CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii

Mwandishi Wetu 0038Hrs   Aprili 11, 2019 Safari
  • Katika ukaguzi wake alibaini madhara ya mimea ya kigeni isiyo ya kawaida katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara inayotishia utalii katika hifadhi hizo.
  • Kama ada ya adhabu kutokana na mauaji ya wanyama, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi (MINAPA) ilipaswa kukusanya 59.2 milioni badala yake ilikusanya Sh1.1 milioni tu.
  • Amebaini utofauti wa taarifa za watalii kati ya Idara ya Utalii na Idara ya Fedha katika Mamlaka ya Usimamizi wa Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad ameibua madudu yaliyofanyika katika sekta ya utalii nchini ikiwemo baadhi ya mamlaka za hifadhi za Taifa kushindwa kudhibiti vifo vya wanyama pori vinavyotokana na ajali za barabarani na kutofautiana kwa takwimu za watalii wanaotembelea Tanzania. 

Katika ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kuhusu mashirika ya umma iliyotolewa leo (Aprili 10, 2019), Prof Assad amesema katika tathmini yake  ya Mamlaka ya Usimamizi wa Eneo la Ngorongoro (NCAA) amebaini tofauti ya taarifa za watalii kati ya Idara ya Utalii na Idara ya Fedha. 

“Nilibaini kuwa Idara ya Utalii ilirekodi jumla ya watalii 1,040,618 na 787,032 kama jumla ya watalii wa nje na wa ndani mtawalia wakati Idara ya Fedha ilirekodi watalii wa nje na wa ndani 1,016,607 na 791,140, mtawalia.” amesema CAG katika ripoti hiyo. 

Hiyo ina maana kuwa Idara ya Utalii ilirekodi watalii wa nje 24,011 zaidi na wa ndani pungufu kwa 4,108 ikilinganishwa na Idara ya Fedha kati ya mwaka 2015/16 na 2017/18. 

Amesema idadi ya watalii ilitakiwa kufanana kwa idara zote kwa kuwa ina athari ya moja kwa moja kwenye mapato yaliyorekodiwa. 

“Kuna uwezekano kuwa taarifa za mapato ya utalii zimekosewa; na menejimenti ya NCAA inaweza kupewa taarifa ambazo si sahihi, hivyo kufanya maamuzi ambayo si sahihi pia,” amefafanua CAG.

Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro imekuwa kuvutio kikubwa kwa watalii wa ndani na njePicha!Mtandao.


Vifo vya wanyama pori

Akizungumzia mamlaka kushindwa kuzuia vifo vya wanyama pori, amesema Hifadhi ya Taifa ya Mikumi (MINAPA) ilishindwa kukusanya ada za adhabu kutokana na mauaji ya wanyama yaliyotokea.

“Kama ada ya adhabu kutokana na mauaji ya wanyama, MINAPA ilipaswa kukusanya Sh59.2 milioni, badala yake, ilikusanya Sh1.1 milioni tu sawa na asilimia mbili,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 

Katika Hifadhi ya MINAPA kuna barabara kuu ya Tanzania-Zambia inayokatisha katika hifadhi hiyo ambapo kwa mujibu wa ripoti ya mazingira na ulinzi hadi kufikia Machi 30, 2018, wanyama 228 waliuawa; ambapo 216 sawa na asilimia 97 waliuawa kwa njia ya ajali za barabarani. 

CAG amesema hali hiyo inaharibu mazingira na usalama wa hifadhi na  hupunguza idadi ya wanyama kupitia mauaji ya ajali za barabarani ambapo amependekeza mamlaka husika kuimarisha hatua za ufuatiliaji wa ajali za barabarani na kufanya matengenezo ya miundombinu.

Barabara kuu ya Tanzania-Zambia inayokatisha katika Hifadhi ya Mikumi. Picha! Mtandao. 


Mimea vamizi na ya kigeni kwenye Hifadhi 

Katika ukaguzi wake alibaini madhara ya mimea ya kigeni isiyo ya kawaida katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. 

Amesema vizazi vamizi vinaweza kusababisha kutokuonekana kwa wanyama katika shughuli za kitalii, kuzuia uzungukaji wa askari wakati wa shughuli za doria, kuzuia ukuaji wa baadhi ya mimea au kuua aina za mimea ya uoto asili.

Katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA), miongoni mwa aina nyingi za vizazi vamizi viletavyo maafa vilivyobainika ni magugu ya ‘Caesalpinia Decapetala’ ambayo yenye kuonekana sana ambayo yanaenea katika hifadhi hiyo kwa kasi. 

“Hifadhi ya ANAPA haina taratibu zozote zinazoendelea ili kukomesha tatizo hili. Hii inasababishwa na ukosefu wa fedha zilizotengwa kutoka makao makuu ya TANAPA kwa ajili ya kutatua tatizo hilo,” amesema Prof Assad.


Zinazohusiana:


Mkoa wa Arusha umekuwa kitovu cha shughuli za utalii nchini kutokana na kuwa eneo la kimkakati katika kuvutia watalii wa kimataifa wanaotembelea vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga za wanyama, shughuli utamaduni na maziwa.

Pia katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara (LMNP) yamebainika magugu ya ‘Acalypha Fruticosa’ ambapo yanatawala eneo kubwa la Hifadhi kiasi cha kutishia kuwapo kwa Flora na Fauna. 

Hata hivyo, hakukuwa na fedha zilizotengwa na hifadhi kwa ajili ya kuondoa vizazi vamizi hivyo ndani ya hifadhi licha ya Sh12.49 milioni zilipokelewa na LMNP kutoka makao makuu ya TANAPA zikiwa ni fedha maalum za kupambana na tatizo hilo. 

Amependekeza ANAPA na LMNP kwa kushirikiana na TANAPA kuchukua hatua stahiki za kuondoa magugu ya vizazi vamizi katika hifadhi zake ili kuchochea shughuli za utalii zitakazosaidia kuongeza mapato.

Related Post