maendeleo yamepata fedha chini ya asilimia 50.
Pamoja na baadhi ya miradi kupata fedha chini ya asilimia 50 baadhi haikupata kabisa licha ya Wizara kukamilisha taratibu zote za maombi ya fedha jambo lililokwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Kawawa ametoa rai kwa Serikali kufuata matakwa ya Bunge kwani wao ni wawakilishi wa wananchi, na ili miradi hiyo iwe na tija inapaswa kutekelezwa kwa wakati.
Vipaumbele vya wizara 2023/24
Masauni amebainisha kuwa kwa mwaka ujao wa fedha Wizara hiyo inakusudia kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama, kuendeleza ushirikishwaji jamii, kukamilisha miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha matumizi ya Tehama katika kutimiza majukumu.
Vipaumbele vingine ni kuboresha mazingira ya kazi pamoja na makazi ya watumishi wa Wizara hiyo, kuimarisha vitendea kazi, kuimarisha sheria za usalama barabarani pamoja na kufanyia mapitio sheria nyingine nane.
Latest