Unavyoweza kujikinga na ugonjwa wa monkeypox
- Vaa barakoa unapomhudumia mgonjwa.
- Nawa kwa maji tiririka na sabuni na tumia kitakasa mikono.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza ugonjwa wa monkeypox kuwa tishio la afya umma duniani, shirika hilo limeanisha njia za kujilinda na ugonjwa huo ulioenea sehemu mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus aliyekuwa akitoa kuhusu ugonjwa huo hivi karibuni amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa huo ni tishio na umeenea zaidi kwenye nchi za Ulaya.
“Mlipuko umeendelea kukua na hadi sasa kuna wagonjwa zaidi ya 16,000 kutoka nchi 45 na vifo vya watu watano,”alisema Dk Tedros July 23, alipozungumza na wanahabari jijini Geneva, Uswisi
Ugonjwa wa monkeypox ni nini
Kwa mujibu wa WHO, Monkeypox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya orthopox vinavyotoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, kitaalamu Zoonotic au Zoonosis.
Ugonjwa huu umepewa jina hilo kwa sababu uligunduliwa kwa nyani kadhaa wa maabara mwaka wa 1958 na baadaye kumpata kijana wa miaka tisa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).
Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa, maumivu makali ya kichwa, misuli, mgongo, kuishiwa nguvu, kuvimba mitoki, na vipele au vidonda kwenye ngozi ya uso, nyayo za miguu au viganja vya mikono.
WHO inasema dalili za ugonjwa huu huchukua wiki mbili hadi nne na huondoka zenyewe bila matibabu, ila unaweza kusababisha kifo kwa baadhi ya makundi ya watu hususani watoto wachanga na watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Soma zaidi:
-
Wagonjwa wa monkeypox wazidi kuongezeka
-
Ni uzushi: Huwezi kupata maambukizi ya Corona kwa kuchangia damu
- Ukweli kuhusu maiti kuambukiza Corona
Jinsi unavyoweza kujikinga na ugonjwa wa Monkeypox
WHO imesema Unaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa monkeypox kwa kufuata hatua zifuatazo:
1. Punguza kukutana na watu unaowashuku kuwa wana ugonjwa huo au ikiwa wana maambukizi yaliyothibitishwa.
Iwapo unahitaji kugusana kimwili na mtu aliye na hali hii kwa sababu ni mfanyakazi wa afya au mnaishi pamoja, mhamasishe mtu aliyeambukizwa ajitenge na kufunika michubuko yoyote ya ngozi kama anaweza (kwa mfano, kwa kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili).
2.Vaa barakoa unapokuwa karibu na mtu aliye na ugonjwa wa monkeypox, hasa ikiwa anakohoa au ana vidonda mdomoni. Pia ikiwa ni lazima uguse nguo au kitanda cha mtu aliyeambukizwa.
3.Epuka kugusana ngozi kwa ngozi na mgonjwa wa monkeypox. Ikiwa una mgusano wowote wa moja kwa moja vaa glavu zinazoweza kutupwa baada ya kutumika.
4.Nawa mikono yako mara kwa mara kwa sabuni na maji au tumia kitakasa mikono, hasa baada ya kugusana na mtu aliyeambukizwa, au kugusa mavazi yake (pamoja na shuka na taulo) au vitu vingine kama vyombo au sahani.
5. Fua nguo, taulo, shuka, na vyombo vya chakula vya mtu aliyeambukizwa kwa maji ya moto na sabuni. Safisha ipasavyo na kuua vijidudu kwenye sehemu zozote zilizochafuliwa na tupa taka zilizochafuliwa (kama vile mavazi).
Latest
