Tanzania yaongeza kibano uwajibikaji miradi ya maendeleo

April 27, 2022 11:42 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaandaa mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi.
  • Utasaidia kupunguza ubadhirifu wa fedha za umma.

Dar es Salaam. Huenda ubadhirifu katika miradi ya maendeleo ukapungua nchini Tanzania baada ya Serikali kuandaa mwongozo maalum utakaowezesha ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema tayari Serikali imeandaa mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo unaoainisha majukumu na wajibu wa kila mdau katika usimamizi wa miradi. 

Amesema mwongozo huo ambao umesambazwa katika Wizara, Halmashauri na taasisi zote za Serikali utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi umeainisha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi. 

“Kwa kufanya hivyo, tutatoa nafasi ya kupima utendaji kwa ujumla na hivyo, kujua tumefikia wapi, tumekwama wapi na wapi tunahitaji kufanya maboresho. Lengo kuu ni kufikia malengo tarajiwa,” amesema Majaliwa.

Amesema ni vyema nchi kuwa na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotoa fursa ya kushirikisha wananchi na wadau wengine ili kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na sekta binafsi. 

Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Aprili 27, 2022) wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma amesema masuala ya ufuatiliaji na tathmini yanapaswa kupewa kipaumbele ili Taifa liendelee kupata matokeo yanayokusudiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.  

“Kwa kuzingatia kwamba nchi yetu ni sehemu ya Afrika na Dunia, tunaungana na nchi nyingine duniani katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ambayo imepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ikiwemo niliyoitaja hapo juu,” amesisitiza.

Hatua hiyo ya Serikali imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana wa ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21 ambazo zinaonyesha ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma zilizoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

CAG Charles Kichere katika ripoti hizo anapendekeza kuwepo kwa mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi ya maemdeleo.


Zinazohusiana:


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha eneo la ufuatiliaji na tathmini linaboreshwa na kusimamiwa ipasavyo.

Amesema mwaka 2008 Serikali kupitia Programu ya Maboresho katika Utumishi wa Umma, iliimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmni kwa kuboresha miundo ya Wizara zote na kuanzisha sehemu za ufuatiliaji na tathmini chini ya Idara za Sera na Mipango. 

“Hii ilikuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kunakuwepo na ufuatiliaji wa karibu katika utekelezaji wa miradi, kuhakikisha matumizi  ya rasilimali za fedha kwa malengo kusudiwa, kuongeza uwajibikaji na kujifunza kutokana na yale tunayoyatekeleza katika mipango ya kifaifa,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ufuatiliaji na Tathmini (TanEA), Profesa Deus Ngaruko amesema malengo makuu ya taasisi hiyo ni kujenga na kuendeleza uwezo wa ufuatiliaji na tathmini ya ndani ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema pamoja na mambo mengine, pia kongamano hilo la siku mbili litatoa fursa ya kujifunza mbinu na mambo mapya kwenye tasnia ya ufuatiliaji na tathmini ili Watanzania waweze kujengewa uwezo wa kufanya ufuatilia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW