Wagonjwa wa Corona wafikia watatu Tanzania

Mwandishi Wetu 0145Hrs   Machi 18, 2020 NuktaFakti
  • Mgonjwa mmoja amekutwa Zanzibar na mwingine jijini Dar es Salaam na kufanya idadi ya wagonjwa kufikia watatu. 
  • Wagonjwa hao wote ni raia wa kigeni ambao wanaendelea kupata matibabu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa wawili wa virusi vya corona Tanzania ambapo mmoja amekutwa Zanzibar na mwingine jijini Dar es Salaam na kufanya idadi ya wagonjwa kufikia watatu. 

Kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona nchini kilithibitishwa Machi 16, 2020 ambapo mgonjwa huyo alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili Tanzania jana Jumapili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Ubelgiji.


Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Machi 18, 2020)  kupitia kituo cha televisheni cha Taifa cha TBC 1, amesema wagonjwa hao wote ni raia wa kigeni ambao wanaendelea kupata matibabu.  

“Tayari wagonjwa wawili wamepatikana wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo, mgonjwa mmoja anatoka Zanzibar ambaye sampuli zake zimeletwa maabara kuu. Yeye ni Mjerumani wa miaka 24 amepata maambukizi kwahiyo sasa yuko kwenye uangalizi.

“Lakini pia hapa jijini Dar es Salaam tuna Mmarekani mwenye miaka 21 naye pia amegulika kuna na virusi vya Corona,” amesema Majaliwa.

Tanzania inakuwa nchi ya tatu ya Afrika Mashariki baada ya Kenya na Rwanda kuthibitisha kuwa na wagonjwa wa virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi duniani.

Aidha, amesitisha masomo kwa vyuo vikuu na vya kati nchini Tanzania kuanzia leo Machi 18, 2020 na kuwataka wanafunzi waliofunga kutorudi vyuoni.


Zinazohusiana


Hata hivyo, amesema shughuli zingine zikiwemo za masoko, maduka, usafiri zitaendelea kama kawaida na kuwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari muhimu ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, na kunawa mikono.

“Huduma za usafirishaji zitaendelea lakini wasafirishaji waendelee kuwaelimisha abiria na hakuna umuhimu wa kuwajaza na wabaki kwenye viti na tuendelee kutoa huduma wakati wote ili Watanzania waweze kupata huduma zote; usafiri, masoko na upatikanaji wa chakula,” amesema Majaliwa.

Takwimu za Shirika za Afya Ulimwenguni (WHO) za hadi jana (Machi 17, 2020) zinaeleza kuwa watu 179,112 wameambukizwa ugonjwa huo duniani huku waliofariki wakifikia 7,426. 

Tahadhari za kuchukua ni pamoja na kuosha mikono, kutumia tishu wakati wa kukohoa na kutoshika mdomo, pua na macho.


Related Post