Uelewa finyu, dharau dhidi ya Corona zinavyohatarisha maisha

July 23, 2021 9:44 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi wanauona ugonjwa kama wa kawaida na hawachukuii tahadhari.
  • Wengine wamesema wataendelea kuchukua tahadhari.
  • Serikali yahimiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalam wa afya huku maambukizi yakiongezeka. 

Mwanza. Licha ya idadi ya wagonjwa wa corona (Uviko-19) kuendelea kuongezeka Tanzania, baadhi ya watu hawaonekani kujali kabisa miongozo ya afya ya kujikinga wasidhurike nao.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wakazi wake wana maoni mseto juu ya tahadhari za kujikinga huku wengi wakionekana kupuuzia maradhi hayo kiasi cha kuongeza hatari ya kuenea kwa maambukizi ya Uviko-19.

Kasi ya maambukizi ya Uviko-19 nchini Tanzania imezidi kuongezeka na hadi Julai 21 watu 682 walikuwa wanaugua ugonjwa huo kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima kutoka watu 408 mapema mwezi huu.  

Tahadhari ambazo zimekuwa zikisisitizwa na wataalam wa afya ni kunawa mikono kwa maji tiririka na sababu, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. Hata hivyo, si wote wanafuata miongozo hiyo.

Wapo wanaokiri kwamba ugonjwa huo upo kutokana na kuongezeka wagonjwa na wengine wanachukulia ugonjwa huo kama magonjwa mengine na kwamba wanaohimiza tahadhari hizo “wanataka kujiimarisha kisiasa” madai yasiyokuwa na ukweli. 

Hadi sasa wanasiasa wote wa vyama vya upinzani na Chama cha Mapinduzi (CCM) bila kujali itikadi wamekuwa wakihimiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 wakiwemo Mwenyekiti wa chama tawala Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyikiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 10, 2021 katika kijiji cha Buyagu wilayani Sengerema, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara viongozi waliohudhuria mkutano huo walionekana kuvaa barakoa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo na kukaa mita moja kama maelekezo ya afya yanavyotaka.

Hata hivyo, kundi kubwa la watu waliojitokeza kwenye mkutano huo wakiwemo wazee walikuwa hawajachukua tahadhari yoyote ya kujikinga. Wazee ni moja ya makundi yaliyo hatarini kupata maambukizi ya Uviko-19. 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilunda wilayani Sengerema wakati alipofanya ziara kwenye eneo la kivuko. Picha|Mariam John.

“Ni ugonjwa wa kisiasa ingawa Serikali inatia msisitizo lakini hauko kama vile tunavyoona sisi,” amesema Shikaho Maghembe mkazi wa kijiji cha Usagara jijini Mwanza bila ya kujua kuwa unaweza kumuathiri muda wowote.

Uelewa mdogo juu ya ukubwa wa madhara ya Uviko-19 umefanya watu wengi katika eneo hili wauone ugonjwa huo kama jambo dogo ikizingatiwa kuwa mtandaoni kumekuwa taarifa luluki za upotoshaji.

Athanas Masanja mkazi wa Kijiji cha Buyagu yeye anasema anuona ugonjwa huo kama kawaida hivyo hauoni sababu ya kuogopa ndiyo maana wakati mkutano huo ukiendelea hakuchukua tahadhari.

“Mimi naona ni ugonjwa wa kawaida tu na watu wanaendelea na shughuli zao labda mtu akiugua ni mafua tu anameza “panadol” (dawa ya kutuliza maumivu) na kuendelea na shughuli zake,” amesema Masanja.

Tofauti na anavyosema Masanja, hadi sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) halijathibitisha uwepo wa dawa yeyote inayoweza kutibu Uviko-19 zaidi kuchukua tahadhari za kiafya kujikinga na kupata chanjo.

