Wanafunzi zaidi ya 3,000 wapata mikopo HESLB awamu ya tatu
- Ni wanafunzi 3,544 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh11.1 bilioni.
- Idadi hiyo inakamilisha orodha ya wanafunzi 53,364wa mwaka wa kwanza ambao wamepangiwa mikopo hadi sasa.
- HESL yafungua dirisha kwa ambao hawajaridhika kukata rufaa.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya tatu ya wanafunzi 3,544 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh11.1 bilioni kwa mwaka wa masomo 2020/21 ulioanza mwishoni mwa mwezi Novemba.
“Kufuatia kutolewa kwa awamu hii ya tatu, hadi sasa jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ni 53,364 yenye thamani ya Sh173.3 bilioni,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa yake iliyotolewa Jumanne Desemba 1, 2020, Jijini Dar es Salaam.
Amesema wanafunzi hao wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kutembelea katika akaunti zao za SIPA (Student’s Individual Permanent Account) walizotumia kuomba mkopo na watapata taarifa za kina kuhusu mkopo waliyopata.
Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati wakiendelea na masomo ya elimu ya juu.
Aidha, Badru amesema wanafunzi 69,625 wanaoendelea na masomo wamepangiwa Sh247.5 bilioni baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka 2019/20.
Soma zaidi:
- Waombaji 10,452 Heslb wapewa siku nne kurekebisha kasoro
- Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu 2019-2020
- TCU yaanika sifa za wanafunzi kujiunga vyuo vikuu Tanzania
Baada ya kutangazwa kwa awamu ya tatu za upangaji mikopo, hatua inayofuata ni kufunguliwa kwa dirisha la rufaa kwa siku saba kuanzia Jumatano, Desemba 2, 2020 ili kuwawezesha waombaji ambao hawajapangiwa mikopo au hawajaridhika na viwango walivyopangiwa kuambatanisha nyaraka za ziada kuthibitisha uhitaji wao.
Kwa mujibu wa Badru amesema katika kipindi cha rufaa, wanafunzi watahitajika kutembelea mfumo wa olas.heslb.go.tz, kufuata maelekezo na kuwasilisha rufaa zao kutoka popote walipo bila malipo yoyote.
“HESLB inatoa wito kwa wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na ni wahitaji, kutumia muda wa siku saba za rufaa kuwasilisha nyaraka sahihi ili hatimaye wapangiwe mikopo ya kuwawezesha kulipia gharama za masomo,” amesema Badru.
Katika mwaka 2020/21, Serikali imetenga Sh464 bilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.
Latest
