Waombaji 10,452 Heslb wapewa siku nne kurekebisha kasoro

TULINAGWE MALOPA 0838Hrs   Oktoba 01, 2019 Habari
  • Ni waombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 ambao fomu zao zina upungufu.
  • Bodi imetoa siku nne kwa ajili ya kufanya marekebisho.
  • Oktoba 6, 2019 itatoa majina ya wanufaika wa mikopo mwaka 2019/20.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) imetoa orodha ya waombaji 10,452 wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 ambao fomu zao zina upungufu ili wafanye marekebisho kwa siku nne.

Taarifa ya Heslb iliyotolewa jumapili (Septemba 29, 2019) imeeleza kuwa marekebisho hayo yanatakiwa kufanyika kuanzia jana Septemba 30 hadi Oktoba 3, 2019 ili iwe kukamilisha mchako wa uchambuzi wa wanafunzi wanaopaswa kupata mikopo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu. 

“Hatua ya HESLB inafuatia kukamilika kwa uhakiki wa maombi ya mikopo ambapo imebainika baadhi ya fomu za maombi ya mikopo zina upungufu unaozuia kuendelea na hatua ya kupangiwa mikopo,” inaeleza taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano cha Heslb. 


Zinazohusiana:


Upungufu huo ni pamoja na kukosa nyaraka ama viambatanisho vilivyothibitishwa na mamlaka husika na saini za waombaji na wadhamini wao.

Baadhi ya waombaji hawajaweka nyaraka zao za vyeti vya kuzaliwa, hawajapata muhuri kutoka kwa mwanasheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na maombi yao kutokuwekewa sahihi.

Orodha hiyo ni ya wanafunzi wanaokwenda kusoma masomo ya Shahada ya kwanza. 

HESLB imejipanga kuhakikisha kazi yote ya uhakiki na uchambuzi wa maombi yote ya mikopo inakamilika ifikapo Oktoba 6, 2019 ili wanafunzi wahitaji wapangiwe mikopo, wapate taarifa na fedha za mikopo zitumwe vyuoni kabla ya vyuo kufunguliwa katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2019.


Related Post