Wagonjwa wa Corona wazidi kuongezeka Tanzania
- Wizara ya Afya yathibitisha wagonjwa wengine wawili wa Corona leo na kufanya jumla ya wagonjwa kuwa sita mpaka sasa.
- Wagonjwa wote wawili ni Watanzania walioingia nchini kwa nyakati tofauti.
- Serikali yawataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kuongezeka kwa visa vingine viwili vya wagonjwa wa Corona nchini Tanzania na kufanya jumla ya wagonjwa kufikia sita.
Taarifa iliyotolewa na Waziri huyo leo (Machi19, 2020), hadi sasa Tanzania ina wagonjwa sita ambapo watano wanatokea Tanzania bara na mmoja anatokea Zanzibar kama ilivyoripotiwa jana Machi 17, 2020.
“Wagonjwa wapya wawili wamethibitika jijini Dar es salaam kuwa na Covid-19, na hivyo kufanya jumla ya wagonjwa waliothibitika nchini mpaka sasa kufikia 06 (sita), ambapo mmoja ni yule wa Zanzibar aliyetolewa taarifa jana,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, Ummy amesema wagonjwa wote wawili ni Watanzania, wanaume wenye umri wa miaka 40 kila mmoja.
Mmoja alisafiri nchi za uswisi, Denmark na Ufaransa kati ya Machi 5, 2020 hadi Machi 13 na kurejea nchini Machi 14.
Mwingine alisafiri kwenda Afrika Kusini kati ya Machi14, 2020 hadi Machi 16 na kurudi nchini usiku wa Machi 17.
Wagonjwa hao wametengwa na juhudi za kuendelea kuwafuatilia watu waliokuwa nao karibu zinaendelea.
“Wahusika wote wametengwa (isolation) na hali zao zinaendelea vizuri. Juhudi za kufuatilia watu waliokuwa karibu na wagonjwa waliothibitika kuwa na COVID-19 (yaani “contacts”) zinaendelea,” amesema Ummy.
Aidha, amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya watu 46 wanafuatiliwa jijini Arusha, na watu 66 wanafuatiliwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilithibitisha mgonjwa wa kwanza wa virusi hivyo Machi 16, na visa vitatu viliongezeka jana huku kimoja kikiripotiwa Zanzibar.
Zinazohusiana
Mpaka sasa ni nchi tatu za Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Rwanda ndiyo zimethibitisha kuwa na wagonjwa wa virusi vya Corona, ambapo jana Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema barani Afrika kuna kesi 233 za watu walioambukizwa.
Wananchi wameshauriwa kuwa watulivu na kuchukua tahadhari zinazotolewa na mamlaka za afya nchini ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa mdomo, pua na macho.
Pia kutumia tishu wakati wa kukohoa na kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima.