Kamati za Bunge kukutana kujiandaa na mkutano wa 18
- Pamoja na mambo mengine zitachambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma.
Dar es salaam. Kamati za Kudumu za Bunge la Tanzania zinatarajia kuanza vikao vyake Januari 6 hadi 24, 2025 jijini Dodoma, ambapo pamoja na mengine zitachambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma leo Januari 3, 2025, vikao hivyo vinatangulia mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza siku ya Jumanne Januari 28, 2025.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa katika kipindi hicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) zitatangulia kuanza vikao Januari 6, 2025, huku Kamati zilizosalia zikianza vikao Januari 13, 2025.
Kamati ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC) itapitia na kutathmini taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ili kubaini ufanisi na kuhakikisha uwekezaji unazingatia kanuni bora za biashara.
Katika vikao hivyo, kamati mbili zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, zitachambua Taarifa ya CAG kuhusu hesabu za wizara, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2023.
“Kamati nne, ambazo ni Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Ustawi wa Jamii, Kamati ya Maji na Mazingira na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), zitapitia na kuchambua miswada ya sheria iliyokwisha wasilishwa,” imebainisha taarifa hiyo.
Aidha, Kamati ya Sheria ndogo itajadili sheria ndogo zilizowasilishwa kwenye mikutano ya 14 na 15 ya Bunge, ili kuhakikisha zinakidhi matakwa ya kisheria na maslahi ya wananchi.
Taarifa ya Bunge imeeleza kuwa kamati 11 za kisekta zitapokea na kuchambua taarifa mbalimbali kuhusu utendaji wa Serikali na taasisi zake ambapo kamati ya bajeti itajikita katika kutathmini utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka, cha Julai hadi Desemba 2024.
Shughuli za Bunge zilihairishwa kwenye mkutano wa 17, kikao cha tisa, Novemba 8 na Naibu Spika, Mussa Azzan Zungu na zinatarajiwa kuendelea tena rasmi Jumanne ya Januari 28, 2025.