Heslb kutoa majina waliopata mikopo awamu ya pili Oktoba 21

October 18, 2021 8:48 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Waliopata awamu ya kwanza ni 37,731.
  • Majina awamu ya pili kutolewa ndani ya siku tatu.
  • Wanafunzi 70,000 wa mwaka kwanza kupata mikopo.

Dar es Salaam. Baada ya wanafunzi 37,731 wa mwaka wa kwanza kupata mikopo elimu ya juu kwa mwaka 2021/22, Serikali inatarajia kutoa awamu ya pili ya orodha ya majina mengine Oktoba 21 mwaka huu. 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza idadi ya wanafunzi hao Oktoba 17, 2021 ambapo mikopo yao thamani yao in Sh99.9 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao (37,731), wanaume ni 23,379 sawa na asilimia 62.

Badru amesema kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni…lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru.

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya awamu ya pili, Badru amesema imepangwa kutolewa Alhamisi, Oktoba 21, 2021 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja… tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili katika siku mbili zijazo,” amesema Badru.

Aidha, Bodi imewataka waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Serikali imetenga Sh570 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka. 

Hadi kufikia Septemba 30, HESLB ilikuwa imepokea maombi 88,688 na huenda asilimia 12 ya walioomba wanaweza wasipate mikopo hiyo kwa sababu ya bajeti iliyopo kutokidhi mahitaji ya waombaji wote.

Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati akisaka elimu hiyo ya juu. 

Wangapi watatoboa awamu ya pili ya HESLB? Usikose kufuatilia habari za HESLB katika tovuti ya www.nukta.co.tz na mitandao yake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW