Chanjo ya virusi vya Corona yaanza kufanyiwa majaribio

Rodgers George 0306Hrs   Machi 19, 2020 Habari
  • Chanjo hiyo imetolewa na Shirika la Afya Duniani likishirikiana na wataalamu mbalimbali.
  • Nchi 10 zimekubali kushiriki majaribio hayo ikiwemo Afrika Kusini.
  • Wanasayansi wanaangalia uwezekano wa kutafuta dawa kutibu wagonjwa wa ugonjwa huo. 

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuanza kwa majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona sambamba na utafiti wa dawa zinazofaa kutibu ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani. 

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dk Tedros Ghebreyesus akiongea na wanahabari jana (Machi 18, 2020) kwenye makao makuu ya shirika hilo yakiyopo nchini Usisi amesema hatua hiyo ni ya mafanikio huku akiwapongeza watafiti walioungana kutathmini majaribio ya chanjo hizo.

“Haya ni mafanikio makubwa, tunawapongeza watafiti kote duniani ambao wamekuja pamoja ili kutathimini majaribio ya tiba. Majaribio madogo madogo ya njia mbalimbali yanaweza yasitupe ushahidi wa kutosha , tunahitaji tiba yoyote ambayo itatusaidia kuokoa maisha.” amesema Dk Ghebreyesus.

Majaribio hayo yanakuja baada ya kutimia siku 60 za nchi ya China kuwasilisha sampuli za virusi vya Corona kwa shirika hilo ambapo watafiti mbalimbali walikuwa wakivifanyia kazi kugundua chanjo dhidi ya virusi hivyo.


Zinazohusiana


Aidha, Dk Ghebreyesus amesema WHO na washirika wake wataendelea na utafiti uliopewa jina la “Majaribio ya mshikamano”  utakaofanyika kwenye baadhi ya nchi zilizokubaliana na utafiti huo zikiwemo Afrika Kusini, Hispania, Uswisi na Thailand ambamo dawa hizo zitajaribiwa ili kuona ufanisi wake.

Nchi nyingine zilizokubaliana na majaribio hayo ni pamoja na Argentina, Bahrain, Canada, Ufaransa, Iran na Norway huku Ghebreyesus akiamini kuwa nchi zingine zitajiunga.

“Naendelea kutiwa moyo na jinsi nchi nyingi zinavyoonyesha mshikamano kote duniani,“ amesema Dk Tedros na kuongeza kwa mfuko  wa kupambana na virusi hivyo hadi sasa umekusanya zaidi ya Sh99.09 bilioni zilizochangwa na zaidi ya watu 173,000 siku chache tu tangu uzinduliwe.

Amesisitiza kwamba virusi hivyo ni tishio kubwa lakini pia ni fursa ya kuja pamoja kukabiliana na adui huyo mkubwa dhidi ya ubinadamu.

Hadi kufikia jana, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na WHO, watu 7,807 duniani wamefariki kutokana na virusi hivyo huku watu 191,127 wakiambukizwa. 

Bara la Afrika limeripoti vifo vinne kati ya watu 233 waliogundulika kupata maambukizi ya virusi hivyo.


Related Post