Bunge laahirishwa kwa maagizo mazito watendaji Serikalini

Daniel Samson 0227Hrs   Novemba 17, 2018 Habari
  • Maagizo hayo ni pamoja na mikoa yote kuanzisha maonesho ya viwanda vidogo, biashara ndogo ndogo na teknolojia.
  • Mikoa mingine yapewa changamoto kuiga mifano ya Pwani, Geita na Simiyu ambayo inafanya vizuri katika sekta ya viwanda na biashara.
  • kuchukuliwa kwa hatua stahiki kudhibiti uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Dar es Salaam. Serikali yatumia fursa ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge Jijini Dodoma kutoa maagizo mbalimbali ikiwemo watendaji katika mikoa kuanzisha maonyesho ya viwanda, biashara ndogo ndogo, teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini ili kuongeza ubunifu na kuchochea ujenzi wa viwanda nchini.

Maagizo hayo yametolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa pongezi kwa mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita ambayo imefanikiwa kuratibu maonyesho hayo katika maeneo yao, jambo lililowavutia wananchi wengi kushiriki katika shughuli za ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vya uzalishaji mali.

"Napenda kuielekeza mikoa mingine iige mifano hiyo ya mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine washiriki ipasavyo katika ujenzi wa viwanda na kuleta teknolojia mpya za viwanda na sekta ya madini.

"Vilevile, niwapongeze sana wazalishaji wenye viwanda na madini pamoja na wadau wote walioshiriki kuonyesha teknolojia mbalimbali na bidhaa mpya za kilimo na madini katika maonesho hayo," amesema Majaliwa.

Amesema maonesho hayo yanafungua fursa mbalimbali kwa washiriki na wananchi kubadilishana uzoefu na kujifunza teknolojia ya kisasa inayoweza kuinua biashara na kuongeza uzalishaji viwandani.

"Ubunifu huu wa kufanya maonyesho ya viwanda ya kimkoa, kikanda na kitaifa ni jambo muhimu sana. Maonesho haya, yanatupa fursa ya kujitangaza na kutathmini hatua tuliyofikia katika utekelezaji wa ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kubaini changamoto zilizopo," amesema.

Septemba mwaka huu, mkoa wa Geita ulikuwa mwenyeji wa maonyesho ya kimataifa ya teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji wa Dhahabu yaliyofanyika katika uwanja wa CCM Kalangalala ambapo yalizikutanisha kampuni zaidi ya 150 za uchimbaji wa dhahabu, wachimbaji wadogo na kati pamoja na sekta mbalimbali zinazounganishwa katika mnyororo wa thamani wa Dhahabu.


Zinazohusiana: Waziri Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini.


Majaliwa mesema kupitia maonyesho hayo, wachimbaji wadogo waliweza kukutana na wataalamu wanaosimamia sekta ya madini na mabenki kwa lengo la kujifunza matumizi ya teknolojia mpya sambamba na kufahamu taratibu mbalimbali za kupata mikopo ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji madini.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na kukuza uchumi.

Mikoa ya Pwani na Simiyu kwa nyakati tofauti imeratibu maonyesho ya viwanda mwaka huu katika maeneo yao ikiwa ni hatua ya kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangamkia fursa za uzalishaji ili kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya kilimo na fedha.

Wachimbaji wadogo bado wanatumia teknolojia duni ya kuchenjua dhahabu jambo linalowafanya wasifaidike na madini hayo. Picha| tanzaniatoday.co.tz

Agizo lingine ni kuchukuliwa hatua stahiki kudhibiti uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Akitoa mfano Majaliwa amesema, "Miradi mingi ya maji nchini imekwama au kutoleta tija kutokana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Hivyo, niwasihi Wabunge wenzangu muwahamasishe wananchi na wadau kutoa maoni yatakayosaidia kujenga na kuboresha vema sheria zinazokusudiwa kulinda mazingira yetu pamoja na vyanzo vya maji."

Hata hivyo, Majaliwa ameweka wazi faraja aliyoipata wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani Lushoto mkoa wa Tanga na kukuta mazingira yametunzwa vizuri na uoto wa asili umehifadhiwa.

"Katika ziara yangu ya hivi karibuni wilayani Lushoto, nilifarijika mno kuona jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi wa wilaya hiyo katika kuhifadhi mazingira. Nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Lushoto na Bumbuli kwa utunzaji mzuri wa mazingira. 

"Naziagiza Halmashauri nyingine nchini ziige mfano huo mzuri wa kuhifadhi mazingira," amesema Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuhairisha bunge hadi Januari 29, 2019.

Related Post