Bajeti ya Wizara ya Madini yapaa kwa miaka mitano mfululizo
- Yafikia Sh213.98 bilioni kutoka Sh163 bilioni mwaka 2023/2024
- Miradi ya maendeleo yasuasua licha ya kupaa kwa bejeti.
Dar es Salaam. Wizara ya Madini imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh213.98 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikiongezeka kwa mara ya tano mfululizo tangu mwaka 2020/21.
Bajeti hiyo itakayoanza kutumika Julai 1, 2024 imeongezeka kutoka Sh163 bilioni ya mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la Sh68.9.bilioni.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa mara tano mfululizo tangu mwaka 2020/21 Serikali ilipoidhinsha Sh62.7 bilioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wizara hiyo.
Waziri wa Wizara ya Madini Antony Mavunde, aliyekuwa akiwasilisha bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 30, 2024 amesema zaidi ya nusu ya fedha hizo ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
“Sh140.66 bilioni sawa na asilimia 60.6 ya bajeti yote ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh91.32 bilioni sawa na asilimia 39.3 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida,” amesema Waziri Mavunde.
Soma zaidi:Wizara ya Katiba na Sheria yaomba kuidhinishiwa Sh441.2 bilioni mwaka 2024-25
Kati ya fedha hizo Sh24.87 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Sh66.44 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ya wizara na taasisi zilizo chini yake.
Bajeti hiyo ya mwaka ujao wa 2024/25 ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka mitano iliyopita.
Mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilipitisha Sh68.54 bilioni kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kiasi kilichoongezeka kwa mwaka 2022/2023 hadi Sh83.44 bilioni iliyoongezeka tena mwaka 2023/2024-25.
Kutokana na kuongezeka kwa bajeti hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti hiyo na kuitaka Wizara ya Madini kuongeza uzalishaji utakaokuza pato la Taifa.
“Kamati inapongeza hatua hiyo ya Serikali kuongeza bajeti ya wizara hii kwani itakuwa ni chachu ya kuboresha utendaji na kuifanya sekta ya madini iendelele kufanya vizuri na kuongeza mchango kwenye pato la Taifa.
Aidha, wizara itumie nyongeza hiyo ya bajeti kuongeza ufanisi wa utendaji kwa watendaji wake,” amesema Kilumbe Ng’enda Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Miradi ya maendeleo yasuasua
Licha ya bajeti ya wizara hiyo kupaa kwa miaka mitano mfululizo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imebaini kusuasua kwa miradi kunakosababishia Serikali hasara.
Mathalan mwaka 2022/2023 uchambuzi wa kamati huo ulionesha kusuasua kwa miradi ya maendeleo kulikosababishwa na ufinyu wa bajeti.
Kati ya Sh96.82 bilioni za maendeleo zilizotengwa katika mwaka huo wa fedha ni asilimia 20.9 tu ya fedha zilizoidhinishwa.
Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kamati hiyo ililiamba bunge kuwa kusuasua kwa miradi hiyo kulitokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya usanifu na wakandarasi katika miradi hiyo.
“Ni vyema usanifu na tathmini ya kina ifanyike kwa kiwango cha kuridhisha kabla ya kutekeleza miradi hii ili kuepuka ongezeko la gharama na kuwezesha miradikukamilka kwa wakati uliopangwa,” amesema Ng’enda.
Latest