Vikao vya kamati za Bunge kuanza Oktoba 21, ripoti za CAG kujadiliwa
- Vikao hivyo vitafanyika kati ya Oktoba 21 hadi Novemba 1 mwaka huu kabla ya mkutano wa 17 wa Bunge utakaoanza Novemba 5.
- Katika vikao hivyo vitashughulikia hoja mbalimbali za ukaguzi kama zilivyoripotiwa katika taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2018.
- Vikao vya kamati ya masuala ya Ukimwi vilianza tangu Oktoba 15 na vinakamilika leo.
Dar es Salaam. Vikao vya kamati za Bunge kwa ajili ya mkutano wa 17 wa Bunge la Tanzania vinatarajiwa kuanza Jumatatu ya Oktoba 21, 2019 huku miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa na vikao hivyo ni kushughulikia hoja mbalimbali zilizopo katika taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2018.
Vikao hivyo vitafanyika kati ya Oktoba 21 hadi Novemba 1 mwaka huu kabla ya mkutano wa 17 wa Bunge utakaoanza Novemba 5.
Hata hivyo, vikao vya kamati ya masuala ya Ukimwi vilianza tangu Oktoba 15 na vinakamilika leo.
“Vikao vya kamati zote vitafanyika katika kumbi za ofisi ya Bunge Dodoma na shughuli zote za kamati hizo, zimepangwa kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari, 2016,” inasomeka sehemu ya ratiba ya vikao hivyo iliyotolewa jana (Oktoba 18, 2019) na Idara ya Kamati za Bunge.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zitashughulikia hoja mbalimbali za ukaguzi kama zilivyoripotiwa katika taarifa ya hesabu zilizokaguliwa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2018.
Kushughulikiwa kwa mapendekezo aliyoyatoa CAG, Profesa Musa Assad katika ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka fedha wa 2017/2018 huenda kukaibua mjadala, ikizingatiwa Bunge liliazimia kutofanya naye kazi.
Aprili 2, 2019, Bunge la Tanzania liliadhimia kutofanya kazi na CAG, Profesa Mussa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kauli yake ya kusema chombo hicho ni dhaifu wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.
Miezi kadhaa iliyopita, Profesa Assad alifanya mahojiano na idhaa hiyo nchini Marekani na kusema Bunge la Tanzania halina meno na ni dhaifu kwa sababu limeshindwa kushughulikia mapendekezo ya ripoti za ukaguzi wa hesabu za Serikali.
Hata hivyo, katika ufafanuzi wake, Bunge lilisema halitafanya kazi na CAG Assad na siyo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT).
Soma zaidi:
- Bunge laahirishwa kwa maagizo mazito watendaji serikalini
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Shughuli nyingine zitakazotekelezwa na kamati hizo katika kipindi hicho ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika udhibiti wa Ukimwi, kifua kikuu na dawa za kulevya, shughuli inayotekelezwa na Kamati ya masuala ya Ukimwi.
Pia kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Serikali kupitia wizara na taasisi zake ambapo shughuli hizi zitatekelezwa na kamati tisa za kisekta.
Kamati ya Bajeti yenyewe itapokea na kujadili taarifa ya mapendekezo ya mwongozo wa kutayarisha mpango wa maendeleo wa Taifa na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Kamati hiyo itaanza shughuli zake Oktoba 21 na kukamilisha Novemba 1 siku chache kabla ya kuanza mkutano wa 17 wa Bunge.
Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma itafanya uchambuzi wa taarifa ya Msajili wa Hazina kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma katika mashirika na taasisi mbalimbali.
Pia Kamati ya Sheria Ndogo itachambua sheria ndogo zilizowasilishwa mezani wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge.
Latest