UDSM yaingia 10 bora wahitimu kuajirika Afrika, yaiweka Tanzania kwenye ramani ya vyuo duniani
- Yashika nafasi ya tatu Afrika Mashariki, yaiweka Tanzania nafasi ya 131 kwenye ramani ya vyuo vikuu duniani.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeandika historia mpya baada ya kuorodheshwa miongoni mwa vyuo 10 bora barani Afrika vinavyozalisha wahitimu wenye uwezo mkubwa wa kuajirika, huku kikishika nafasi ya 131 duniani katika kipengele cha matokeo ya wahitimu katika soko la ajira.
Kwa mujibu wa Viwango vya Kimataifa vya Vyuo Vikuu (QS) vya mwaka 2027, UDSM imepata alama 85.3 katika kipengele cha ‘Employment Outcomes’, kinachopima uwezo wa chuo kuwaandaa wanafunzi kwa ajira, pamoja na mchango ambao wahitimu wake wanautoa katika uchumi, sekta binafsi, serikali na taasisi mbalimbali duniani.
Mafanikio hayo yametokana na tathmini iliyohusisha zaidi ya vyuo vikuu 8,800 duniani, huku ni vyuo 1,504 pekee vikifanikiwa kuingia kwenye orodha rasmi ya viwango hivyo.
QS World University Rankings ni mfumo wa kimataifa wa kuorodhesha vyuo vikuu duniani unaotolewa na kampuni ya Quacquarelli Symonds (QS), kutokea nchini Uingereza.
Mfumo huo hupima utendaji wa vyuo kwa kutumia vigezo mbalimbali, ikiwemo sifa za kitaaluma, maoni ya waajiri, matokeo ya wahitimu katika soko la ajira, ubora wa utafiti na ushirikiano wa kimataifa.
Tofauti na viwango vinavyojikita zaidi katika tafiti au machapisho ya kitaaluma, kipengele cha uwezo wa kuajirika huangalia kama elimu inayotolewa chuoni inatafsirika kuwa ujuzi unaohitajika na waajiri.
Hii inamaanisha kuwa kwa UDSM kuingia kwenye orodha kunaiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazotambulika kimataifa kwa ubora wa elimu ya juu na uwezo wa kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa.

Namba 3 Afrika Mashariki
Mbali na mafanikio ya kuajirika kwa wahitimu, UDSM pia imeingia kwa mara ya kwanza katika orodha kuu ya Viwango vya Kimataifa vya Vyuo Vikuu (QS) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970 ikiwa katika kundi la nafasi kati ya 1201 hadi 1400 duniani.
Kwa upande wa Afrika, UDSM imeingia kwenye orodha ya vyuo 10 bora vinavyozalisha wahitimu wenye uwezo mkubwa wa kuajirika ikishika nafasi miongoni mwa vyuo vitatu bora Afrika Mashariki, hatua inayoiweka mbele ya mamia ya vyuo vikuu vilivyozoeleka kimataifa.
‘Ni mafanikio ya elimu ya juu Tanzania’
Mafanikio ya UDSM yanakuja wakati ambapo Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ajira kwa vijana, hali inayofanya ubora wa wahitimu na uwezo wao wa kuingia kwenye soko la ajira kuwa moja ya vigezo vinavyozidi kupewa uzito katika kupima ubora wa taasisi za elimu ya juu.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo idara ya tafiti, Profesa Nelson Boniface, amesema nafasi hiyo ni uthibitisho wa ubora wa elimu inayotolewa na UDSM pamoja na uwezo wa wahitimu wake kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Profesa Boniface ameiambia Nukta Habari kuwa mafanikio hayo hayaishii kuwa heshima kwa chuo pekee, bali yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi kwenye ramani ya elimu ya juu duniani na kuonyesha uwezo wa nchi kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu na ushindani wa kimataifa.
“Haya si mafanikio ya UDSM pekee, bali ni mafanikio ya Tanzania. Yanaiwezesha nchi yetu kutambulika zaidi katika sekta ya elimu ya juu duniani na yanathibitisha kuwa tuna uwezo wa kuzalisha wahitimu wanaoweza kushindana na kufanya vizuri popote duniani,” amesema Profesa Boniface.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa kupitia elimu bora, utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu.