Tabia ya watu katika baadhi ya maeneo ya Tanzania kupuuza miongozo ya kujikinga na maradhi ya Uviko-19, kwa mujibu wa Dk Gwajima, imefanya maambukizi ya ugonjwa huo kuongezeka kwa kasi ndani ya muda mfupi.

Tanzania kama mataifa mengine ulimwenguni inakabiliwa na wimbo la tatu la Uviko-19 ambalo wataalamu wa afya wanasema lina nguvu kubwa kuliko mawimbi mengine yaliyopita.

Mfano, Rais Samia aliwaeleza wahariri jijini Dar es Salaam Juni 28, 2021 kuwa hadi Juni 26 kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 100 ambao kati yao 70 walikuwa wakipata tiba ya oksjeni na waliosalia walikuwa wakipata matibabu ya kawaida.

Matibabu ya oksijeni ni tiba ya kiwango cha juu anachohitaji mgonjwa wa Uviko-19 ili kuokoa maisha yake.

Hata wakati baadhi ya wakazi wa Sengerema wakikosa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, wengine wamesema wataendelea kuchukua tahadhari kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya.

Mkazi wa kijiji cha Ilunda wilayani humo, Martha Yakubu amesema ataendelea kuchukua tahadhari kuhakikisha anajikinga na ugonjwa huo.

“Wahenga  walisema kabla msiba haujakupata haujui uchungu wake, tunatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepukana na dhahama hii ambayo watalaam wanatueleza,” amesema Martha.

Katika kata mbili ambazo waziri huyo alitembelea kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo wengi  hawana habari ya kuchukua tahadhari, hata vifaa vya kunawia mikono na kupaka vitakasa mikono havipo.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kuhimiza wananchi kuchukua tahadhari kwa sababu ugonjwa huo uko nchini.

Naibu waziri Waitara anawataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuwa wimbi la tatu la ugonjwa huo halichagui rika la mtu.

Akitoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kwenye vijiji hivyo vya Buyagu na Ilunda, Waitara anasema mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huo kutokana na mwingiliano wa watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Na mbaya zaidi vimelea vya ugonjwa huo havionekani kwa macho, hivyo kama mtu amevaa barakoa na kupaka vitasa mikono anakuwa na asilimia chache za kuambukizwa ugonjwa huo.

“Wazazi wawahamasishe watoto wao wawapo shuleni kuhakikisha wananawa mikono na sabuni mara kwa mara ili kujikinga na ugonjwa huo,” anasema kiongozi huyo.

Katika jamii ambayo baadhi wana mawazo hasi juu ya madhara ya Uviko-19 hasa kwa kuusisha ugonjwa huu na siasa, wanasiasa wana kazi kubwa ya kufanya katika kutoa elimu mtaani.

Miongoni mwa kazi za awali ni kubadilisha mtazamo wanaouchukulia ugonjwa huu ili kupunguza vifo visivyo na sababu.

Mbunge wa Jimbo la Sengerema Hamis Tabasamu anasema ili kutekeleza maendeleo katika maeneo yao lazima wananchi wawe na afya njema.

Kufanikisha afya hiyo, Tabasamu anawataka wananchi hao kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19.

Nyongeza na Nuzulack Dausen. 

Makala hii ni mfululizo wa ripoti maalum za Nukta Habari katika kukabiliana na Uviko-19 kwa ushirika wa Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MFUMUKO WA BEI kuendelea kuwa mdogo licha ya gharama za mafuta

MFUMUKO WA BEI kuendelea kuwa mdogo licha ya gharama za mafuta

Nukta TV

Hali ya uchumi Tanzania: Makadirio ya ukuaji wa uchumi Bara 6%, Zanzibar 6.6%

Hali ya uchumi Tanzania: Makadirio ya ukuaji wa uchumi Bara 6%, Zanzibar 6.6%

Nukta TV

BoT: Yatangaza ongezeko la riba ya Benki kuu hadi 6.25%

BoT: Yatangaza ongezeko la riba ya Benki kuu hadi 6.25%

Nukta TV