Bunge lamtenga rasmi CAG Assad

Daniel Samson 0500Hrs   Aprili 02, 2019 Habari
  • Limedhia kutofanya kazi naye baada ya kumtia hatiani kwa kauli yake ya kusema chombo hicho ni dhaifu wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa. 
  • Azimio limetolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge Haki na Madaraka ya Bunge kwa kuliomba bunge kuridhia kutofanya kazi na CAG kwa sababu ameshusha hadhi ya bunge kwa kauli zake. 
  • Mbowe amesema uamuzi huo utalihukumu bunge kwa sababu limejipa utukufu wa Mungu.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limeadhimia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kauli yake ya kusema chombo hicho ni dhaifu wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa. 

Miezi kadhaa iliyopita, Profesa Assad alifanya mahojiano na Idhaa hiyo nchini Marekani na kusema Bunge la Tanzania halina meno na ni dhaifu kwa sababu limeshindwa kushughulikia mapendekezo ya ripoti za ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Hatua hiyo imefikiwa leo (Aprili 2, 2019) baada ya Kamati ya Maadili ya Bunge Haki na Madaraka ya Bunge kuliomba bunge kuridhia kutofanya kazi na CAG kwa sababu ameshusha hadhi ya bunge kwa kauli zake. 

Akisoma ripoti ya Kamati iliyomhoji CAG Assad Januari 21 mwaka huu, Mwenyekiti wa kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Emanuel Mwakasaka amesema wakati Profesa Assad anahojiwa na kamati hiyo alionyesha dharau na hakujutia kauli yake. 

Amesema bila kupima athari yake wakati akizungumza katika redio ya kimataifa alikosa uwajibikaji wa pamoja na hiyo ni tabia mbaya kwasababu alikataa kuomba msamaha mbele ya wajumbe wa kamati.

“Kamati ya Maadili ya Bunge tulimuuliza CAG Assad kama ataacha kulitumia neno udhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia na hakujutia kulitumia dhidi ya Bunge,” amesema Mwakasaka. 


Soma zaidi:


Amesema CAG ni mteule wa Rais na kutokana na kadhia hiyo, bunge haliko tayari kufanya kazi naye na haliko tayari kushirikiana naye kutokana na majukumu yake. 

Kutokana na uamuzi huo wa bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema azimio hilo litalihukumu bunge kwa sababu limejipa utukufu wa Mungu ambao hawakustahili.

"Azimio la kutokuwa tayari kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) litalihukumu Bunge. Bunge mnajipa utukufu ambao ni wa MUNGU pekee, azimio mnalotaka kulijadili hii leo, mmelishafanyia kazi,” amesema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.

Pia Kamati hiyo imependekeza Bunge kumsimamisha mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia tarehe ya azimio hilo kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG,Profesa Mussa Assad kuwa Bunge ni dhaifu ambapo Mdee alihojiwa na kamati hiyo kwa kauli hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameagiza Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu.

Related Post